Mithali 8:22-36
Mithali 8:22-36 NEN
“BWANA aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, kabla ya matendo yake ya zamani; niliteuliwa tangu milele, tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa. Wakati hazijakuwepo bahari, nilikwishazaliwa, wakati hazijakuwepo chemchemi zilizojaa maji; kabla milima haijawekwa mahali pake, kabla vilima havijakuwepo, nilikwishazaliwa, kabla hajaumba dunia wala mashamba yake au vumbi lolote la dunia. Nilikuwepo alipoziweka mbingu mahali pake, wakati alichora mstari wa upeo wa macho juu ya uso wa kilindi, wakati aliweka mawingu juu na kuziweka imara chemchemi za bahari, wakati aliiwekea bahari mpaka wake ili maji yasivunje agizo lake, na wakati aliweka misingi ya dunia. Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake. Nilijazwa na furaha siku baada ya siku, nikifurahi daima mbele zake, nikifurahi katika dunia yake yote nami nikiwafurahia wanadamu. “Basi sasa wanangu, nisikilizeni; heri wale wanaozishika njia zangu. Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima; msiyapuuze. Heri mtu yule anisikilizaye mimi, akisubiri siku zote malangoni mwangu, akingoja kwenye vizingiti vya mlango wangu. Kwa maana yeyote anipataye mimi amepata uzima na kujipatia kibali kutoka kwa BWANA. Lakini yeyote ashindwaye kunipata hujiumiza mwenyewe; na wote wanichukiao mimi hupenda mauti.”