Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Tito 3:1-15

Tito 3:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema. Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikilizano, wawe daima wapole kwa kila mtu. Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukachukiana. Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu ulipofunuliwa, alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji. Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu, ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uhai wa milele tunaotumainia. Jambo hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, yaani mambo mazuri na ya kuwafaa watu. Lakini jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya sheria. Mambo hayo hayana faida yoyote na ni ya bure tu. Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye. Wajua kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba amekosea. Baada ya kumtuma kwako Artema au Tukiko, fanya bidii kuja Nikopoli unione, maana nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi. Jitahidi kumsaidia mwanasheria Zena na Apolo ili waweze kuanza ziara zao, na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji. Ni lazima watu wetu wajifunze kuutumia wakati wao katika kutenda mema ili wasaidie katika mahitaji ya kweli, na maisha yao yawe ya kufaa. Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani. Nawatakieni nyote neema ya Mungu.

Shirikisha
Soma Tito 3

Tito 3:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa watawala na wenye mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema; wasimtukane mtu yeyote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakiwa wapole sana kwa watu wote. Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana. Lakini wema wake Mungu Mwokozi wetu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa mara ya pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu. Ni neno la kuaminiwa; na mambo hayo nataka uyasisitizie sana, ili wale waliomwamini Mungu wakumbuke kudumu katika matendo mema. Mambo hayo ni mazuri sana, tena yana manufaa kwa wanadamu. Lakini ujiepushe na mabishano ya kipumbavu, nasaba, magomvi, na mabishano ya sheria. Kwa kuwa hayana manufaa, tena hayafai kitu. Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, tengana naye; maana unajua ya kuwa mtu kama huyo ni mpotovu na mtenda dhambi, naye amejihukumia hatia yeye mwenyewe. Wakati nitakapomtuma Artema kwako au Tikiko, jitahidi uwezavyo kujiunga nami katika Nikopoli; kwa kuwa nimekusudia kukaa huku wakati wa baridi. Jaribu uwezavyo kumsaidia Zena, yule mwanasheria, na Apolo, ili wakiwa safarini wasipungukiwe na chochote. Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda. Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Tusalimie wale watupendao katika imani. Neema na iwe pamoja nanyi nyote.

Shirikisha
Soma Tito 3

Tito 3:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema; wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote. Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana. Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu. Ni neno la kuaminiwa; na mambo hayo nataka uyanene kwa nguvu, ili wale waliomwamini Mungu wakumbuke kudumu katika matendo mema. Hayo ni mazuri, tena yana faida kwa wanadamu. Lakini maswali ya upuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana. Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae; ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe. Wakati nitakapomtuma Artema kwako au Tikiko, jitahidi kuja kwangu huku Nikopoli; kwa maana huku nimekusudia kukaa wakati wa baridi. Zena, yule mwana-sheria, na Apolo, uwasafirishe kwa bidii, wasipungukiwe na cho chote. Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda. Watu wote walio pamoja nami wakusalimu. Tusalimie wale watupendao katika imani. Neema na iwe pamoja nanyi nyote.

Shirikisha
Soma Tito 3

Tito 3:1-15 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Wakumbushe watu kunyenyekea kwa watawala na kwa wenye mamlaka, na kutii, wakiwa tayari kutenda kila lililo jema, wasimnenee mtu yeyote mabaya, wasiwe wagomvi bali wawe wema, wakiwa wapole kwa watu wote. Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi. Lakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa, alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kupitia kwa Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kupitia kwa Isa Al-Masihi Mwokozi wetu, ili, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele. Hili ni neno la kuaminiwa. Nami nataka uyasisitize mambo haya, ili wale ambao wamemwamini Mungu wapate kuwa waangalifu kujitoa kwa ajili ya kutenda mema wakati wote. Mambo haya ni mazuri tena ya manufaa kwa kila mtu. Lakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu hayana faida, tena ni ubatili. Mtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena. Kwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe. Mara nitakapomtuma Artema au Tikiko kwako, jitahidi kuja unione huko Nikopoli, kwa sababu nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi. Fanya kila uwezalo uwasafirishe Zena yule mwanasheria na Apolo na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji katika safari yao. Watu wetu hawana budi kujifunza kutenda mema, ili waweze kuyakimu mahitaji ya kila siku, wasije wakaishi maisha yasiyokuwa na matunda. Wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu wale wanaotupenda katika imani.

Shirikisha
Soma Tito 3