Matendo 7
7
Hotuba ya Stefano
1Kuhani mkuu akamwambia Stefano, “Mambo haya ndivyo yalivyo?” 2Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu Wayahudi, nisikilizeni! Mungu wetu mkuu na mwenye utukufu alimtokea Abrahamu, baba yetu, alipokuwa Mesopotamia. Kabla hajahamia Harani. 3Mungu alimwambia, ‘Ondoka katika nchi yako na watu wako, kisha uende katika nchi nitakayokuonesha.’#Mwa 12:1
4Hivyo Abrahamu akaondoka katika nchi ya Ukaldayo#7:4 Ukaldayo Au “Babeli”, nchi iliyo kusini mwa Mesopotamia. Tazama mstari wa 2. na kwenda kuishi Harani. Baada ya baba yake kufa, Mungu akamleta katika nchi hii, mahali mnapoishi sasa. 5Lakini Mungu hakumpa Abrahamu sehemu yoyote ya ardhi hii, hata eneo dogo lenye ukubwa wa unyayo wake. Lakini Mungu aliahidi kuwa atampa Abrahamu nchi hii yeye na watoto wake hapo baadaye. Hii ilikuwa kabla Abrahamu hajapata watoto.
6Mungu alimwambia: ‘Wazao wako wataishi katika nchi nyingine. Watakuwa wageni. Watu wa huku watawafanya kuwa watumwa na kuwatendea vibaya kwa miaka mia nne. 7Lakini nitaliadhibu taifa lililowafanya watumwa.’#Mwa 15:13-14 Pia, Mungu alisema, ‘Baada ya mambo hayo kutokea, watu wako watatoka katika nchi hiyo. Kisha wataniabudu mahali hapa.’#Mwa 15:14; Kut 3:12
8Mungu aliweka agano na Abrahamu; alama ya agano hili ilikuwa tohara. Na Abrahamu alipopata mwana, alimtahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa. Jina la mwanaye lilikuwa Isaka. Pia, Isaka alimtahiri mwanaye Yakobo. Na Yakobo alifanya vivyo hivyo kwa wanaye, ambao ndiyo baba wakuu kumi na mbili wa watu wetu.
9Baba zetu hawa walimwonea wivu Yusufu ndugu yao na wakamwuza ili awe mtumwa Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, 10akamwokoa kutoka katika matatizo yake yote. Wakati huo Farao alikuwa mfalme wa Misri. Alimpenda na akamheshimu Yusufu kwa sababu ya hekima ambayo Mungu alimpa. Farao alimfanya Yusufu kuwa gavana wa Misri na msimamizi wa watu wote na kila kitu katika kasri lake. 11Lakini nchi yote ya Misri na Kanaani zikakosa mvua na mazao ya chakula hayakuweza kuota. Watu waliteseka sana na watu wetu hawakuweza kupata chakula chochote.
12Lakini Yakobo aliposikia kulikuwa chakula Misri aliwatuma mababa zetu huko. Hii ilikuwa safari yao ya kwanza kwenda Misri. 13Kisha walikwenda safari ya pili. Safari hii Yusufu akawaeleza ndugu zake yeye ni nani. Ndipo Farao akatambua kuhusu familia ya Yusufu. 14Kisha Yusufu aliwatuma kaka zake wamwambie Yakobo, baba yake, ahamie Misri. Aliwaalika pia ndugu zake wote, jumla yao wote walikuwa watu sabini na tano. 15Hivyo Yakobo alitelemka kwenda Misri. Yeye na baba zetu waliishi huko mpaka walipokufa. 16Baadaye, miili yao ilihamishiwa Shekemu, ambako iliwekwa katika kaburi ambalo Abrahamu alilinunua kwa fedha kutoka kwa wana wa Hamori.
17Watu wetu walipokuwa Misri idadi yao iliongezeka. Watu wetu walikuwa wengi mno huko. Ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa Abrahamu ilikuwa karibu kutimia. 18Ndipo mfalme mwingine akaanza kutawala Misri, ambaye hakujua lolote kuhusu Yusufu. 19Mfalme huyu aliwahadaa watu wetu. Akawatendea vibaya sana, akawalazimisha wawaache watoto wao nje ili wafe.
