YouVersion Logo
Search Icon

Isaya 60

60
Utukufu wa Sayuni
1“Ondoka, angaza, kwa kuwa nuru yako imekuja
na utukufu wa Mwenyezi Mungu umezuka juu yako.
2Tazama, giza litaifunika dunia,
na giza nene litayafunika mataifa,
lakini Mwenyezi Mungu atazuka juu yako
na utukufu wake utaonekana juu yako.
3Mataifa watakuja kwenye nuru yako
na wafalme kwa mwanga wa mapambazuko yako.
4“Inua macho yako na utazame pande zote:
Wote wanakusanyika na kukujia,
wana wako wanakuja toka mbali,
nao binti zako wanabebwa mikononi.
5Ndipo utatazama na kutiwa nuru,
moyo wako utasisimka na kujaa furaha,
mali iliyo baharini italetwa kwako,
utajiri wa mataifa utakujilia.
6Makundi ya ngamia yatajaa katika nchi yako,
ngamia vijana wa Midiani na Efa.
Nao watu wote wanaotoka Sheba watakuja,
wakichukua dhahabu na uvumba
na kutangaza sifa za Mwenyezi Mungu.
7Makundi yote ya Kedari yatakusanyika kwako,
kondoo dume wa Nebayothi watakutumikia,
watakubalika kama sadaka juu ya madhabahu yangu,
nami nitalipamba Hekalu langu tukufu.
8“Ni nani hawa warukao kama mawingu,
kama hua kuelekea kwenye viota vyao?
9Hakika visiwa vinanitazama;
merikebu za Tarshishi#60:9 au: za biashara(taz. 1 Wafalme 10:22; 22:48; 2 Nyakati 9:21; 20:36; Isaya 2:16). ndizo zinazotangulia,
zikiwaleta wana wenu kutoka mbali,
wakiwa na fedha na dhahabu zao,
kwa heshima ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli,
kwa maana amekujalia utukufu.
10“Wageni watazijenga upya kuta zako,
na wafalme wao watakutumikia.
Ingawa katika hasira nilikupiga,
lakini katika upendeleo wangu
nitakuonesha huruma.
11Malango yako yatakuwa wazi siku zote,
kamwe hayatafungwa, mchana wala usiku,
ili watu wapate kukuletea utajiri wa mataifa:
wafalme wao wakiongoza maandamano ya ushindi.
12Kwa maana taifa au ufalme ule ambao hautakutumikia utaangamia;
utaharibiwa kabisa.
13“Utukufu wa Lebanoni utakujilia,
msunobari, mvinje pamoja na mteashuri,
ili kupapamba mahali pangu patakatifu,
nami nitapatukuza mahali pa miguu yangu.
14Wana wa wale waliokutesa watakuja wakisujudu mbele yako;
wote wanaokudharau watasujudu miguuni pako;
nao watakuita Mji wa Mwenyezi Mungu,
Sayuni ya Aliye Mtakatifu wa Israeli.
15“Ingawa umeachwa na kuchukiwa,
bila yeyote anayesafiri ndani yako,
nitakufanya kuwa fahari ya milele,
na furaha ya vizazi vyote.
16Utanyonya maziwa ya mataifa,
na kunyonyeshwa matiti ya wafalme.
Ndipo utakapojua kwamba Mimi, Mwenyezi Mungu,
ni Mwokozi wako, Mkombozi wako,
niliye Mwenye Nguvu wa Yakobo.
17Badala ya shaba nitakuletea dhahabu,
na fedha badala ya chuma.
Badala ya mti nitakuletea shaba,
na chuma badala ya mawe.
Nitafanya amani kuwa mtawala wako,
na haki kuwa mfalme wako.
18Jeuri hazitasikika tena katika nchi yako,
wala maangamizi au uharibifu
ndani ya mipaka yako,
lakini utaita kuta zako Wokovu,
na malango yako Sifa.
19Jua halitakuwa tena nuru yako mchana,
wala mwangaza wa mwezi hautakuangazia,
kwa maana Mwenyezi Mungu atakuwa nuru yako ya milele,
naye Mungu wako atakuwa utukufu wako.
20Jua lako halitazama tena,
nao mwezi wako hautafifia tena;
Mwenyezi Mungu atakuwa nuru yako milele,
nazo siku zako za huzuni zitakoma.
21Ndipo watu wako wote watakuwa waadilifu,
nao wataimiliki nchi milele.
Wao ni chipukizi nililolipanda,
kazi ya mikono yangu,
ili kuonesha utukufu wangu.
22Aliye mdogo kwenu atakuwa elfu,
mdogo kuliko wote atakuwa taifa lenye nguvu.
Mimi ndimi Mwenyezi Mungu;
katika wakati wake nitayatimiza haya upesi.”

Currently Selected:

Isaya 60: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in