Ufunuo 11:15-19
Ufunuo 11:15-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele. Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vya enzi vyao wakaanguka kifudifudi, wakamsujudia Mungu wakisema, Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa sababu umeutwaa uweza wako ulio mkuu, na kumiliki. Na mataifa walikasirika, hasira yako nayo ikaja, na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa, na wa kuwapa thawabu yao watumishi wako manabii na watakatifu, na hao walichao jina lako, wadogo kwa wakubwa, na wa kuwaharibu hao waiharibuo nchi. Kisha hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la Agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua kubwa ya mawe.
Ufunuo 11:15-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele. Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vya enzi vyao wakaanguka kifulifuli, wakamsujudia Mungu wakisema, Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa sababu umeutwaa uweza wako ulio mkuu, na kumiliki. Na mataifa walikasirika, hasira yako nayo ikaja, na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa, na wa kuwapa thawabu yao watumwa wako manabii na watakatifu, na hao walichao jina lako, wadogo kwa wakubwa, na wa kuwaharibu hao waiharibuo nchi. Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua ya mawe nyingi sana.
Ufunuo 11:15-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yule malaika wa saba akaipiga tarumbeta yake, pakawa na sauti kubwa mbinguni iliyosema: “Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atatawala milele na milele.” Nao wale wazee ishirini na wanne, waliokuwa wameketi mbele za Mungu, kwenye viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, wakisema: “Tunakushukuru, BWANA Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa kuwa umetwaa uweza wako mkuu na ukaanza kutawala. Mataifa walikasirika nao wakati wa ghadhabu yako umewadia. Wakati umewadia wa kuwahukumu waliokufa na kuwapa thawabu watumishi wako manabii na watakatifu wako pamoja na wale wote wanaoliheshimu Jina lako, wakubwa kwa wadogo: na kuwaangamiza wale wanaoiangamiza dunia.” Ndipo hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana humo ndani. Kukatokea mianga ya umeme wa radi, ngurumo, sauti za radi, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.
Ufunuo 11:15-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, malaika wa saba akapiga tarumbeta yake. Na sauti kuu zikasikika mbinguni zikisema, “Sasa ufalme wa ulimwengu ni wa Bwana wetu na Kristo wake. Naye atatawala milele na milele!” Kisha, wale wazee ishirini na wanne walioketi mbele ya Mungu katika viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, wakisema: “Tunakushukuru ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu, uliyeko na uliyekuwako! Maana umetumia nguvu yako kuu, ukaanza kutawala! Watu wa mataifa waliwaka hasira, lakini ghadhabu yako imefika, naam wakati wa kuwahukumu wafu. Ndio wakati wa kuwatuza watumishi wako manabii, watakatifu na wote wanaolitukuza jina lako, wakubwa kwa wadogo. Ni wakati wa kuwaangamiza waangamizi wa dunia.” Kisha hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana hekaluni mwake. Kukatokea umeme, sauti, ngurumo, tetemeko la ardhi, na mvua kubwa ya mawe.