Waroma 2:17-29
Waroma 2:17-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Na wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia sheria na kujivunia kuwa wa Mungu; kwa njia ya sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema; wewe unajiona kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga kwa wale walio gizani; unajiona kuwa mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa wale wasiokomaa bado. Unayo katika sheria picha kamili ya elimu na ukweli. Basi, wewe unawafundisha wengine; kwa nini hujifundishi wewe mwenyewe? Unawahubiria wengine wasiibe, lakini kumbe wewe mwenyewe unaiba. Unasema: “Msizini,” na huku wewe unazini; unachukia sanamu za miungu hali wewe unajitajirisha kwa kuiba katika nyumba za miungu. Kwa kujigamba ati unayo sheria ya Mungu, je huoni kwamba kwa kuivunja sheria unamdharau Mungu? Kama vile Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Watu wa mataifa mengine wamelikufuru jina la Mungu kwa sababu yenu nyinyi Wayahudi!” Kutahiriwa kwako kutakuwa na maana kama ukiitii sheria. Lakini kama unaivunja sheria, basi, ni afadhali ungalibaki bila kutahiriwa. Kama mtu wa mataifa mengine ambaye hakutahiriwa akitimiza matakwa ya sheria, hakika atafikiriwa kana kwamba ametahiriwa. Watu wa mataifa mengine watakuhukumu wewe Myahudi kama ukiivunja sheria, ingawaje unayo maandishi ya sheria na umetahiriwa, hali wao wanaitii sheria ingawa hawakutahiriwa. Ndiyo kusema, si kila anayeonekana kwa nje kuwa Myahudi ni Myahudi wa kweli, wala mtu hawi Myahudi wa kweli ati kwa kuwa ametahiriwa kimwili. Myahudi wa kweli ni yule aliye Myahudi kwa ndani, yaani yule ambaye ametahiriwa moyoni. Hili ni jambo la Roho, na si jambo la maandishi ya sheria. Mtu wa namna hiyo anapata sifa, si kutoka kwa watu, bali kutoka kwa Mungu.
Waroma 2:17-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini wewe, ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea torati, na kujisifu katika Mungu, na kuyajua mapenzi yake, na kuyakubali mambo yaliyo bora, nawe umeelimishwa katika torati, na kujua hakika ya kuwa wewe mwenyewe u kiongozi wa vipofu, mwanga wao walio gizani, mkufunzi wa wajinga, mwalimu wa watoto wachanga, mwenye namna ya maarifa na ya kweli katika torati; basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe? Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wayaibia mahekalu? Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati? Kwa maana jina la Mungu latukanwa katika Mataifa kwa ajili yenu, kama ilivyoandikwa. Kwa maana kutahiriwa kwafaa kama ukiwa mtendaji wa sheria, lakini ukiwa mvunjaji wa sheria kutahiriwa kwako kumekuwa kutotahiriwa. Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutotahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa? Na yeye asiyetahiriwa kwa asili, aishikaye torati, je! Hatakuhukumu wewe, uliye na kutahiriwa, ukaivunja torati? Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili; bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu.
Waroma 2:17-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini wewe, ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea torati, na kujisifu katika Mungu, na kuyajua mapenzi yake, na kuyakubali mambo yaliyo bora, nawe umeelimishwa katika torati, na kujua hakika ya kuwa wewe mwenyewe u kiongozi wa vipofu, mwanga wao walio gizani, mkufunzi wa wajinga, mwalimu wa watoto wachanga, mwenye namna ya maarifa na ya kweli katika torati; basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe? Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu? Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati? Kwa maana jina la Mungu latukanwa katika Mataifa kwa ajili yenu, kama ilivyoandikwa. Kwa maana kutahiriwa kwafaa kama ukiwa mtendaji wa sheria, lakini ukiwa mvunjaji wa sheria kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa. Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutokutahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa? Na yeye asiyetahiriwa kwa asili, aishikaye torati, je! Hatakuhukumu wewe, uliye na kutahiriwa, ukaihalifu torati? Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili; bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu.
Waroma 2:17-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Tazama, wewe ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea sheria na kujisifia uhusiano wako na Mungu, kama unajua mapenzi ya Mungu na kukubali lililo bora kwa sababu umefundishwa na hiyo sheria, kama unatambua kuwa wewe ni kiongozi wa vipofu, na mwanga kwa wale walio gizani, mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga, kwa kuwa una maarifa ya kweli katika hiyo sheria, basi wewe, uwafundishaye wengine, mbona hujifunzi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, wewe mwenyewe waiba? Wewe usemaye mtu asizini, wewe mwenyewe wazini? Wewe uchukiaye miungu ya sanamu, wafanya jambo la kumchukiza katika mahekalu? Wewe ujivuniaye sheria, wamwaibisha Mungu kwa kuvunja sheria? Kama ilivyoandikwa, “Kwa ajili yenu ninyi, Jina la Mungu linatukanwa miongoni mwa watu wa Mataifa.” Kutahiriwa kuna thamani ikiwa unatii sheria, lakini kama unavunja sheria, kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa. Hivyo, ikiwa wale wasiotahiriwa wanatimiza mambo ambayo sheria inataka, je, kutokutahiriwa kwao hakutahesabiwa kuwa sawa na kutahiriwa? Ndipo wale ambao hawakutahiriwa kimwili lakini wanaitii sheria watawahukumu ninyi, ambao ingawa mmetahiriwa na kuijua sana sheria ya Mungu iliyoandikwa, lakini mwaivunja. Kwa maana mtu si Myahudi kwa vile alivyo kwa nje, wala tohara ya kweli si kitu cha nje au cha kimwili. Lakini mtu ni Myahudi alivyo ndani, nayo tohara ya kweli ni jambo la moyoni, ni la Roho, wala si la sheria iliyoandikwa. Mtu wa namna hiyo hapokei sifa kutoka kwa wanadamu bali kwa Mungu.