Mwanzo 49
49
Wasia wa Yakobo kwa wanawe
1 #
Kum 4:30; 33:1; Amo 3:7; Hes 24:14 Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku zijazo.
2 #
Zab 34:11
Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo,
Msikilizeni Israeli, baba yenu.
3 #
Kum 21:17
Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza,
Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu.
Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu.
4 #
Kum 27:20; 1 Nya 5:1 Umekuwa kama maji yavukavyo mpaka, basi nawe hutafana tena,
Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako,
Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu.
5 #
Mit 18:9; Mwa 34:25 Simeoni na Lawi ni ndugu;
Panga zao ni silaha za jeuri.
6 #
Mit 1:15; Zab 26:9 Nafsi yangu, usiingie katika siri yao,
Fahari yangu usiungane na kusanyiko lao,
Maana katika ghadhabu yao walimwua mtu,
Na kwa ukaidi wao walikata mshipa wa ng'ombe;
7 #
Yos 21:1; 1 Nya 4:24 Ghadhabu yao na ilaaniwe, maana ilikuwa kali,
Na hasira yao, maana ilikuwa haina huruma.
Nitawagawa katika Yakobo,
Nitawatawanya katika Israeli.
8Yuda, ndugu zako watakusifu,
Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako.
Wana wa baba yako watakuinamia.
9 #
Hes 24:9
Yuda ni mwanasimba,
Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda;
Aliinama akajilaza kama simba,
Na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha?
10 #
Hes 24:17; Zab 60:7; 1 Nya 5:2; Isa 11:1; Eze 21:27; Dan 9:25; Mt 21:9; Lk 1:32; Isa 2:2; 11:10; 60:1-5; Hag 2:7; Lk 2:30; 2 Fal 18:32 Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda,
Wala mfanya sheria kati ya miguu yake,
Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki,
Ambaye mataifa watamtii.
11Atafunga punda wake katika mzabibu,
Na mwanapunda wake katika mzabibu mzuri.
Amefua nguo zake kwa mvinyo,
Na mavazi yake kwa damu ya zabibu.
12Macho yake yatakuwa mekundu kwa mvinyo,
Na meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa.
13 #
Kum 33:18
Zabuloni atakaa pwani ya bahari,
Naye atakuwa kama pwani za kuegesha merikebu,
Na mpaka wake utakuwa kando ya Sidoni.
14Isakari ni punda hodari,
Ajilazaye kati ya mazizi ya kondoo;
15Akaona mahali pa raha, kuwa pema,
Na nchi, ya kuwa ni nzuri,
Akainama bega lake lichukue mizigo,
Akawa mtumishi kwa kazi ngumu.
16 #
Amu 13:2; 15:20 Dani atahukumu watu wake,
Kama moja ya makabila ya Israeli;
17 #
Amu 18:27
Dani atakuwa nyoka barabarani,
Bafe katika njia,
Aumaye visigino vya farasi,
Na apandaye akaanguka chali.
18 #
Zab 25:3,5; 62:5; Isa 25:9; 40:31; Rum 2:7; 1 Kor 1:7; Flp 3:20; Tit 2:13 Wokovu wako nimeungoja, Ee BWANA.
19 #
Kum 33:20
Gadi, jeshi litamsonga,
Lakini atawasonga wao mpaka visigino.
20Asheri, chakula chake kitakuwa kinono,
Naye atatoa tunu za kifalme.
21Naftali ni ayala aliyefunguliwa;
Anatoa maneno mazuri.
22Yusufu ni mti mchanga wenye kuzaa,
Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi,
Matawi yake yametanda ukutani.
23 #
Mwa 37:24
Wapiga mishale walimtenda machungu,
Wakamlenga na kumbana sana
24 #
Ayu 29:20; Zab 132:2,5; 80:1; Isa 28:16 Lakini upinde wake ukakaa imara,
Mikono yake ikapata nguvu,
Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo;
Kwa jina la mchungaji, yeye mwamba wa Israeli,
25 #
Kum 33:13
Naam, kwa Mungu wa baba yako atakayekusaidia;
Kwa baraka za juu mbinguni.
Baraka za vilindi vilivyo chini,
Baraka za maziwa, na za mimba.
26Baraka za baba yako
Ni nyingi kuliko za milima ya kale,
Vitu vinavyotamanika vya vilima vya milele;
Na vikae juu ya kichwa cha Yusufu,
Juu ya utosi wa kichwa chake, yeye aliyeteuliwa kati ya ndugu zake.
27 #
Amu 20:21,25; Hes 23:24; Est 8:11; Eze 39:10; Zek 14:1,7 Benyamini ni mbwamwitu mwenye kuraruararua
Asubuhi atakula mawindo,
Na jioni atagawanya mateka.
28Hayo yote ndiyo makabila ya Israeli kumi na mawili. Na hayo ndiyo aliyowaambia baba yao, na kuwabariki; mmoja mmoja kwa baraka zake aliwabariki.
Kufa kwa Yakobo na kuzikwa kwake
29 #
Mwa 15:15; 25:8; 2 Sam 19:37; Mwa 47:30; 50:13 Akawaamuru, akasema, Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti; 30#Mwa 23:16 katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua Abrahamu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia. 31#Mwa 23:19; 25:9; 35:29 Humo walimzika Abrahamu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka mkewe; nami humo nikamzika Lea; 32shamba na pango lililomo lililonunuliwa kwa wazawa wa Hethi. 33Basi Yakobo alipokwisha kuwaagiza wanawe, akakunja miguu yake kitandani, akafa, akakusanywa pamoja na watu wake.
Currently Selected:
Mwanzo 49: SRUV
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.