YouVersion Logo
Search Icon

Tito 1

1
Salamu
1Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Isa Al-Masihi kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu na kuijua kweli iletayo utauwa: 2imani na ujuzi katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu, asiyesema uongo, aliahidi hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, 3naye kwa wakati wake aliouweka alilidhihirisha neno lake kupitia kwa mahubiri ambayo mimi nimewekewa amana kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu.
4Kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tunayoshiriki sote.
Neema na amani zitokazo kwa Mungu, Baba#1:4 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi, Mwokozi wetu, ziwe nawe.
Sifa za wazee wa kundi la waumini
5Sababu yangu ya kukuacha huko Krete ni ili uweke utaratibu mambo yale yaliyosalia na kuwateua wazee wa kundi la waumini katika kila mji, kama nilivyokuagiza. 6Mzee wa kundi la waumini asiwe na lawama, awe mume wa mke mmoja, mtu ambaye watoto wake ni waumini, wala hawashtakiwi kwa ufisadi. 7Kwa kuwa mwangalizi wa kundi ni wakili wa Mungu, imempasa kuwa mtu asiye na lawama, asiwe mwenye majivuno au mwepesi wa hasira, wala mlevi, wala asiwe mtu mwenye tamaa ya mapato yasiyo ya halali. 8Bali awe mkarimu, anayependa mema, mwenye kiasi, mwenye haki, mwadilifu, mnyofu, mtakatifu na mwenye kuitawala nafsi yake. 9Lazima alishike kwa uthabiti lile neno la imani kama lilivyofundishwa, ili aweze kuwatia moyo wengine kwa mafundisho yenye uzima na kuwakanusha wale wanaopingana nayo.
Kemea wale wasiotii
10Kwa maana wako wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, hasa wale wa kikundi cha tohara. 11Hao ni lazima wanyamazishwe, kwa sababu wanaharibu watu wa nyumba nzima wakifundisha mambo yasiyowapasa kufundisha. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia mapato ya udanganyifu. 12Hata mmoja wa manabii wao mwenyewe amesema, “Wakrete ni waongo siku zote, wanyama wabaya, walafi, wavivu.” 13Ushuhuda huu ni kweli. Kwa hiyo, uwakemee kwa ukali wapate kuwa wazima katika imani, 14ili wasiendelee kuangalia hadithi za Kiyahudi au maagizo ya wale watu wanaoikataa kweli. 15Kwa wale walio safi, kila kitu ni safi kwao. Lakini kwa wale waliopotoka na wasioamini, hakuna chochote kilicho safi. Kwa kweli nia zao na dhamiri zao zimepotoka. 16Wanadai kumjua Mungu, lakini kwa matendo yao wanamkana. Hao watu ni chukizo, wasiotii, wasiofaa kwa jambo lolote jema.

Currently Selected:

Tito 1: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in