Methali 8:22-36
Methali 8:22-36 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mwenyezi-Mungu aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, zama za zama kabla ya kuwako kitu chochote. Nilifanywa mwanzoni mwa nyakati, nilikuwako kabla ya dunia kuanza. Nilizaliwa kabla ya vilindi vya bahari, kabla ya chemchemi zibubujikazo maji. Kabla ya milima haijaumbwa, na vilima kusimamishwa mahali pake, mimi nilikuwako tayari. Kabla Mungu hajaumba dunia na mashamba yake, wala chembe za kwanza za mavumbi ya dunia. Nilikuwako wakati alipoziweka mbingu, wakati alipopiga duara juu ya bahari; wakati alipoimarisha mawingu mbinguni, alipozifanya imara chemchemi za bahari; wakati alipoiwekea bahari mpaka wake, maji yake yasije yakavunja amri yake; wakati alipoiweka misingi ya dunia. Nilikuwa pamoja naye kama fundi stadi, nilikuwa furaha yake kila siku, nikishangilia mbele yake daima, nikifurahia dunia na wakazi wake, na kupendezwa kuwa pamoja na wanadamu. “Sasa basi wanangu, nisikilizeni: Heri wale wanaofuata njia zangu. Sikilizeni mafunzo mpate hekima, wala msiyakatae. Heri mtu anayenisikiliza, anayekaa kila siku mlangoni pangu, anayekesha karibu na milango yangu. Anayenipata mimi amepata uhai, amepata upendeleo kwa Mwenyezi-Mungu. Asiyenipata anajidhuru mwenyewe; wote wanaonichukia wanapenda kifo.”
Methali 8:22-36 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale. Nilitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijakuwako dunia. Wakati havijakuwapo vilindi nilizaliwa, Wakati hazijakuwapo chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nilizaliwa. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala mashamba Wala chanzo cha udongo wa dunia; Alipozithibitisha mbingu nilikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari; Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu; Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi; Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake; Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu. Basi, wanangu, nisikilizeni sasa; Maana heri hao wazishikao amri zangu. Sikieni mafundisho, mpate hekima, Wala msiikatae. Ana heri mtu yule anisikilizaye, Akisubiri sikuzote malangoni pangu, Akingoja penye vizingiti vya milango yangu. Maana yeye anionaye mimi aona uzima, Naye atapata kibali kwa BWANA. Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, Na wao wanichukiao hupenda mauti.
Methali 8:22-36 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale. Nalitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde Wala chanzo cha mavumbi ya dunia; Alipozithibitisha mbingu nalikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari; Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu; Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi; Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake; Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu. Basi, wanangu, nisikilizeni sasa; Maana heri hao wazishikao amri zangu. Sikieni mafundisho, mpate hekima, Wala msiikatae. Ana heri mtu yule anisikilizaye, Akisubiri sikuzote malangoni pangu, Akingoja penye vizingiti vya milango yangu. Maana yeye anionaye mimi aona uzima, Naye atapata kibali kwa BWANA. Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, Na wao wanichukiao hupenda mauti.
Methali 8:22-36 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“BWANA aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, kabla ya matendo yake ya zamani; niliteuliwa tangu milele, tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa. Wakati hazijakuwepo bahari, nilikwishazaliwa, wakati hazijakuwepo chemchemi zilizojaa maji; kabla milima haijawekwa mahali pake, kabla vilima havijakuwepo, nilikwishazaliwa, kabla hajaumba dunia wala mashamba yake au vumbi lolote la dunia. Nilikuwepo alipoziweka mbingu mahali pake, wakati alichora mstari wa upeo wa macho juu ya uso wa kilindi, wakati aliweka mawingu juu na kuziweka imara chemchemi za bahari, wakati aliiwekea bahari mpaka wake ili maji yasivunje agizo lake, na wakati aliweka misingi ya dunia. Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake. Nilijazwa na furaha siku baada ya siku, nikifurahi daima mbele zake, nikifurahi katika dunia yake yote nami nikiwafurahia wanadamu. “Basi sasa wanangu, nisikilizeni; heri wale wanaozishika njia zangu. Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima; msiyapuuze. Heri mtu yule anisikilizaye mimi, akisubiri siku zote malangoni mwangu, akingoja kwenye vizingiti vya mlango wangu. Kwa maana yeyote anipataye mimi amepata uzima na kujipatia kibali kutoka kwa BWANA. Lakini yeyote ashindwaye kunipata hujiumiza mwenyewe; na wote wanichukiao mimi hupenda mauti.”