Zaburi 27:1-14
Zaburi 27:1-14 BHN
Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu, ni nani nitakayemwogopa? Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu, sitamwogopa mtu yeyote. Waovu wakinishambulia, na kutaka kuniangamiza, hao wapinzani wangu watajikwaa na kuanguka. Hata jeshi likinizunguka, moyo wangu hautaogopa kitu; hata nikikabiliwa na vita, bado nitakuwa na tumaini. Jambo moja nimemwomba Mwenyezi-Mungu, nalo ndilo ninalolitafuta: Nikae nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu siku zote za maisha yangu; niuone uzuri wake Mwenyezi-Mungu, na kutafuta maongozi yake hekaluni mwake. Siku ya taabu atanificha bandani mwake; atanificha katika hema lake, na kunisalimisha juu ya mwamba. Nami kwa fahari nitaangalia juu ya maadui zangu wanaonizunguka. Nitamtolea tambiko kwa shangwe hekaluni mwake, nitaimba na kumshangilia Mwenyezi-Mungu. Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, ninapokulilia, unionee huruma na kunijibu. Moyo wangu waniambia: “Njoo umtafute Mungu!” Basi, naja kwako, ee Mwenyezi-Mungu. Usiache kuniangalia kwa wema. Usinikatae kwa hasira mimi mtumishi wako; wewe umekuwa daima msaada wangu. Usinitupe wala usiniache, ee Mungu Mwokozi wangu. Hata kama wazazi wangu wakinitupa, Mwenyezi-Mungu atanipokea kwake. Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu; uniongoze katika njia iliyo sawa, kwa sababu ya maadui zangu. Usiniache maadui wanitende wapendavyo; maana mashahidi wa uongo wananikabili, nao wanatoa vitisho vya ukatili. Naamini nitauona wema wake Mwenyezi-Mungu katika makao ya walio hai. Mtegemee Mwenyezi-Mungu! Uwe na moyo, usikate tamaa! Naam, mtegemee Mwenyezi-Mungu!