Wagalatia 5
5
Uhuru ndani ya Al-Masihi
1Al-Masihi alitupatia uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na nira ya utumwa.
2Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba mkikubali kutahiriwa, basi Al-Masihi hatakuwa na thamani kwenu hata kidogo. 3Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika Torati yote. 4Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kupitia kwa Torati mmetengwa na Al-Masihi, mko mbali na neema ya Mungu. 5Kwa maana, kupitia Roho wa Mungu tunangojea kwa shauku tumaini la haki kwa imani. 6Kwa maana ndani ya Al-Masihi Isa, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kupitia kwa upendo.
7Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli? 8Ushawishi kama huo haukutoka kwa yule anayewaita. 9“Chachu kidogo huchachua donge zima.” 10Nina hakika katika Bwana Isa kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani. 11Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa. 12Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!
13Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14Kwa maana Torati yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”#5:14 Walawi 19:18 15Lakini mkiumana na kutafunana, angalieni msije mkaangamizana.
Maisha ya Kiroho
16Kwa hiyo nasema, nendeni kwa Roho wa Mungu, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. 18Lakini mkiongozwa na Roho wa Mungu, hamko chini ya Torati.
19Basi matendo ya mwili ni dhahiri, nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi ufalme wa Mungu.
22Lakini tunda la Roho wa Mungu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24Wote walio wa Al-Masihi Isa wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25Kwa kuwa tunaishi kwa Roho wa Mungu, basi, tuenende kwa Roho. 26Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.
Currently Selected:
Wagalatia 5: NENO
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.