YouVersion Logo
Search Icon

Isaya 58

58
Mfungo wa kweli
1“Piga kelele, usizuie.
Paza sauti yako kama tarumbeta.
Watangazieni watu wangu uasi wao,
na kwa nyumba ya Yakobo dhambi zao.
2Kwa maana kila siku hunitafuta,
wanaonekana kutaka kujua njia zangu,
kana kwamba walikuwa taifa linalotenda lililo sawa,
na ambalo halijaziacha amri za Mungu wake.
Hutaka kwangu maamuzi ya haki,
nao hutamani Mungu awakaribie.
3Wao husema, ‘Mbona tumefunga, nawe hujaona?
Mbona tumejinyenyekeza, nawe huangalii?’
“Lakini katika siku ya kufunga kwenu, mnafanya mnavyotaka
na kuwadhulumu wafanyakazi wenu wote.
4Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano,
na kupigana ninyi kwa ninyi kwa ngumi za uovu.
Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo
na kutazamia sauti zenu kusikiwa huko juu.
5Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua,
siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza?
Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete,
na kwa kujilaza juu ya gunia na majivu?
Je, huo ndio mnaouita mfungo,
siku iliyokubalika kwa Mwenyezi Mungu?
6“Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua:
kufungua minyororo ya udhalimu,
na kufungua kamba za nira,
kuwaweka huru waliodhulumiwa,
na kuvunja kila nira?
7Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa
na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi,
unapomwona aliye uchi, umvike,
wala si kumkimbia mtu wa mwili wako
na damu yako mwenyewe?
8Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko
na uponyaji wako utatokea upesi;
ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako,
na utukufu wa Mwenyezi Mungu utakuwa mlinzi nyuma yako.
9Ndipo utaita, naye Mwenyezi Mungu atajibu,
utalia kuomba msaada,
naye atasema: Mimi hapa.
“Ukiiondoa nira ya udhalimu,
na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,
10nanyi mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu
na kutosheleza mahitaji ya waliodhulumiwa,
ndipo nuru yenu itang’aa gizani,
nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.
11Mwenyezi Mungu atakuongoza siku zote,
atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame,
naye ataitia nguvu mifupa yako.
Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri,
kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.
12Watu wako watajenga tena magofu ya zamani
na kuinua misingi ya kale;
utaitwa Mwenye Kukarabati Kuta Zilizobomoka,
Mwenye Kurejesha Barabara za Makao.
13“Ukitunza miguu yako isivunje Sabato,
na kutokufanya kama vile upendavyo katika siku yangu takatifu,
ukiita Sabato siku ya furaha
na siku takatifu ya Mwenyezi Mungu ya kuheshimiwa,
kama utaiheshimu kwa kutoenenda
katika njia zako mwenyewe,
na kutokufanya yakupendezayo
au kusema maneno ya upuzi,
14ndipo utakapojipatia furaha yako katika Mwenyezi Mungu,
nami nitakufanya upande juu ya miinuko ya nchi
na kusherehekea urithi wa Yakobo baba yako.”
Kinywa cha Mwenyezi Mungu kimenena haya.

Currently Selected:

Isaya 58: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in