Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 27:1-14

Zaburi 27:1-14 SRUV

BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? BWANA ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumainia BWANA. Neno moja nimelitaka kwa BWANA, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa BWANA Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa BWANA, Na kutafakari hekaluni mwake. Maana atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba. Na sasa kichwa changu kitainuka Juu ya adui zangu wanaonizunguka. Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake; Nitaimba, naam, nitamhimidi BWANA. Ee BWANA, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu. Uliposema, “Nitafuteni uso wangu,” Moyo wangu umekuambia, BWANA, uso wako nitautafuta. Usinifiche uso wako, Usimkatalie mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Hata baba yangu na mama yangu wakiniacha, Bali BWANA atanikaribisha kwake. Ee BWANA, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea; Usinitie katika nia ya watesi wangu; Maana mashahidi wa uongo wamenijia, Nao watoao jeuri kama pumzi. Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA Katika nchi ya walio hai. Umtumainie BWANA, uwe imara, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA.

Soma Zaburi 27