Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 27:1-14

Zaburi 27:1-14 NEN

BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? BWANA ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? Waovu watakaposogea dhidi yangu ili wanile nyama yangu, adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia, watajikwaa na kuanguka. Hata jeshi linizunguke pande zote, moyo wangu hautaogopa; hata vita vitokee dhidi yangu, hata hapo nitakuwa na ujasiri. Jambo moja ninamwomba BWANA, hili ndilo ninalolitafuta: niweze kukaa nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa BWANA na kumtafuta hekaluni mwake. Kwa kuwa siku ya shida, atanihifadhi salama katika maskani yake, atanificha uvulini mwa hema yake na kuniweka juu kwenye mwamba. Kisha kichwa changu kitainuliwa juu ya adui zangu wanaonizunguka. Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe; nitamwimbia BWANA na kumsifu. Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee BWANA, unihurumie na unijibu. Moyo wangu unasema kuhusu wewe, “Utafute uso wake!” Uso wako, BWANA “Nitautafuta.” Usinifiche uso wako, usimkatae mtumishi wako kwa hasira; wewe umekuwa msaada wangu. Usinikatae wala usiniache, Ee Mungu Mwokozi wangu. Hata kama baba yangu na mama wakiniacha, BWANA atanipokea. Nifundishe njia yako, Ee BWANA, niongoze katika njia iliyonyooka kwa sababu ya watesi wangu. Usiniachilie kwa nia za adui zangu, kwa maana mashahidi wa uongo wameinuka dhidi yangu, wakipumua ujeuri. Nami bado nina tumaini hili: nitauona wema wa BWANA katika nchi ya walio hai. Mngojee BWANA, uwe hodari na mwenye moyo mkuu, nawe, umngojee BWANA.