YouVersion Logo
Search Icon

Wagalatia 6

6
Chukulianeni mizigo
1Ndugu zangu, ikiwa mtu amepatikana akitenda dhambi, basi ninyi mnaoishi kwa Roho wa Mungu mnapaswa kumrejesha mtu huyo kwa upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. 2Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Al-Masihi. 3Mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe. 4Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine. 5Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe. 6Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.
7Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho wa Mungu, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waumini.
Si kutahiriwa bali kuwa kiumbe kipya
11Angalieni herufi kubwa ninazotumia nikiwaandikia kwa mkono wangu mwenyewe!
12Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanataka wawalazimishe kutahiriwa. Sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Al-Masihi. 13Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu. 14Lakini mimi naomba nisije nikajivunia kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, ambaye kwake ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. 15Kwa maana katika Al-Masihi Isa, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu! 16Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii, hata kwa Israeli wa Mungu.
17Hatimaye, tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Isa.
18Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe pamoja na roho zenu. Amen.

Currently Selected:

Wagalatia 6: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in