20Huu ni wakati ambapo Musa alizaliwa. Alikuwa mtoto mzuri sana, na kwa miezi mitatu wazazi wake walimtunza nyumbani. 21Walipolazimishwa kumtoa nje, Binti wa Farao alimchukua. Alimkuza kama mwanaye wa kumzaa. 22Musa alielimishwa kwa elimu bora ya Kimisri. Wamisri walimfundisha kila kitu walichojua. Alikuwa mwenye nguvu katika yote aliyosema na kutenda.
23Musa alipokuwa na umri wa miaka kama arobaini, aliamua kuwatembelea watu wake mwenyewe, watu wa Israeli. 24Aliona mmoja wao ananyanyaswa na Mmisri, hivyo akamtetea; Musa akampiga na kumwua Mmisri ili kulipiza kwa kumwumiza Mwisraeli. 25Musa alidhani kwamba watu wake wangeelewa kuwa Mungu alikuwa anamtumia kuwaokoa. Lakini hawakuelewa.
26Siku iliyofuata, Musa akawaona wawili wa watu wake wakipigana. Alijaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Ninyi ni ndugu! Kwa nini mnataka kuumizana?’ 27Aliyekuwa akimwumiza mwenzake akamsukuma Musa na akamwambia, ‘Nani amekufanya wewe uwe mtawala na mwamuzi wetu? 28Unataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri jana?’#Kut 2:14 29Musa alipomsikia akisema hili, alikimbia Misri. Alikwenda kuishi Midiani kama mgeni. Katika kipindi alichoishi huko, alipata wana wawili.
30Miaka arobaini baadaye, Musa alipokuwa jangwani karibu na Mlima Sinai, malaika alimtokea katika mwali wa moto uliokuwa unawaka katika kichaka. 31Musa alipoliona hili, alishangaa. Alisogea ili kuangalia kwa karibu. Akasikia sauti; ilikuwa sauti ya Bwana. 32Bwana alisema, ‘Mimi ni Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zako. Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo.’#Kut 3:6 Musa akaanza kutetemeka kwa woga. Aliogopa kukitazama kichaka.
33Kisha Bwana akamwambia, ‘Vua viatu vyako, kwa sababu mahali uliposimama ni ardhi takatifu. 34Nimewaona watu wangu wanavyoteseka sana Misri. Nimesikia watu wangu wakilia na nimeshuka ili kuwaokoa. Njoo sasa, Musa, ninakutuma urudi Misri.’#Kut 3:5-10
35Huyu ni Musa ndiye aliyekataliwa na watu wake. Walisema, ‘Nani amekufanya uwe mtawala na mwamuzi wetu?’#Kut 2:14 Lakini ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mtawala na mwokozi. Mungu alimtuma pamoja na msaada wa malaika,#7:35 Hapa inamaanisha kuwa Musa aliambatana na nguvu za Mungu na ulinzi wa malaika. ambaye Musa alimwona katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. 36Hivyo Musa aliwaongoza watu kutoka Misri. Alitenda maajabu na ishara za miujiza Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa miaka arobaini.
37Huyu ni Musa yule yule aliyewaambia maneno haya watu wa Israeli: ‘Mungu atakupa nabii. Nabii huyo atakuja kutoka miongoni mwa watu wako mwenyewe. Atakuwa kama mimi.’#Kum 18:15 38Musa huyo huyo alikuwa pamoja na kusanyiko la watu wa Mungu jangwani. Alikuwa na malaika aliyezungumza naye alipokuwa Mlima Sinai, na alikuwa pamoja na baba zetu. Alipokea maneno yaletayo uzima kutoka kwa Mungu, na Musa akatupa sisi Maneno hayo.
39Lakini baba zetu hawakutaka kumtii Musa. Walimkataa, wakataka kurudi Misri. 40Walimwambia Haruni, ‘Musa alituongoza kutoka katika nchi ya Misri. Lakini hatujui kilichompata. Hivyo tengeneza miungu ili iwe mbele yetu ituongoze.’#Kut 32:1 41Hivyo watu wakatengeneza kinyago kinachofanana na ndama. Kisha wakakitolea sadaka za kuteketezwa. Walifurahia kile walichotengeneza kwa mikono yao wenyewe. 42Lakini Mungu akawaacha, nao wakaendelea kuabudu nyota na sayari.#7:42 nyota na sayari Ama jeshi lililoko angani. Nyakati za kale watu waliamini kuwa nyota na sayari zilikuwa miungu au malaika. Kitabu cha manabii#7:42 Kitabu cha manabii Hiki ni kitabu cha manabii wadogo kumi na mbili: Kuanzia Hosea mpaka Malaki. kinasema hivi:
‘Watu wa Israeli, hamkunipa dhabihu
jangwani kwa miaka arobaini.
