Waroma 2:17-29
Waroma 2:17-29 BHN
Na wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia sheria na kujivunia kuwa wa Mungu; kwa njia ya sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema; wewe unajiona kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga kwa wale walio gizani; unajiona kuwa mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa wale wasiokomaa bado. Unayo katika sheria picha kamili ya elimu na ukweli. Basi, wewe unawafundisha wengine; kwa nini hujifundishi wewe mwenyewe? Unawahubiria wengine wasiibe, lakini kumbe wewe mwenyewe unaiba. Unasema: “Msizini,” na huku wewe unazini; unachukia sanamu za miungu hali wewe unajitajirisha kwa kuiba katika nyumba za miungu. Kwa kujigamba ati unayo sheria ya Mungu, je huoni kwamba kwa kuivunja sheria unamdharau Mungu? Kama vile Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Watu wa mataifa mengine wamelikufuru jina la Mungu kwa sababu yenu nyinyi Wayahudi!” Kutahiriwa kwako kutakuwa na maana kama ukiitii sheria. Lakini kama unaivunja sheria, basi, ni afadhali ungalibaki bila kutahiriwa. Kama mtu wa mataifa mengine ambaye hakutahiriwa akitimiza matakwa ya sheria, hakika atafikiriwa kana kwamba ametahiriwa. Watu wa mataifa mengine watakuhukumu wewe Myahudi kama ukiivunja sheria, ingawaje unayo maandishi ya sheria na umetahiriwa, hali wao wanaitii sheria ingawa hawakutahiriwa. Ndiyo kusema, si kila anayeonekana kwa nje kuwa Myahudi ni Myahudi wa kweli, wala mtu hawi Myahudi wa kweli ati kwa kuwa ametahiriwa kimwili. Myahudi wa kweli ni yule aliye Myahudi kwa ndani, yaani yule ambaye ametahiriwa moyoni. Hili ni jambo la Roho, na si jambo la maandishi ya sheria. Mtu wa namna hiyo anapata sifa, si kutoka kwa watu, bali kutoka kwa Mungu.