YouVersion Logo
Search Icon

Mathayo 27

27
Isa apelekwa kwa Pilato
(Marko 15:1; Luka 23:1; Yohana 18:28)
1Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Isa ili kumuua. 2Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, aliyekuwa mtawala Mrumi.
Yuda ajinyonga
(Matendo 1:18-19)
3Yuda, aliyemsaliti Isa, alipoona kuwa Isa amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 4Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.”
Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”
5Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.
6Wale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.” 7Hivyo basi, baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni. 8Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo. 9Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyowekewa na watu wa Israeli, 10wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoniagiza.”#27:10 Zekaria 11:12, 13; Yeremia 19:1-13; 32:6-9
Pilato amhoji Isa
(Marko 15:1-15; Luka 23:3-25; Yohana 18:28–19:16)
11Wakati huo Isa akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?”
Isa akasema, “Wewe wasema hivyo.”
12Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno. 13Ndipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?” 14Lakini Isa hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.
Pilato amtoa Isa asulubiwe
(Marko 15:6-15; Luka 23:13-25; Yohana 18:39–19:16)
15Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu. 16Palikuwa na mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba. 17Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza hao watu, “Mnataka niwafungulie yupi: Baraba au Isa aitwaye Al-Masihi?” 18Kwa kuwa alitambua kwamba walikuwa wamemkabidhi Isa kwake kwa ajili ya wivu.
19Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”
20Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakashawishi umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe, naye Isa auawe.
21Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?”
Wakajibu, “Baraba.”
22Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Isa aitwaye Al-Masihi?”
Wakajibu wote, “Msulubishe!”
23Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”
Lakini wao wakazidi kupiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”
24Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lolote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya umati wa watu, akasema, “Sina hatia kwa damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!”
25Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”
26Basi akawafungulia Baraba. Lakini baada ya kuamuru Isa apigwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
Askari wamdhihaki Isa
(Marko 15:16-20; Yohana 19:2-3)
27Kisha askari wa mtawala wakampeleka Isa kwenye Praitorio#27:27 Praitorio ilikuwa makao makuu ya mtawala wa jimbo. Hapa ni jumba la kifalme ambapo Pontio Pilato aliishi huko Yerusalemu, palipokuwa na kiti cha hukumu., na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka. 28Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha 29wakasokota taji la miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” 30Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena. 31Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe.
Isa asulubishwa
(Marko 15:21-32; Luka 23:26-43; Yohana 19:17-27)
32Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. 33Wakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). 34Hapo wakampa Isa divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa. 35Walipokwisha kumsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”]#27:35 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya. 36Kisha wakaketi, wakamchunga. 37Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi:
Huyu ni Isa
Mfalme wa Wayahudi.
38Wanyang’anyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. 39Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao, 40na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu#27:40 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili., shuka msalabani.”
41Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa Torati pamoja na wazee wakamdhihaki, wakisema, 42“Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni mfalme wa Israeli! Ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. 43Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ” 44Hata wale wanyang’anyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.
Kifo cha Isa
(Marko 15:33-41; Luka 23:44-49; Yohana 19:28-30)
45Tangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote. 46Ilipofika saa tisa, Isa akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?”#27:46 Zaburi 22:1 (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)
47Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Ilya.”
48Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Isa ili anywe. 49Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Ilya atakuja kumwokoa.”
50Isa alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.
51Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka. 52Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa. 53Wakatoka makaburini, na baada ya Isa kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi.
54Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Isa walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa sana, wakapaza sauti na kusema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”
55Wanawake wengi walikuwa pale wakitazama kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Isa tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake. 56Miongoni mwao walikuwemo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.
Maziko ya Isa
(Marko 15:42-47; Luka 23:50-56; Yohana 19:38-42)
57Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yusufu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Isa. 58Akamwendea Pilato ili kumwomba mwili wa Isa. Pilato akaamuru apewe. 59Yusufu akauchukua mwili wa Isa, akaufunga kwa kitambaa cha kitani safi, 60na kuuweka katika kaburi lake mwenyewe jipya, alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa katika ingilio la kaburi, akaenda zake. 61Mariamu Magdalene na yule Mariamu mwingine walikuwa mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.
Walinzi pale kaburini
62Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalizi ya Sabato, viongozi wa makuhani na Mafarisayo#27:62 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. wakamwendea Pilato 63na kusema, “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mdanganyifu wakati alikuwa bado hai alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’ 64Basi uamuru kaburi lilindwe kwa uthabiti hadi baada ya siku tatu. La sivyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kuuiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuliwa kutoka kwa wafu. Udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.”
65Pilato akawaambia, “Ninyi mnao askari walinzi. Nendeni, liwekeeni ulinzi kadiri mnavyoweza.” 66Hivyo basi wakaenda na walinzi ili kulilinda kaburi kwa uthabiti, wakatia muhuri kwenye lile jiwe na kuweka ulinzi.

Currently Selected:

Mathayo 27: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in