Mathayo 26
26
Mpango wa kumwua Yesu
1 #
Mt 7:28; 11:1; 13:53; 19:1 Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake, 2#Mk 14:1,2; Lk 22:1,2 Mnajua ya kuwa baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, na Mwana wa Adamu atasalitiwa asulubiwe.#Kut 12:1-27; Mt 20:18 3Wakati ule wakuu wa makuhani, na wazee wa watu, wakakusanyika katika behewa ya Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa; 4wakafanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua. 5Lakini wakasema, Isiwe wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia miongoni mwa watu.
Yesu apakwa mafuta Bethania
6 #
Mk 14:3-9; Lk 7:36-50; Yn 12:1-8 Naye Yesu alipokuwapo Bethania katika nyumba ya Simoni mwenye ukoma, 7#Lk 7:37-38 mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya thamani kubwa alimkaribia akaimimina kichwani pake alipoketi chakulani. 8Wanafunzi wake walipoona, wakakasirika, wakasema, Ni wa nini upotevu huu? 9Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini. 10#Lk 11:7 Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi. 11#Kum 15:11 Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamko nami siku zote. 12Maana kwa kunimwagia mwili wangu marhamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu. 13Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu yake.
Yuda akubali kumsaliti Yesu
14 #
Mk 14:10,11; Lk 22:3-6 Wakati huo mmoja wa wale Kumi na Wawili, jina lake Yuda Iskarioti, aliwaendea wakuu wa makuhani, 15#Zek 11:12; Yn 11:57 akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha.#26:15 Yapata kama shilingi 90. 16#1 Tim 6:9,10 Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti.
Yesu katika Pasaka pamoja na wanafunzi
17 #
Mk 14:12-16; Lk 22:7-13 Katika siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka?#Kut 12:18-20 18#Mt 21:3 Akasema, Nendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. 19Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. 20#Mk 14:17-26; Lk 22:14-23; Yn 13:21-26 Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Kumi na Wawili. 21Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. 22Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? 23#Zab 41:10 Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika bakuli, ndiye atakayenisaliti. 24Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. 25Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.
Kuanzishwa kwa chakula cha Bwana
26 #
Mt 14:19; 1 Kor 11:23-25 Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu 27Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Kuyweni nyote katika hiki; 28#Kut 24:8; Yer 31:31-34; Zek 9:11 kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 29Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu. 30#Zab 113—118; Lk 22:39; Yn 18:1 Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda katika mlima wa Mizeituni.
Yesu asema kuwa Petro atamkana
31 #
Mk 14:27-31; Lk 22:31-34 Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.#Zek 13:7; Yn 16:32 32#Mt 28:7,16 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. 33Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe. 34#Yn 13:38 Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. 35#Mt 26:56 Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe. Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo.
Yesu aomba katika Gethsemane
36 #
Mk 14:32-42; Lk 22:40-46 Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe. 37#Ebr 5:7 Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. 38#Zab 43:5; Yn 12:27 Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. 39#Yn 18:11; Ebr 5:8 Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniondokee; lakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. 40Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41#Ebr 2:14; 4:15 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho iko radhi, lakini mwili ni dhaifu. 42Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniondokee nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. 43Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yalijawa na usingizi. 44#2 Kor 12:8 Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale. 45Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi. 46#Yn 14:31 Ondokeni, twende zetu! Tazama, yule anayenisaliti amekaribia.
Kusalitiwa na kukamatwa kwa Yesu
47 #
Mk 14:43-50; Lk 22:47-53; Yn 18:3-12 Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Kumi na Wawili akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu. 48Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni. 49Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu. 50Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu. 51Na tazama, mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. 52#Mwa 9:6; Ufu 13:10 Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. 53#Yoe 3:11 Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? 54Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri? 55#Lk 19:47; 21:37 Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang'anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku niliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. 56#Mt 26:31 Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
Yesu mbele ya Kuhani Mkuu
57 #
Mk 14:53-72; Lk 22:54-71; Yn 18:12-27 Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee. 58Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho. 59Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; 60wasiuone ingawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. 61#Yn 2:19-21 Na baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu. 62Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? 63#Mt 27:12 Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu. 64#Dan 7:13; Zab 110:1; Mt 16:27; 24:30 Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi katika mkono wa kulia wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni. 65#Law 24:16; Mt 9:3; Yn 10:33 Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake; 66#Yn 19:7 mwaonaje ninyi? Wakajibu, wakasema, Imempasa kuuawa. 67#Isa 50:6 Ndipo wakamtemea mate usoni, wakampiga ngumi; na wengine wakampiga makofi, 68wakisema, Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga?
Petro amkana Yesu
69Na Petro alikuwa ameketi nje uani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya. 70Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo. 71Naye alipotoka nje hadi ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti. 72Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu. 73Punde kidogo, wale waliokuwapo wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. 74Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara jogoo akawika. 75#Mt 26:34 Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, Kabla ya jogoo kuwika, utanikana mara tatu. Akatoka nje, akalia kwa majonzi.
Currently Selected:
Mathayo 26: SRUV
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.