Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 13:1-9

Zekaria 13:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

“Siku hiyo, kutatokea chemchemi ya kuwatakasa dhambi na unajisi wazawa wa Daudi na wakazi wote wa Yerusalemu. Wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, majina ya vinyago vya miungu nchini nitayaondoa, wala hayatakumbukwa tena. Na wanaojidai kuwa manabii nitawaondolea mbali pamoja na tamaa zao za kuabudu sanamu. Mtu yeyote akijidai kuwa nabii, baba na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Unapaswa kufa kwa kuwa unasema uongo kwa jina la Mwenyezi-Mungu’. Na haohao wazazi wake watamchoma kisu akiwa anatabiri. Siku hiyo, kila nabii atayaonea aibu maono yake anapotabiri. Hawatavaa mavazi ya manyoya ili kudanganya watu, bali kila mmoja atasema, ‘Mimi si nabii. Mimi ni mkulima tu; nimeimiliki ardhi tangu ujana wangu’. Na mtu akimwuliza mmoja wao, ‘Vidonda hivi ulivyo navyo mgongoni vimetoka wapi?’ Yeye atajibu, ‘Vidonda hivi nilivipata katika nyumba ya rafiki zangu.’” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Amka, ee upanga! Inuka umshambulie mchungaji wangu; naam, mchungaji anayenitumikia. Mpige mchungaji na kondoo watawanyike. Nitaunyosha mkono wangu, kuwashambulia watu wadhaifu. Theluthi mbili za watu katika nchi zitaangamizwa; ni theluthi moja tu itakayosalimika. Theluthi hiyo moja itakayosalia, nitaijaribu na kuitakasa, kama mtu asafishavyo fedha, naam, kama ijaribiwavyo dhahabu. Hapo wao wataniomba mimi, nami nitawajibu. Nitasema, ‘Hawa ni watu wangu’, nao watasema, ‘Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu.’”

Shirikisha
Soma Zekaria 13

Zekaria 13:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Katika siku hiyo watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, watafunguliwa chemchemi ya kuwatakasa kutoka kwa dhambi na kwa unajisi. Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema BWANA wa majeshi, nitakatilia mbali majina ya sanamu katika nchi, yasikumbukwe tena; pia nitawafukuza manabii, na roho ya uchafu, watoke katika nchi. Tena itakuwa ya kwamba, mtu awaye yote atakapotoa unabii, basi baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, Hutaishi; kwa maana unanena maneno ya uongo kwa jina la BWANA; na baba yake na mama yake waliomzaa watamtumbua atoapo unabii. Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba manabii, kila mmoja wao, atayaonea haya maono yake atoapo unabii; wala hawatavaa joho la nywele ili kudanganya watu; bali atasema, Mimi si nabii kamwe; mimi ni mkulima wa nchi; kwa maana nilifanywa mtumwa tokea ujana wangu. Na mtu yeyote akimwuliza, Je! Majeraha haya yote uliyo nayo katikati ya mikono yako ni nini? Naye atajibu, Ni majeraha niliyotiwa katika nyumba ya rafiki zangu. Amka, Ee upanga, juu ya mchungaji wangu, na juu ya mtu aliye mwenzangu, asema BWANA wa majeshi; mpige mchungaji, nao kondoo watatawanyika; nami nitaugeuza mkono wangu juu ya wadogo. Hata itakuwa, ya kwamba katika nchi yote mafungu mawili yatakatiliwa mbali, nao watakufa, asema BWANA; lakini fungu la tatu litabaki humo. Nami nitalileta fungu lile la tatu na kulipitisha kati ya moto, nami nitawasafisha kama fedha isafishwavyo, nami nitawajaribu kama dhahabu ijaribiwavyo; wataliitia jina langu, nami nitawasikia; mimi nitasema, Watu hawa ndio wangu; nao watasema, BWANA ndiye Mungu wangu.

Shirikisha
Soma Zekaria 13

Zekaria 13:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Katika siku hiyo watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, watafunguliwa chemchemi kwa dhambi na kwa unajisi. Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema BWANA wa majeshi, nitakatilia mbali majina ya sanamu katika nchi, yasikumbukwe tena; pia nitawafukuza manabii, na roho ya uchafu, watoke katika nchi. Tena itakuwa ya kwamba, mtu awaye yote atakapotoa unabii, basi baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, Hutaishi; kwa maana unanena maneno ya uongo kwa jina la BWANA; na baba yake na mama yake waliomzaa watamtumbua atoapo unabii. Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba manabii, kila mmoja wao, atayaonea haya maono yake atoapo unabii; wala hawatavaa joho ya nywele ili kudanganya watu; bali atasema, Mimi si nabii kamwe; mimi ni mkulima wa nchi; kwa maana nalifanywa mtumwa tokea ujana wangu. Na mtu atamwambia, Je! Jeraha hizi ulizo nazo kati ya mikono yako ni nini? Naye atajibu, Ni jeraha nilizotiwa katika nyumba ya rafiki zangu. Amka, Ee upanga, juu ya mchungaji wangu, na juu ya mtu aliye mwenzangu, asema BWANA wa majeshi; mpige mchungaji, nao kondoo watatawanyika; nami nitaugeuza mkono wangu juu ya wadogo. Hata itakuwa, ya kwamba katika nchi yote mafungu mawili yatakatiliwa mbali, nao watakufa, asema BWANA; lakini fungu la tatu litabaki humo. Nami nitalileta fungu lile la tatu na kulipitisha kati ya moto, nami nitawasafisha kama fedha isafishwavyo, nami nitawajaribu kama dhahabu ijaribiwavyo; wataliitia jina langu, nami nitawasikia; mimi nitasema, Watu hawa ndio wangu; nao watasema, BWANA ndiye Mungu wangu.

Shirikisha
Soma Zekaria 13

Zekaria 13:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Katika siku hiyo, chemchemi itafunguliwa kwa nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu, kuwatakasa dhambi na unajisi. “Katika siku hiyo, nitayakatilia mbali majina ya sanamu kutoka nchi, nayo hayatakumbukwa tena,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. “Nitaondoa manabii wao pamoja na roho ya uchafu katika nchi. Ikiwa yupo yeyote atakayeendelea kutabiri, baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Ni lazima ufe, kwa sababu umesema uongo kwa jina la BWANA.’ Atakapotabiri, wazazi wake mwenyewe watampasua tumbo. “Katika siku hiyo, kila nabii ataaibika kwa maono ya unabii wake. Hatavaa vazi la kinabii la nywele ili apate kudanganya watu. Atasema, ‘Mimi sio nabii. Mimi ni mkulima; ardhi imekuwa kazi yangu tangu ujana wangu.’ Ikiwa mtu atamuuliza, ‘Majeraha haya yaliyo mwilini mwako ni ya nini?’ Atajibu, ‘Ni majeraha niliyoyapata katika nyumba ya rafiki zangu.’ “Amka, ee upanga, dhidi ya mchungaji wangu, dhidi ya mtu aliye karibu nami!” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. “Mpige mchungaji, nao kondoo watatawanyika, nami nitageuza mkono wangu dhidi ya walio wadogo, katika nchi yote,” asema BWANA, “theluthi mbili watapigwa na kuangamia; hata hivyo theluthi moja watabaki ndani yake. Hii theluthi moja nitaileta katika moto; nitawasafisha kama fedha isafishwavyo na kuwajaribu kama dhahabu. Wataliitia Jina langu nami nitawajibu; nitasema, ‘Hawa ni watu wangu,’ nao watasema, ‘BWANA ni Mungu wetu.’ ”

Shirikisha
Soma Zekaria 13