Mwanzo 2
2
1Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyokamilika pamoja na vitu vyote vilivyomo. 2Siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyofanya; siku hiyo ya saba Mungu akapumzika baada ya kazi yake yote aliyofanya. 3Mungu akaibariki siku ya saba na kuitakasa, kwa kuwa siku hiyo Mungu alipumzika baada ya kazi yake yote ya kuumba. 4Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyoumbwa.
Bustani ya Edeni
Siku ile Mwenyezi-Mungu#2:4 Mwenyezi-Mungu: Katika makala ya Kiebrania ni Yahweh. Neno hili halina wingi; kadhalika na neno la Kiswahili Mwenyezi-Mungu halina wingi. Lamtaja Mungu aliye peke yake Mungu alipoziumba mbingu na dunia, 5Hapakuwa na mimea juu ya nchi wala miti haikuwa imechipua kwani Mwenyezi-Mungu hakuwa ameinyeshea nchi mvua, wala hapakuwa na mtu wa kuilima. 6Hata hivyo, maji yalitoka ardhini yakainywesha ardhi yote. 7Basi, Mwenyezi-Mungu akamfanya mwanamume kwa mavumbi ya udongo, akampulizia puani pumzi ya uhai, na huyo mwanamume akawa kiumbe hai.
8Kisha Mwenyezi-Mungu akapanda bustani huko Edeni, upande wa mashariki, na humo akamweka huyo mwanamume aliyemuumba. 9Mwenyezi-Mungu akaotesha kutoka ardhini kila aina ya miti mizuri izaayo matunda yafaayo kwa chakula. Katikati ya bustani hiyo kulikuwa na mti wa uhai na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.#2:9 mti wa uhai: Ufu 2:7; 22:2,14; Ujuzi wa mema na mabaya; tafsiri nyingine: Ujuzi wa kila kitu (vilevile aya 17 na 3:5,22.)
10Kulikuwa na mto huko Edeni uliotiririka maji na kuinywesha hiyo bustani; kutoka huko mto huo uligawanyika kuwa mito minne. 11Jina la mto wa kwanza ni Pishoni; huo waizunguka nchi yote ya Hawila ambako kuna dhahabu. 12Dhahabu ya nchi hiyo ni safi kabisa. Huko pia kuna marashi yaitwayo bedola na vito viitwavyo shohamu. 13Jina la mto wa pili ni Gihoni; huo waizunguka nchi yote ya Kushi#2:13 nchi yote ya Kushi: Hufikiriwa na wengine kuwa Mesopotamia. Lakini baadhi wadhani ni sehemu ya kaskazini ya Afrika, kusini ya Misri (Sudani au Ethiopia.). 14Jina la mto wa tatu ni Tigri#2:14 Tigri: Kiebrania: Mto huo ni Hidekeli., nao watiririkia upande wa mashariki wa nchi ya Ashuru; na jina la mto wa nne ni Eufrate.
15Basi, Mwenyezi-Mungu akamtwaa huyo mwanamume, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. 16Mwenyezi-Mungu alimwamuru huyo mwanamume, “Waweza kula matunda ya mti wowote katika bustani; 17lakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, usile, maana siku utakapokula matunda ya mti huo, hakika utakufa.”
18Kisha Mwenyezi-Mungu akasema, “Si vizuri huyu mwanamume kuwa peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.” 19Basi, kutoka katika udongo, Mwenyezi-Mungu akaumba kila mnyama wa porini na kila ndege wa angani, halafu akamletea huyo mwanamume aone atawapa majina gani; na majina aliyowapa viumbe hao, yakawa ndio majina yao. 20Basi, huyo mwanamume akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, wanyama wa porini na ndege wote wa angani. Lakini hakupatikana msaidizi yeyote wa kumfaa.
21Basi, Mwenyezi-Mungu akamletea huyo mwanamume usingizi mzito, na alipokuwa usingizini, akatwaa ubavu wake mmoja na kupafunika mahali pale kwa nyama. 22Na huo ubavu Mwenyezi-Mungu alioutoa kwa yule mwanamume akaufanya kuwa mwanamke, akamleta kwa huyo mwanamume. 23Ndipo huyo mwanamume akasema,
“Naam! Huyu ni mfupa kutoka mifupa yangu,
na nyama kutoka nyama yangu.
Huyu ataitwa ‘Mwanamke#2:23 Kiebrania: Maneno mwanamume … mwanamke; “ishi, isha” yanafanana.’,
kwa sababu ametolewa katika mwanamume.”
24Ndiyo maana mwanamume humwacha baba yake na mama yake, akaambatana na mkewe, nao wawili huwa mwili mmoja.
25Huyo mwanamume na mkewe wote walikuwa uchi, lakini hawakuona haya.
Currently Selected:
Mwanzo 2: SCLDC10
ማድመቅ
Share
Copy
ያደመቋቸው ምንባቦች በሁሉም መሣሪያዎችዎ ላይ እንዲቀመጡ ይፈልጋሉ? ይመዝገቡ ወይም ይግቡ
Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.