Matendo 10
10
Petro na Kornelio
1Kulikuwa mtu aliyeitwa Kornelio katika mji wa Kaisaria. Mtu huyu alikuwa ofisa wa kikosi kilichoitwa “Kikosi cha Kiitalia” katika jeshi la Rumi. 2Alikuwa mcha Mungu. Yeye na watu wengine wote walioishi katika nyumba yake walikuwa wanamwabudu Mungu wa kweli. Alitoa pesa zake nyingi kuwasaidia maskini miongoni mwa Wayahudi na daima alimwomba Mungu kwa kufuata utaratibu kama ilivyokuwa. 3Mchana mmoja yapata saa tisa, kwa uwazi na dhahiri Kornelio aliona maono. Alimwona malaika kutoka kwa Mungu akimwendea na akamwambia, “Kornelio!”
4Akiwa anashangaa na kuogopa, Kornelio akasema, “Unataka nini, bwana?”
Malaika akamwambia, “Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako unazowapa maskini. Anakukumbuka kwa yote uliyotenda. 5Tuma baadhi ya watu sasa waende katika mji wa Yafa wakamlete mtu anayeitwa Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 6Anakaa kwa mtu ambaye naye pia anaitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko kwenye ufukwe wa bahari.” 7Malaika aliyeongea na Kornelio akaondoka. Ndipo Kornelio aliita watumishi wake wawili na askari mmoja. Askari alikuwa mcha Mungu, mmoja wa wasaidizi wake wa karibu. 8Kornelio akawaelekeza kila kitu watu hawa watatu kisha akawatuma kwenda Yafa.
9Siku iliyofuata wakati wa adhuhuri walipokuwa wanaukaribia mji wa Yafa, Petro alipanda juu ya paa#10:9 paa Nyakati za Biblia, nyumba zilikuwa na paa zilizosawa kama sakafu, zilizotumika kama vyumba vya ziada au sehemu za kufanyia mazungumzo. kuomba. 10Alihisi njaa na akataka chakula. Lakini walipokuwa wanamwandalia chakula ili ale, aliona maono. 11Aliona mbingu zikifunguka na kitu kama shuka kubwa kikishushwa chini kutoka mbinguni kwa pembe nne. 12Ndani yake mlikuwa aina zote za wanyama, watambaao na ndege. 13Kisha sauti ikamwambia, “Petro simama uchinje chochote hapa kisha ule.”
14Lakini Petro akasema, “Siwezi kufanya hivyo, Bwana! Sijawahi kula kitu chochote kisicho safi au kisicho stahili kutumiwa kwa chakula.”
15Lakini sauti ikamwambia tena, “Mungu amekwisha vitakasa vitu vyote hivi. Usiseme havistahili kuliwa.” 16Hili lilimtokea mara tatu. Kisha likachukuliwa mbinguni. 17Petro alijiuliza maono haya yalikuwa na maana gani.
Watu ambao Kornelio aliwatuma walishaiona nyumba ya Simoni na walikuwa wamesimama mlangoni. 18Waliuliza, “Je! Simoni Petro yuko hapa?”
19Petro akiwa bado anafikiri kuhusu maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Sikiliza, kuna watu watatu wanakutafuta. 20Inuka na ushuke chini. Nenda nao, usisite, kwa sababu nimewatuma.” 21Hivyo Petro akashuka chini na kuwaambia, “Nafikiri mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja hapa?”
22Wale watu wakasema, “Malaika mtakatifu amemwambia Kornelio akualike nyumbani mwake. Ni mtu mwema na hutenda kwa haki, na anamwabudu Mungu na Wayahudi wote wanamheshimu. Malaika alimwambia akualike nyumbani kwake ili asikilize yale utakayosema.” 23Petro akawakaribisha ndani watu wale ili walale usiku huo.
Siku iliyofuata Petro alijiandaa na kuondoka na wale watu watatu. Baadhi ya waamini katika mji wa Yafa walikwenda pamoja naye. 24Siku iliyofuata walifika katika mji wa Kaisaria. Kornelio alikuwa anawasubiri na alikuwa amewakusanya jamaa na rafiki zake wa karibu nyumbani mwake.
