Methali 8:22-36
Methali 8:22-36 BHN
“Mwenyezi-Mungu aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, zama za zama kabla ya kuwako kitu chochote. Nilifanywa mwanzoni mwa nyakati, nilikuwako kabla ya dunia kuanza. Nilizaliwa kabla ya vilindi vya bahari, kabla ya chemchemi zibubujikazo maji. Kabla ya milima haijaumbwa, na vilima kusimamishwa mahali pake, mimi nilikuwako tayari. Kabla Mungu hajaumba dunia na mashamba yake, wala chembe za kwanza za mavumbi ya dunia. Nilikuwako wakati alipoziweka mbingu, wakati alipopiga duara juu ya bahari; wakati alipoimarisha mawingu mbinguni, alipozifanya imara chemchemi za bahari; wakati alipoiwekea bahari mpaka wake, maji yake yasije yakavunja amri yake; wakati alipoiweka misingi ya dunia. Nilikuwa pamoja naye kama fundi stadi, nilikuwa furaha yake kila siku, nikishangilia mbele yake daima, nikifurahia dunia na wakazi wake, na kupendezwa kuwa pamoja na wanadamu. “Sasa basi wanangu, nisikilizeni: Heri wale wanaofuata njia zangu. Sikilizeni mafunzo mpate hekima, wala msiyakatae. Heri mtu anayenisikiliza, anayekaa kila siku mlangoni pangu, anayekesha karibu na milango yangu. Anayenipata mimi amepata uhai, amepata upendeleo kwa Mwenyezi-Mungu. Asiyenipata anajidhuru mwenyewe; wote wanaonichukia wanapenda kifo.”