YouVersion Logo
Search Icon

Matendo 11

11
Petro Arudi Yerusalemu
1Mitume na waamini katika Uyahudi walisikia kwamba watu wasio Wayahudi wameyapokea mafundisho ya Mungu pia. 2Lakini Petro alipokuja Yerusalemu, baadhi ya waamini wa Kiyahudi#11:2 waamini wa Kiyahudi Kwa maana ya kawaida, “watu wa tohara”. Hii inaweza kuwa na maana ya Wayahudi waliodhani kuwa wafuasi wote wa Kristo ni lazima watahiriwe na kutii Sheria ya Musa. Tazama Gal 2:12. walimkosoa. 3Walisema, “Uliingia katika nyumba za watu wasio Wayahudi ambao hawajatahiriwa na ukala pamoja nao!”
4Hivyo Petro akawaelezea namna ilivyotokea. 5Akasema, “Nilikuwa katika mji wa Yafa. Nilipokuwa nikiomba, niliona maono. Niliona kitu kikishuka chini kutoka mbinguni. Kilionekana kama shuka kubwa ikishushwa chini kwa pembe zake nne. Kikaja chini karibu yangu. 6Nilipotazama ndani yake, niliona aina zote za wanyama, pamoja na wale wa porini, wanyama wanaotambaa na ndege. 7Nilisikia sauti ikiniambia. Chinja chochote hapa na ule!”
8“Lakini nilisema, ‘Siwezi kufanya hivyo Bwana! Sijawahi kula kitu cho chote kisicho safi au kisichostahili kuliwa kama chakula.’
9Lakini sauti kutoka mbinguni ikajibu tena, ‘Mungu amevitakasa vitu hivi. Usiseme havistahili kuliwa!’
10Hili lilitokea mara tatu. Ndipo kitu chote kikachukuliwa kurudi mbinguni. 11Saa hiyo hiyo baada ya hayo wakawepo watu watatu wamesimama nje ya nyumba nilimokuwa ninakaa. Walikuwa wametumwa kutoka Kaisaria kunichukua. 12Roho Mtakatifu aliniambia niende nao bila kuwa na mashaka. Ndugu hawa hapa sita walikwenda pamoja nami, na tulikwenda katika nyumba ya Kornelio. 13Alitwambia kuhusu malaika aliyemwona amesimama katika nyumba yake. Malaika alimwambia, ‘Tuma baadhi ya watu waenda Yafa kumchukua Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 14Atazungumza na wewe. Ujumbe atakaokwambia utakuokoa wewe na kila mtu anayeishi katika nyumba yako.’
15Nilipoanza kuzungumza, Roho Mtakatifu alikuja juu yao kama vile alivyokuja juu yetu mwanzo.#11:15 mwanzo Siku ya Pentekoste katika Mdo 2, Roho Mtakatifu alipowashukia wafuasi wa mwanzo wa Yesu na kuwapa nguvu ya kuanza kuuhubiri ulimwengu Habari Njema za wokovu kupitia Yesu. 16Ndipo nilikumbuka maneno ya Bwana Yesu, aliyosema: ‘Yohana alibatiza katika maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17Mungu amewapa watu hawa karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo. Hivyo ningewezaje kupinga yale ambayo Mungu alitaka kufanya?”
18Waamini wa Kiyahudi waliposikia hili, wakaacha kubisha. Wakamsifu Mungu na kusema, “Kwa hiyo Mungu anawaruhusu watu wasio Wayahudi kubadili mioyo yao na kuwa na maisha anayotoa!”
Habari Njema Zafika Antiokia
19Waamini walitawanyika kwa sababu ya mateso#11:19 mateso Au “kipindi cha mateso”. Hiki ni kipindi ambacho viongozi wa Kiyahudi katika mji wa Yerusalemu walikuwa wakiwaadhibu watu wanaomwamini Kristo. Tazama Mdo 8:1-4. yaliyoanza baada ya Stefano kuuawa. Baadhi ya waamini walikwenda mbali mpaka Foeniki, Kipro na Antiokia. Walihubiri Habari Njema katika maeneo haya, lakini kwa Wayahudi tu. 20Baadhi ya waamini hawa walikuwa watu kutoka Kipro na Kirene. Watu hawa walipofika Antiokia, walianza kuwahubiri watu wasio Wayahudi.#11:20 watu wasio Wayahudi Kwa maana ya kawaida, “Wa mataifa” au “Wahelenisti”, au watu waliochangamana na kuathiriwa na utamaduni wa Kiyunani (Kigiriki). Nakala zingine za Kiyunani zina “Wayunani” au “Wagiriki”. Waliwahubiri Habari Njema kuhusu Bwana Yesu. 21Nguvu ya Bwana iliambatana na watu hawa, na idadi kubwa ya watu waliamini na kuamua kumfuata Bwana.
22Kanisa katika mji wa Yerusalemu liliposikia kuhusu hili, lilimtuma Barnaba kwenda Antiokia. 23-24Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu na imani. Alipokwenda Antiokia na kuona jinsi Mungu alivyowabariki waamini pale, alifurahi sana. Akawatia moyo wote, akasema, “Iweni waaminifu kwa Bwana daima. Mtumikieni Yeye kwa mioyo yenu yote.” Watu wengi zaidi wakawa wafuasi wa Bwana.
25Kisha Barnaba alikwenda katika mji wa Tarso kumtafuta Sauli. 26Alipompata, alimpeleka Antiokia. Walikaa pale mwaka mzima. Kila wakati kanisa lilipokusanyika, Barnaba na Sauli walikutana nao na kuwafundisha watu wengi. Ni katika mji wa Antiokia ambako wafuasi wa Bwana Yesu walianza kuitwa “Wafuasi wa Kristo”.#11:26 Wafuasi wa Kristo Yaani, Wakristo.
27Katika wakati huo huo baadhi ya manabii walitoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. 28Mmoja wao, aliyeitwa Agabo, huku akisaidiwa na Roho Mtakatifu, alisimama na kuzungumza. Alisema, “Wakati mbaya sana unakuja katika dunia yote. Hakutakuwa chakula kwa ajili ya watu kula.” (Kipindi hiki cha njaa kilitokea Klaudio alipokuwa mtawala wa Kirumi) 29Wafuasi wa Bwana wakaamua kwamba kila mmoja wao atatuma kiasi anachoweza kuwasaidia ndugu wote#11:29 ndugu wote Yaani, Jamaa yote ya Waamini. wanaoishi Uyahudi. 30Walikusanya pesa na kuwapa Barnaba na Sauli, waliozipeleka kwa wazee, katika Uyahudi.

Currently Selected:

Matendo 11: TKU

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

Video for Matendo 11