Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Warumi 2:17-29

Warumi 2:17-29 NENO

Tazama, wewe ukiwa unajiita Myahudi na kuitegemea Torati na kujisifia uhusiano wako na Mungu, kama unajua mapenzi ya Mungu na kukubali lililo bora kwa sababu umefundishwa na hiyo Torati, kama unatambua kuwa wewe ni kiongozi wa vipofu, na mwanga kwa wale walio gizani, mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga, kwa kuwa una maarifa ya kweli katika hiyo Torati, basi wewe, uwafundishaye wengine, mbona hujifunzi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, wewe mwenyewe waiba? Wewe usemaye mtu asizini, wewe mwenyewe wazini? Wewe uchukiaye miungu ya sanamu, wafanya jambo la kumchukiza katika mahekalu? Wewe ujivuniaye Torati, wamwaibisha Mungu kwa kuvunja Torati? Kama ilivyoandikwa, “Kwa ajili yenu ninyi, Jina la Mungu linatukanwa miongoni mwa watu wa Mataifa.” Kutahiriwa kuna thamani ikiwa unatii Torati, lakini kama unavunja Torati, kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa. Hivyo, ikiwa wale wasiotahiriwa wanatimiza mambo ambayo Torati inataka, je, kutokutahiriwa kwao hakutahesabiwa kuwa sawa na kutahiriwa? Ndipo wale ambao hawakutahiriwa kimwili lakini wanaitii Torati watawahukumu ninyi, ambao ingawa mmetahiriwa na kuijua sana Torati ya Mungu iliyoandikwa, lakini mwaivunja. Kwa maana mtu si Myahudi kwa vile alivyo kwa nje, wala tohara ya kweli si kitu cha nje au cha kimwili. Lakini mtu ni Myahudi alivyo ndani, nayo tohara ya kweli ni jambo la moyoni, ni la Roho wa Mungu, wala si la sheria iliyoandikwa. Mtu kama huyo hapokei sifa kutoka kwa wanadamu bali kwa Mungu.