Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 7

7
Onyo dhidi ya mwanamke mzinzi
1Mwanangu, shika maneno yangu
na kuzihifadhi amri zangu ndani yako.
2Shika amri zangu nawe utaishi;
linda mafundisho yangu kama mboni ya jicho lako.
3Yafunge katika vidole vyako;
yaandike katika kibao cha moyo wako.
4Mwambie hekima, “Wewe ni dada yangu,”
uite ufahamu jamaa yako;
5watakuepusha na mwanamke mzinzi,
kutokana na mwanamke mpotovu
na maneno yake ya kubembeleza.
6Kwenye dirisha la nyumba yangu
nilitazama nje kupitia upenyo
kwenye mwimo wa dirisha.
7Niliona miongoni mwa wajinga,
nikagundua miongoni mwa wanaume vijana,
kijana asiye na akili.
8Alikuwa akishuka njiani karibu na pembe ya kwake,
akielekea kwenye nyumba ya huyo mwanamke
9wakati wa machweo, jua likipungua nuru yake,
giza la usiku lilipokuwa likiingia.
10Ndipo huyo mwanamke akatoka kumlaki,
hali amevaa kama kahaba akiwa na nia ya hila.
11(Ni mwanamke mwenye makelele na mkaidi,
miguu yake haitulii nyumbani;
12mara kwenye barabara za mji,
mara kwenye viwanja vikubwa,
kwenye kila pembe huvizia.)
13Huyo mwanamke alimkumbatia kijana na kumbusu,
na kwa uso usio na haya akamwambia:
14“Nina sadaka za amani nyumbani;
leo nimetimiza nadhiri zangu.
15Kwa hiyo nimetoka nje kukulaki;
nimekutafuta na nimekupata!
16Nimetandika kitanda changu
kwa kitani za rangi kutoka Misri.
17Nimetia manukato kitanda changu
kwa manemane, udi na mdalasini.
18Njoo, tuzame katika mapenzi hadi asubuhi;
tujifurahishe wenyewe kwa mapenzi!
19Mume wangu hayupo nyumbani;
ameenda safari ya mbali.
20Amechukua mkoba uliojazwa fedha
na hatakuwa nyumbani karibuni.”
21Kwa maneno laini yule mwanamke akampotosha;
alimshawishi kwa maneno yake laini.
22Mara huyo kijana alimfuata yule mwanamke
kama fahali aendaye machinjoni,
kama kulungu aingiaye kwenye kitanzi,
23hadi mshale umchome ini lake,
kama ndege anayenaswa kwenye mtego,
bila kujua itamgharimu maisha yake.
24Sasa basi wanangu, nisikilizeni;
sikilizeni kwa makini nisemalo.
25Usiruhusu moyo wako ugeukie njia za huyo mwanamke,
wala usitangetange katika mapito yake.
26Aliowaangusha ni wengi;
aliowachinja ni kundi kubwa.
27Nyumba yake ni njia kuu iendayo kaburini#7:27 Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol.,
ielekeayo chini kwenye vyumba vya mauti.

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 7: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia