YouVersion Logo
Search Icon

Isaya 57

57
Ibada batili ya sanamu ya Israeli
1Mwenye haki hupotea,
wala hakuna hata mmoja awazaye hilo moyoni mwake;
watu wanaomcha Mungu huondolewa,
wala hakuna hata mmoja anayeelewa
kuwa wenye haki wameondolewa
ili wasipatikane na maovu.
2Wale wanaoenda kwa unyofu
huwa na amani;
hupata pumziko wanapolala mautini.
3“Lakini ninyi:
Njooni hapa, ninyi wana wa wachawi,
ninyi wazao wa wazinzi na makahaba!
4Mnamdhihaki nani?
Ni nani mnayemcheka kwa dharau,
na kumtolea ndimi zenu?
Je, ninyi si watoto wa waasi,
uzao wa waongo?
5Mnawaka tamaa katikati ya mialoni
na chini ya kila mti uliotanda matawi;
mnawatoa kafara watoto wenu kwenye mabonde
na chini ya majabali yenye mianya.
6“Sanamu zilizo kati ya mawe laini ya mabondeni ndizo fungu lenu;
hizo ndizo sehemu yenu.
Naam, kwa hizo mmemimina sadaka za vinywaji,
na kutoa sadaka za nafaka.
Katika haya yote,
niendelee kuona huruma?
7Umeweka kitanda chako juu kwenye kilima kirefu kilichoinuka,
huko ulienda kutoa dhabihu zako.
8Nyuma ya milango yako na miimo yako
umeweka alama zako za kipagani.
Kwa kuniacha mimi, ulifunua kitanda chako,
umepanda juu yake na kukipanua sana;
ulifanya patano na wale ambao unapenda vitanda vyao,
nawe uliangalia uchi wao.
9Ulienda kwa Moleki#57:9 au kwa mfalme ukiwa na mafuta ya zeituni,
na ukaongeza manukato yako.
Ukawatuma wajumbe wako mbali sana,
ukashuka kwenye kaburi#57:9 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol. lenyewe!
10Ulikuwa umechoshwa na njia zako zote,
lakini hukusema, ‘Hakuna tumaini.’
Ulipata uhuisho wa nguvu zako,
kwa sababu hiyo hukuzimia.
11“Ni nani uliyemhofu hivyo na kumwogopa
hata ukawa mwongo kwangu,
wala hukunikumbuka
au kutafakari hili moyoni mwako?
Si ni kwa sababu nimekuwa kimya muda mrefu
hata huniogopi?
12Nitaifunua haki yako na matendo yako,
nayo hayatakufaidi.
13Utakapolia kwa kuhitaji msaada,
sanamu zako ulizojikusanyia na zikuokoe!
Upepo utazipeperusha zote,
pumzi peke yake itazipeperusha,
Lakini mtu atakayenifanya kimbilio lake,
atairithi nchi
na kuumiliki mlima wangu mtakatifu.”
Faraja kwa wenye majuto
14Tena itasemwa:
“Jengeni, jengeni, itengenezeni njia!
Ondoeni vikwazo katika njia ya watu wangu.”
15Kwa maana hili ndilo asemalo Aliye juu,
yeye aliyeinuliwa sana,
yeye aishiye milele,
ambaye jina lake ni Mtakatifu:
“Ninaishi mahali palipoinuka
na patakatifu,
lakini pia pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu,
na mwenye roho ya unyenyekevu,
ili kuzihuisha roho za wanyenyekevu
na kuihuisha mioyo yao waliotubu.
16Sitaendelea kulaumu milele,
wala sitakasirika siku zote,
kwa kuwa roho ya mwanadamu
ingezimia mbele zangu:
yaani pumzi ya mwanadamu niliyemuumba.
17Nilighadhibika na tamaa yake ya dhambi;
nilimwadhibu, nikauficha uso wangu kwa hasira,
na bado aliendelea katika njia zake za tamaa.
18Nimeziona njia zake, lakini nitamponya,
nitamwongoza na kumrudishia upya faraja,
19nikiumba sifa midomoni ya waombolezaji
katika Israeli.
Amani, amani, kwa wale walio mbali
na kwa wale walio karibu,”
asema Mwenyezi Mungu. “Nami nitawaponya.”
20Bali waovu ni kama bahari ichafukayo,
ambayo haiwezi kutulia,
mawimbi yake hutupa takataka na matope.
21Mungu wangu asema,
“Hakuna amani kwa waovu.”

Currently Selected:

Isaya 57: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in