Zaburi 65:1-13
Zaburi 65:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Wastahili sifa, ee Mungu, huko Siyoni, watu watakutimizia wewe ahadi zao, maana wewe wajibu sala zetu. Binadamu wote watakujia wewe. Tunapolemewa na makosa yetu, wewe mwenyewe watusamehe. Heri wale unaowachagua na kuwaleta karibu, waishi katika maskani yako. Sisi tutatoshelezwa na mema ya nyumba yako; mema ya hekalu lako takatifu. Kwa matendo yako makuu watuitikia na kutuokoa, ewe Mungu wa wokovu wetu; wewe ndiwe tumaini la viumbe vyote, duniani kote na mbali baharini. Kwa nguvu yako uliisimika milima mahali pake. Wewe una nguvu mno! Watuliza mshindo wa bahari na wa mawimbi yake, wakomesha ghasia za watu. Ulimwengu wote washangazwa na matendo yako. Wasababisha furaha kila mahali, toka mashariki hata magharibi. Wewe waitunza nchi kwa kuinyeshea mvua, waijalia rutuba na kuistawisha; mto wako umejaa maji tele, waifanikisha nchi na kuipatia mavuno. Hivi ndivyo uitengenezavyo nchi: Mashamba wayanyeshea mvua kwa wingi, na kuyalowanisha kwa maji; ardhi wailainisha kwa manyunyu, na kuibariki mimea ichipue. Wautunukia mwaka wote mema yako, kila ulipopitia pamejaa fanaka. Mbuga za majani zimejaa mifugo, milima nayo imejaa furaha. Malisho yamejaa kondoo, mabonde yamefunikwa kwa ngano. Kila kitu kinashangilia kwa furaha.
Zaburi 65:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee Mungu, wastahili sifa katika Sayuni, Na kwako Wewe itaondolewa nadhiri. Wewe usikiaye maombi, Wote wenye mwili watakujia. Tutakapozidiwa na matendo maovu Wewe utatuondolea uovu wetu. Heri mtu yule umchaguaye, Na kumkaribisha akae nyuani mwako. Na tushibe wema wa nyumba yako, Patakatifu pa hekalu lako. Kwa mambo ya kutisha utatujibu, Katika haki, Ee Mungu wa wokovu wetu. Wewe uliye tumaini la miisho yote ya dunia, Na la bahari iliyo mbali sana, Milima waiweka imara kwa nguvu zako, Huku ukijifunga uweza kama mshipi. Watuliza kuvuma kwa bahari, Kuvuma kwa mawimbi yake, Na ghasia za watu; Kwa hiyo wakaao mbali kabisa huogopa ishara zako; Milango ya asubuhi na jioni waifurahisha. Umeijia nchi na kuisitawisha, Umeitajirisha sana; Mto wa Mungu umejaa maji; Wawapa watu nafaka Maana ndiwe uitengenezaye ardhi. Matuta yake wayajaza maji; Wapasawazisha palipoinuka, Wailainisha nchi kwa manyunyu; Waibariki mimea yake. Umeuvika mwaka taji la wema wako; Mapito yako yadondoza unono. Huyadondokea malisho ya nyikani, Na vilima vimejawa na furaha. Na malisho yamejawa na kondoo, Na mabonde yamepambwa nafaka, Yanashangilia, na kuimba pamoja kwa shangwe.
Zaburi 65:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee Mungu, sifa zakulaiki katika Sayuni, Na kwako Wewe itaondolewa nadhiri. Wewe usikiaye kuomba, Wote wenye mwili watakujia. Ingawa maovu mengi yanamshinda, Wewe utayafunika maasi yetu. Heri mtu yule umchaguaye, Na kumkaribisha akae nyuani mwako. Na tushibe wema wa nyumba yako, Patakatifu pa hekalu lako. Kwa mambo ya kutisha utatujibu, Katika haki, Ee Mungu wa wokovu wetu. Wewe uliye tumaini la miisho yote ya dunia, Na la bahari iliyo mbali sana, Milima waiweka imara kwa nguvu zako, Huku ukijifunga uweza kama mshipi. Wautuliza uvumi wa bahari, Uvumi wa mawimbi yake, Na ghasia ya mataifa; Kwa hiyo wakaao mbali kabisa huogopa ishara zako; Milango ya asubuhi na jioni waifurahisha. Umeijilia nchi na kuisitawisha, Umeitajirisha sana; Mto wa Mungu umejaa maji; Wawaruzuku watu nafaka Maana ndiwe uitengenezaye ardhi. Matuta yake wayajaza maji; Wapasawazisha palipoinuka, Wailainisha nchi kwa manyunyu; Waibariki mimea yake. Umeuvika mwaka taji ya wema wako; Mapito yako yadondoza unono. Huyadondokea malisho ya nyikani, Na vilima vyajifunga furaha. Na malisho yamevikwa kondoo, Na mabonde yamepambwa nafaka, Yanashangilia, naam, yanaimba.
Zaburi 65:1-13 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ee Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni; kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa. Ewe usikiaye maombi, watu wote watakuja kwako wewe. Tulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi, wewe ulisamehe makosa yetu. Heri wale uliowachagua na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako! Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako, mema ya Hekalu lako takatifu. Unatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki, Ee Mungu Mwokozi wetu, tumaini la miisho yote ya duniani na la bahari zilizo mbali sana, uliyeumba milima kwa uwezo wako, ukiwa umejivika nguvu, uliyenyamazisha dhoruba za bahari, ngurumo za mawimbi yake, na ghasia za mataifa. Wale wanaoishi mbali sana wanaogopa maajabu yako, kule asubuhi ipambazukiapo na kule jioni inakofifilia umeziita nyimbo za furaha. Waitunza nchi na kuinyeshea, waitajirisha kwa wingi. Vijito vya Mungu vimejaa maji ili kuwapa watu nafaka, kwa maana wewe umeviamuru. Umeilowesha mifereji yake na kusawazisha kingo zake; umeilainisha kwa manyunyu na kuibariki mimea yake. Umeuvika mwaka taji la baraka, magari yako yanafurika kwa wingi. Mbuga za majani za jangwani umezineemesha; vilima vimevikwa furaha. Malisho yamejaa makundi ya wanyama, na mabonde yamepambwa kwa mavuno; vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba.