Mathayo 25
25
Mfano wa wanawali kumi
1 #
Lk 12:35; Ufu 19:7 Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. 2Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. 3Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; 4bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. 5Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. 6Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. 7Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao. 8Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika. 9Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie. 10Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa. 11#Lk 13:25 Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie. 12#Mt 7:23 Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi. 13#Mt 24:42 Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.
Mfano wa talanta
14 #
Lk 19:11-27
Maana itakuwa kama mfano wa mtu aliyetaka kusafiri, akawaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake.#Mt 21:33 15#Rum 12:6 Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. 16Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. 17Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. 18Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. 19Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. 20Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. 21#Mt 25:23; Mt 24:45-47; Lk 16:10 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. 22Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida. 23#Mt 25:21 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. 24Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nilitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; 25basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. 26Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; 27basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake. 28Basi, mnyang'anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi. 29#Mt 13:12; Mk 4:25; Lk 8:18 Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa. 30#Mt 8:12; 22:13; Lk 13:28 Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
Hukumu kwa mataifa
31 #
Mt 16:27; 19:28; Zek 14:5; Ufu 20:11-13 Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; 32#Rum 14:10 na mataifa yote yatakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; 33#Eze 34:17 atawaweka kondoo katika mkono wake wa kulia, na mbuzi mkono wake wa kushoto. 34Kisha Mfalme atawaambia wale walioko katika mkono wake wa kulia, Njooni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; 35#Isa 58:7 kwa maana nilikuwa na njaa, mkanipa chakula; nilikuwa na kiu, mkaninywesha; nilikuwa mgeni, mkanikaribisha; 36nilikuwa uchi, mkanivika nilikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nilikuwa kifungoni, mkanijia. 37#Mt 6:3 Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona ukiwa na njaa, tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38Tena ni lini tulipokuona ukiwa mgeni, tukakukaribisha, au ukiwa uchi, tukakuvika? 39Ni lini tena tulipokuona ukiwa mgonjwa, au ukiwa kifungoni, tukakujia? 40#Mit 19:17; Ebr 2:11 Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi. 41#Mt 7:23; Ufu 20:10,15 Kisha atawaambia na wale walioko katika mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; 42kwa maana nilikuwa na njaa, msinipe chakula; nilikuwa na kiu, msininyweshe; 43nilikuwa mgeni, msinikaribishe; nilikuwa uchi, msinivike; nilikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama. 44Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe ukiwa na njaa, au ukiwa na kiu, au ukiwa mgeni, au ukiwa uchi, au ukiwa mgonjwa, au ukiwa kifungoni, tusikuhudumie? 45Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. 46#Dan 12:2; Yn 5:29 Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.
Currently Selected:
Mathayo 25: SRUV
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.