Zaburi 27:1-14
Zaburi 27:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? BWANA ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini. Neno Moja nimelitaka kwa BWANA, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa BWANA Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa BWANA, Na kutafakari hekaluni mwake. Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba. Na sasa kichwa changu kitainuka Juu ya adui zangu wanaonizunguka. Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake; Nitaimba, naam, nitamhimidi BWANA. Ee BWANA, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu. Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia, BWANA, uso wako nitautafuta. Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali BWANA atanikaribisha kwake. Ee BWANA, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea; Usinitie katika nia ya watesi wangu; Maana mashahidi wa uongo wameniondokea, Nao watoao jeuri kama pumzi. Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA Katika nchi ya walio hai. Umngoje BWANA, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA.
Zaburi 27:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu, ni nani nitakayemwogopa? Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu, sitamwogopa mtu yeyote. Waovu wakinishambulia, na kutaka kuniangamiza, hao wapinzani wangu watajikwaa na kuanguka. Hata jeshi likinizunguka, moyo wangu hautaogopa kitu; hata nikikabiliwa na vita, bado nitakuwa na tumaini. Jambo moja nimemwomba Mwenyezi-Mungu, nalo ndilo ninalolitafuta: Nikae nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu siku zote za maisha yangu; niuone uzuri wake Mwenyezi-Mungu, na kutafuta maongozi yake hekaluni mwake. Siku ya taabu atanificha bandani mwake; atanificha katika hema lake, na kunisalimisha juu ya mwamba. Nami kwa fahari nitaangalia juu ya maadui zangu wanaonizunguka. Nitamtolea tambiko kwa shangwe hekaluni mwake, nitaimba na kumshangilia Mwenyezi-Mungu. Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, ninapokulilia, unionee huruma na kunijibu. Moyo wangu waniambia: “Njoo umtafute Mungu!” Basi, naja kwako, ee Mwenyezi-Mungu. Usiache kuniangalia kwa wema. Usinikatae kwa hasira mimi mtumishi wako; wewe umekuwa daima msaada wangu. Usinitupe wala usiniache, ee Mungu Mwokozi wangu. Hata kama wazazi wangu wakinitupa, Mwenyezi-Mungu atanipokea kwake. Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu; uniongoze katika njia iliyo sawa, kwa sababu ya maadui zangu. Usiniache maadui wanitende wapendavyo; maana mashahidi wa uongo wananikabili, nao wanatoa vitisho vya ukatili. Naamini nitauona wema wake Mwenyezi-Mungu katika makao ya walio hai. Mtegemee Mwenyezi-Mungu! Uwe na moyo, usikate tamaa! Naam, mtegemee Mwenyezi-Mungu!
Zaburi 27:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? BWANA ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumainia BWANA. Neno moja nimelitaka kwa BWANA, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa BWANA Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa BWANA, Na kutafakari hekaluni mwake. Maana atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba. Na sasa kichwa changu kitainuka Juu ya adui zangu wanaonizunguka. Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake; Nitaimba, naam, nitamhimidi BWANA. Ee BWANA, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu. Uliposema, “Nitafuteni uso wangu,” Moyo wangu umekuambia, BWANA, uso wako nitautafuta. Usinifiche uso wako, Usimkatalie mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Hata baba yangu na mama yangu wakiniacha, Bali BWANA atanikaribisha kwake. Ee BWANA, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea; Usinitie katika nia ya watesi wangu; Maana mashahidi wa uongo wamenijia, Nao watoao jeuri kama pumzi. Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA Katika nchi ya walio hai. Umtumainie BWANA, uwe imara, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA.
Zaburi 27:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? BWANA ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? Waovu watakaposogea dhidi yangu ili wanile nyama yangu, adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia, watajikwaa na kuanguka. Hata jeshi linizunguke pande zote, moyo wangu hautaogopa; hata vita vitokee dhidi yangu, hata hapo nitakuwa na ujasiri. Jambo moja ninamwomba BWANA, hili ndilo ninalolitafuta: niweze kukaa nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa BWANA na kumtafuta hekaluni mwake. Kwa kuwa siku ya shida, atanihifadhi salama katika maskani yake, atanificha uvulini mwa hema yake na kuniweka juu kwenye mwamba. Kisha kichwa changu kitainuliwa juu ya adui zangu wanaonizunguka. Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe; nitamwimbia BWANA na kumsifu. Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee BWANA, unihurumie na unijibu. Moyo wangu unasema kuhusu wewe, “Utafute uso wake!” Uso wako, BWANA “Nitautafuta.” Usinifiche uso wako, usimkatae mtumishi wako kwa hasira; wewe umekuwa msaada wangu. Usinikatae wala usiniache, Ee Mungu Mwokozi wangu. Hata kama baba yangu na mama wakiniacha, BWANA atanipokea. Nifundishe njia yako, Ee BWANA, niongoze katika njia iliyonyooka kwa sababu ya watesi wangu. Usiniachilie kwa nia za adui zangu, kwa maana mashahidi wa uongo wameinuka dhidi yangu, wakipumua ujeuri. Nami bado nina tumaini hili: nitauona wema wa BWANA katika nchi ya walio hai. Mngojee BWANA, uwe hodari na mwenye moyo mkuu, nawe, umngojee BWANA.