Matendo 6
6
Watu Saba Wachaguliwa kwa Kazi Maalumu
1Watu wengi zaidi walipokuwa wafuasi wa Yesu. Wafuasi waliokuwa wakizungumza Kiyunani walianza kuwalalamikia wafuasi wenzao waliokuwa wanazungumza Kiebrania au Kiaramu. Walisema kuwa wajane wao walikuwa hawapewi mgao wao kutokana na kile wafuasi walikuwa wanapewa kila siku. 2Mitume kumi na mbili wakaita kundi lote la wafuasi pamoja.
Mitume wakawaambia, “Haitakuwa sahihi sisi kuacha kazi yetu ya kuwafundisha watu neno la Mungu ili tuwe wasimamizi wa ugawaji wa chakula kwa watu. 3Hivyo, kaka zetu na dada zetu, chagueni wanaume saba miongoni mwenu wenye ushuhuda mzuri, watu waliojaa hekima na Roho. Nasi tutawaweka kuwa wasimamizi wa kazi hii muhimu. 4Na hivyo itatuwezesha sisi kutumia muda wetu wote katika kuomba na kufundisha neno la Mungu.”
5Kundi lote la waamini likakubaliana na wazo hili. Hivyo wakawachagua wanaume saba: Stefano (aliyejaa imani na Roho Mtakatifu), Filipo,#6:5 Filipo Siyo mtume aliyeitwa Filipo. Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena, na Nikolasi (mtu wa Antiokia aliyeongoka na kufuata dini ya Kiyahudi). 6Kisha, wakawaweka watu hawa mbele ya mitume, nao mitume waliwaombea na kuweka mikono juu yao.
7Neno la Mungu lilikuwa linawafikia watu wengi zaidi. Kundi la wafuasi katika Yerusalemu likawa kubwa sana. Hata idadi kubwa ya makuhani wa Kiyahudi waliamini na kutii.
Baadhi ya Wayahudi Wampinga Stefano
8Mungu alimpa Stefano nguvu ya kutenda maajabu makuu na miujiza katikati ya watu. 9Lakini baadhi ya Wayahudi pale waliotoka katika sinagogi la Watu Huru,#6:9 Watu Huru Wayahudi waliokuwa watumwa au ambao baba zao walikuwa watumwa, lakini wao walikuwa huru. kama lilivyoitwa. Kundi hili lilijumuisha Wayahudi kutoka Kirene, Iskanderia, Kilikia na Asia. Walianza kubishana na Stefano. 10Lakini Roho Mtakatifu alimwezesha kuzungumza kwa hekima. Maneno yake yalikuwa na nguvu hata Wayahudi hawa hawakuweza kubishana naye.
11Hivyo wakawaambia baadhi ya watu waseme, “Tumemsikia Stefano akimtukana Musa na Mungu!” 12Jambo hili liliwakasirisha sana watu, wazee wa Kiyahudi na walimu wa sheria. Wakamkamata Stefano na kumpeleka mbele ya Baraza Kuu.
13Wayahudi wakawaleta baadhi ya watu kwenye mkutano ili kusema uongo kuhusu Stefano. Watu hawa walisema, “Daima mtu huyu husema maneno kinyume na mahali hapa patakatifu na kinyume na Sheria ya Musa. 14Tulimsikia akisema kwamba Yesu kutoka Nazareti atapaharibu mahali hapa na kubadilisha yale ambayo Musa aliyotuambia kufanya.” 15Kila mtu aliyekuwa kwenye mkutano wa baraza alikuwa akimshangaa Stefano kwani uso wake ulionekana kama uso wa malaika.
Currently Selected:
Matendo 6: TKU
Highlight
Share
Copy

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International