43Mlibeba hema kwa ajili ya kumwabudia Moleki,
na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani.
Hizi zilikuwa sanamu mlizotengeneza ili mziabudu.
Hivyo nitawahamishia mbali, kuvuka Babeli.’#Amo 5:25-27
44Baba zetu walikuwa na Hema Takatifu walipokuwa jangwani. Mungu alimwelekeza Musa jinsi ya kutengeneza hema hii. Aliitengeneza kwa kufuata ramani aliyoonyeshwa na Mungu. 45Baadaye, Yoshua aliwaongoza baba zetu kuteka ardhi ya mataifa mengine. Watu wetu waliingia, na Mungu akawafukuza watu wengine. Watu wetu walipoingia katika ardhi hii mpya, waliibeba hema hii pamoja nao. Watu wetu waliipata hema hii kutoka kwa baba zao, na watu wetu waliitunza mpaka wakati wa Daudi. 46Mungu alimpenda Daudi.#7:46 Mungu alimpenda Daudi Au “alipendelewa na Mungu”. Na Daudi akamwomba Mungu amruhusu ajenge Hekalu kwa ajili ya watu wa Israeli#7:46 watu wa Israeli Kwa maana ya kawaida, “nyumba ya Yakobo”. Nakala zingine za Kiyunani zina “Mungu wa Yakobo”. 47Lakini Sulemani ndiye aliyemjengea Mungu Hekalu.
48Lakini Mungu Aliye Juu sana hahitaji yumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu ili aishi ndani yake. Nabii aliandika hivi:
49‘Bwana asema, Mbingu ni kiti changu cha enzi,
na dunia ni sehemu ya kuweka miguu yangu.
Hivyo mnadhani mnaweza kunijengea nyumba?
Je! ninahitaji mahali pa kupumzika?
50Kumbukeni, niliumba vitu vyote hivi?’”#Isa 66:1-2
51Kisha Stefano akasema, “Enyi viongozi wa Kiyahudi mlio wakaidi! Mnakataa kumpa Mungu mioyo yenu na mnakataa hata kumsikiliza. Daima mko kinyume na Roho Mtakatifu. Baba zenu walikuwa vivyo hivyo, nanyi mko kama wao! 52Walimtesa kila nabii aliyewahi kuishi. Waliwaua hata wale ambao zamani zilizopita walisema kwamba Mwenye Haki ilikuwa aje. Na sasa mmekuwa kinyume na Mwenye Haki na mmemwua. 53Ninyi ndiyo mliipokea Sheria ya Mungu,#7:53 Sheria ya Mungu Yaani Torati. aliyoitoa kupitia malaika zake. Lakini hamtaki kuitii!”
Stefano Auawa
54Waliokuwa kwenye mkutano wa baraza waliposikia maneno haya, walikasirika sana na wakamsagia meno Stefano kwa hasira. 55Lakini Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alitazama juu mbinguni, na kuuona utukufu wa Mungu. Alimwona Yesu amesimama upande wa kulia wa Mungu. 56Stefano akasema, “Tazama! Naona mbingu zimefunguka. Na ninamwona Mwana wa Adamu amesimama upande wa kulia wa Mungu.”
57Kila mmoja pale akaanza kupiga kelele, wakaziba masikio yao kwa mikono yao. Wote kwa pamoja wakamvamia Stefano. 58Wakamtoa nje ya mji na kuanza kumpiga kwa mawe. Mashahidi walioshuhudia uongo kinyume cha Stefano waliacha makoti yao kwa kijana aliyeitwa Sauli. 59Walipokuwa wanampiga kwa mawe, Stefano aliomba, akisema, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60Alianguka kwa magoti yake na kupaza sauti, akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii!” Haya yalikuwa maneno yake ya mwisho kabla ya kufa.
Currently Selected:
Matendo 7: TKU
Highlight
Share
Copy

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International