BibleProject | Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio / Sehemu ya 1 - LukaMfano
Mariamu alipokaribia kujifungua, yeye na mchumba wake, Yusufu, wanahitaji kwenda mji wa Bethlehemu kujiandikisha kwenye sensa iliyoamuriwa na Kaisari Augusto. Wanawasili, na Mariamu anapatwa na uchungu wa kuzaa. Hawapati chumba cha wageni na sehemu pekee wanayopata ni zizi la wanyama. Mariamu anajifungua na kumweka mwana atakayekuwa mfalme wa Israeli horini.
Karibu na alipozaliwa mwana, wachungaji wako makondeni wakilisha mifugo yao kisha ghafla malaika mwenye utukufu anawatokea. Tukio hili, bila shaka, linawaogopesha. Lakini malaika anawaambia wafurahie kwa sababu Mwokozi amezaliwa. Wanaelezwa kuwa watamkuta mtoto amevikwa nguo na amelazwa horini. Kwaya ya Malaika inatokea ikisherehekea kwa kumsifu Mungu aliyeleta amani yake ulimwenguni. Wachungaji wanaondoka haraka kwenda kumtafuta mtoto. Wanamkuta mtoto Yesu horini kama alivyosema malaika. Wanastaajabu. Wanaeneza habari za walioyashuhudia na kila anayesikia habari hizi anashangaa.
Hakuna aliyetarajia kuwa Mungu angejitokeza namna hii––kazaliwa kwenye zizi na msichana na kutukuzwa na wachungaji wasiojulikana. Kila tukio kwenye simulizi ya Luka linakinzana na matarijio, na hilo ndilo lengo. Anaonyesha jinsi Ufalme wa Mungu hufika mahali pasipo na hadhi––kwa wanaosubiri, wajane, maskini––kwa sababu Yesu yu hapa kuleta wokovu kwa kugeuza taratibu za ulimwengu wetu chini-juu.
Soma, Tafakari, kisha Ujibu:
•Je, wachungaji walipokea vipi habari za kustaajabisha zilizoletwa na malaika? Je, ingekuwa wewe ungehisi vipi? Je, unapokea vipi habari za amani ya Mungu kuja ulimwenguni kupitia kwa mtoto aliyelazwa horini?
•Je, Simeoni na Ana wanampokea vipi mtoto Yesu anapoletwa hekaluni? Je, wanamtambua vipi kuwa mfalme wa Israeli?
•Je, ungetarajia mfalme mtukufu aje vipi? Je, hali za kuja kwa Yesu zinaonyesha nini kuhusu Ufalme wa Mungu?
•Kusoma na kutafakari kwako kukuchochee kuomba. Mshukuru Mungu kwa kuja kupitia Yesu. Zungumza naye kuhusu jinsi unavyokubaliana na ujumbe wake, kile usichokiamini na kile unachohitaji leo.
Andiko
Kuhusu Mpango huu
Shirika la BibleProject liliandaa mwongozo wa Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio Sehemu ya 1 kuwahimiza watu binafsi, vikundi vidogo na familia kusoma kitabu chote cha Luka kwa siku 20. Mwongozo huu unajumuisha video za katuni, muhtasari wa uchambuzi na maswali ya kutafakari ili kuwasaidia wahusika kumfahamu Yesu na kufuatilia mtiririko wa mawazo ya Luka pamoja na kuyaelewa mafunzo yake.
More
Tungependa kushukuru shirika la BibleProject kwa kutoa mwongozo huu. Kwa maelezo zaidi, tafadhali tembelea: www.bibleproject.com