YouVersion Logo
Search Icon

Mathayo 4

4
Isa ajaribiwa nyikani
(Marko 1:12-13; Luka 4:1-13)
1Kisha Isa akaongozwa na Roho Mtakatifu wa Mungu hadi nyikani ili ajaribiwe na ibilisi. 2Baada ya kufunga siku arobaini usiku na mchana, hatimaye akaona njaa. 3Mjaribu akamjia na kumwambia, “Ikiwa wewe ndiwe Mwana wa Mungu#4:3 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1), wa kiroho, bali si wa kimwili., amuru mawe haya yawe mikate.”
4Lakini Isa akajibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’#4:4 Kumbukumbu 8:3
5Ndipo ibilisi akampeleka Isa hadi mji mtakatifu na kumweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu#4:5 Nyumba kuu ya ibada kwa Waisraeli iliyokuwa Yerusalemu., 6akamwambia, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini. Kwa kuwa imeandikwa:
“ ‘Atakuagizia malaika wake,
nao watakuchukua mikononi mwao
ili usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’#4:6 Zaburi 91:11, 12
7Isa akamjibu, “Pia imeandikwa: ‘Usimjaribu Mwenyezi Mungu, Mungu wako.’#4:7 Kumbukumbu 6:16
8Kwa mara nyingine, ibilisi akampeleka Isa hadi kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonesha falme zote za dunia na fahari zake, 9kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote ukinisujudia na kuniabudu.”
10Isa akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Mwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’#4:10 Kumbukumbu 6:13
11Ndipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumhudumia.
Isa aanza kuhubiri
(Marko 1:14-15; Luka 4:14-15)
12Isa aliposikia kwamba Yahya alikuwa amefungwa gerezani, alirudi Galilaya. 13Akaondoka Nasiri akaenda kuishi Kapernaumu, mji ulio karibu na bahari, katika nchi ya Zabuloni na Naftali, 14ili kutimiza neno lililonenwa na nabii Isaya, aliposema:
15“Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali,
kwenye njia ya bahari,
ng’ambo ya Yordani,
Galilaya ya Mataifa:
16watu wale waliokaa gizani
wameona nuru kuu;
nao wale walioishi katika nchi ya uvuli wa mauti,
nuru imewazukia.”#4:16 Isaya 9:1, 2
17Tangu wakati huo, Isa alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”
Wanafunzi wa kwanza wa Isa
(Marko 1:16-20; Luka 5:1-11; Yohana 1:35-51)
18Isa alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa kuwa walikuwa wavuvi. 19Isa akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” 20Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.
21Alipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakizitengeneza nyavu zao. Isa akawaita. 22Nao mara moja wakaiacha mashua yao, pamoja na baba yao, wakamfuata.
Isa afundisha na kuponya wagonjwa
(Luka 6:17-19)
23Isa akazunguka Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi#4:23 Nyumba za ibada na mafunzo. yao, akihubiri Habari Njema za ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu. 24Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Siria, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya. 25Makundi makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli#4:25 yaani Miji Kumi, Yerusalemu, Yudea, na kutoka ng’ambo ya Yordani.

Currently Selected:

Mathayo 4: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in