25Petro alipoingia ndani ya nyumba, Kornelio alimlaki kisha akaanguka miguuni kwa Petro na akamwabudu. 26Lakini Petro akamwambia asimame. Petro akasema, “Simama! Mimi ni mtu tu kama wewe.” 27Petro aliendelea kuzungumza na Kornelio. Ndipo Petro akaingia ndani na kuona kundi kubwa la watu wamekusanyika pale.
28Petro akawaambia watu wale kuwa, “Mnaelewa kuwa ni kinyume na sheria yetu kwa Myahudi kushirikiana au kumtembelea mtu ambaye si Myahudi. Lakini Mungu amenionyesha kuwa nisimchukulie mtu yeyote kuwa yu kinyume na desturi za Kiyahudi. 29Ndiyo sababu sikubisha watu wenu waliponiambia kuja hapa. Sasa, tafadhali niambieni kwa nini mmeniita hapa.”
30Kornelio akasema, “Siku nne zilizopita, kama saa tisa mchana nilikuwa ninaomba ndani ya nyumba yangu. Ghafla akawepo mtu mmoja amesimama mbele yangu amevaa mavazi meupe yanayong'aa. 31Akasema, ‘Kornelio, Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako kwa maskini. Anakukumbuka wewe na yote uliyofanya. 32Hivyo tuma baadhi ya watu kwenye mji wa Yafa na wamwambie Simoni Petro kuja. Anakaa na mtu mwingine anayeitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko pembeni mwa bahari.’ 33Hivyo nikawatuma kwako haraka. Imekuwa vizuri sana umekuja hapa. Sasa sote tupo hapa mbele za Mungu na tuko tayari kusikia kila kitu ambacho Bwana amekwamuru utuambie.”
Petro Ahubiri Katika nyumba ya Kornelio
34Petro akaanza kwa kusema: “Hakika sasa ninaelewa ni kwa nini Mungu hawachukulii kundi fulani la watu kuwa bora kuliko wengine. 35Anamkubali yeyote anayemwabudu na anayetenda haki. Haijalishi wanatoka katika taifa lipi. 36Mungu amezungumza na watu wa Israeli. Aliwaletea Habari Njema kwamba amani imekuja kupitia Yesu Kristo ambaye ndiye Bwana wa watu wote.
37Mnafahanu kilichotokea katika Uyahudi yote. Kilianzia Galilaya baada ya Yohana kuwaambia watu kuwa inawapasa kubatizwa. 38Mnajua kuhusu Yesu kutoka Nazareti. Mungu alimfanya Masihi kwa kumpa Roho Mtakatifu na nguvu. Yesu alikwenda kila mahali akiwatendea mema watu. Akawaponya wale waliokuwa wakitawaliwa na yule Mwovu, akionyesha kuwa Mungu alikuwa pamoja naye.
39Tuliona yote ambayo Yesu alitenda katika Uyahudi na katika mji wa Yerusalemu. Lakini aliuawa. Walimpigilia kwenye msalaba uliotengenezwa kwa mti. 40Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, Mungu alimfufua na kumfanya aonekane wazi wazi. 41Hakuonekana kwa Wayahudi wote, lakini alionekana kwetu sisi tu, ambao Mungu tayari alikwisha kutuchagua tuwe mashahidi. Tulikula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu.
42Yesu alitwambia twende na kuwaeleza watu. Alituagiza tuwaeleza kwamba yeye ndiye ambaye Mungu amemchagua kuwa mwamuzi wa wote walio hai na wote walio kufa. 43Na ya kwamba kila atakayemwamini Yesu, atasamehewa dhambi zake kupitia nguvu jina Lake. Manabii wote wanakubali kuwa jambo hili ni la kweli.”
Roho Mtakatifu Awashukia Watu Wasio Wayahudi
44Petro alipokuwa bado anazungumza, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanamsikiliza. 45Waamini wa Kiyahudi waliofuatana na Petro walishangaa kwamba Roho Mtakatifu amemiminwa kama zawadi hata kwa watu wasio Wayahudi. 46Waliwasikia wakiongea lugha mbalimbali na kumsifu Mungu. Ndipo Petro akasema, 47“Je! mtu yeyote anawezaje kuzuia watu hawa wasibatizwe katika maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea!” 48Hivyo Petro akawaambia wambatize Kornelio pamoja na jamaa zake na rafiki zake katika jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba Petro akae nao kwa siku chache.
Currently Selected:
Matendo 10: TKU
Highlight
Share
Copy

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International