Luka 20
20
Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mt 21:23-27; Mk 11:27-33)
1Siku moja Yesu alikuwa anawafundisha watu katika eneo la Hekalu. Alikuwa anawahubiri Habari njema. Viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikwenda kuzungumza na Yesu. 2Wakamwambia, “Tuambie, una mamlaka gani kutenda mambo haya! Ni nani aliyekupa mamlaka hii?”
3Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali pia. Niambieni: 4Yohana alipobatiza watu, mamlaka yake ilitoka kwa Mungu au kwa watu fulani?”
5Makuhani, walimu wa sheria na viongozi wa Kiyahudi wakajadiliana kwa pamoja kuhusu hili. Wakasema, “Kama tukijibu ‘Ubatizo wa Yohana ulitoka kwa Mungu,’ atasema, ‘Sasa kwa nini hamkumwamini Yohana?’ 6Lakini kama tukisema ulitoka kwa watu fulani, watu hawa watatupiga kwa mawe mpaka tufe. Kwa sababu wote wanaamini Yohana alikuwa nabii.” 7Hivyo wakajibu, “Hatujui.”
8Ndipo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni nani alinipa mamlaka kufanya mambo haya.”
Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu
(Mt 21:33-46; Mk 12:1-12)
9Yesu akawaambia watu kisa hiki; “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Kisha akalikodisha kwa wakulima, kisha akasafiri kwa muda mrefu. 10Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, alimtuma mmoja wa watumishi wake kwa wakulima wale ili wampe sehemu yake ya zabibu. Lakini wakulima wale walimpiga yule mtumishi na wakamfukuza bila kumpa kitu. 11Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi mwingine. Wakulima walimpiga mtumishi huyu pia, wakamwaibisha na kumfukuza bila kumpa kitu. 12Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi wa tatu. Wakulima wakampiga sana mtumishi huyu na wakamtupa nje ya shamba la mizabibu.
13Mmiliki wa shamba la mizabibu akasema, ‘Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa. Yumkini watamheshimu.’ 14Lakini wakulima walipomwona mwana wa mwenye shamba, wakajadiliana wakisema, ‘Huyu ni mwana wa mmiliki wa shamba. Shamba hili la mizabibu litakuwa lake. Tukimwua, litakuwa letu.’ 15Hivyo wakulima wakamtupa mwana wa mmiliki wa shamba nje ya shamba la mizabibu na wakamwua.
Je! mmiliki wa shamba la mizabibu atafanya nini? 16Atakuja na atawaua wale wakulima, kisha atalikodisha shamba kwa wakulima wengine.”
Watu waliposikia mfano huu, wakasema, “Hili lisije kutokea!” 17Lakini Yesu akawakazia macho na akasema, “Hivyo basi, Maandiko haya yanamaanisha nini:
‘Jiwe lililokataliwa na wajenzi,
limekuwa jiwe kuu la pembeni?’#20:17 Zab 118:22. Yesu, ambaye ndiye “Jiwe” katika Zaburi hii, anajitambulisha mwenyewe kama mwana katika simulizi hii ambapo anauawa na wakulima wale. Tazama Mdo 4:11.
18Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika na ikiwa jiwe hilo litaangukia, litakusaga!”
19Walimu wa sheria na wakuu wa makuhani waliposikia kisa hiki, walijua unawahusu wao. Hivyo walitaka kumkamata Yesu wakati huo huo, lakini waliogopa watu wangewadhuru.
Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego
(Mt 22:15-22; Mk 12:13-17)
20Hivyo viongozi wa Kiyahudi walitafuta namna ya kumtega Yesu. Walituma watu waliojifanya kuwa wenye haki, ili waweze kumnasa ikiwa angesema jambo ambalo wangeweza kutumia kinyume naye. Ikiwa angesema jambo lolote baya, wangemkamata na kumpeleka kwa gavana wa Kirumi, mwenye mamlaka ya kumhukumu na kumwadhibu. 21Hivyo wale watu wakamwambia Yesu, “Mwalimu, tunafahamu kwamba yale unayosema na kufundisha ni kweli. Haijalishi ni nani anasikiliza, unafundisha sawa kwa watu wote. Daima unafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu. 22Tuambie, ni sahihi sisi kulipa kodi kwa Kaisari, au si sahihi?”
23Lakini Yesu alitambua watu hawa walikuwa wanajaribu kumtega. Akawaambia, 24“Nionesheni sarafu ya fedha,” Kisha akauliza, “Jina na picha katika sarafu hii ni ya nani?”
Wakamjibu, “Ya Kaisari.”
25Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari vilivyo vya Kaisari, na mpeni Mungu vilivyo vya Mungu.”
26Watu wale wakashangaa jibu lake la hekima. Hawakusema kitu. Hawakuweza kumtega Yesu pale mbele za watu. Hakusema chochote kibaya ambacho wangekitumia ili kumnasa.
Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu
(Mt 22:23-33; Mk 12:18-27)
27Baadhi ya Masadukayo walimwendea Yesu. (Masadukayo wanaamini watu hawatafufuka kutoka kwa wafu.) Wakamwuliza, 28“Mwalimu, Musa aliandika kwamba mtu aliyeoa akifa na hakuwa na watoto, kaka au mdogo wake amwoe mjane wake, ili wawe na watoto kwa ajili ya yule aliyekufa.#20:28 kwa ajili ya yule aliyekufa Tazama Kum 25:5-6. 29Walikuwepo ndugu saba. Wa kwanza alioa mke lakini akafa bila ya kuwa na watoto. 30Wa pili akamuoa yule mwanamke kisha akafa. 31Na wa tatu akamwoa mwanamke na akafa. Kitu kile kile kikawatokea ndugu wote saba. Walikufa bila ya kuwa na watoto. 32Mwanamke akawa wa mwisho kufa. 33Lakini ndugu wote saba walimwoa. Sasa, watu watakapofufuka kutoka kwa wafu, atakuwa mke wa yupi?”
34Yesu akawaambia Masadukayo, “Watu huoana katika ulimwengu huu. 35Baadhi ya watu watastahili kufufuliwa kutoka kwa wafu na kuishi tena katika ulimwengu ujao. Katika maisha yale hawataoa kamwe. 36Katika maisha hayo, watu watakuwa kama malaika na hawatakufa. Ni watoto wa Mungu, kwa sababu wamefufuliwa kutoka kwa wafu. 37Musa alionesha dhahiri kwamba watu hufufuliwa kutoka kwa wafu. Alipoandika kuhusu kichaka kilichokuwa kinaungua,#20:37 kichaka kilichokuwa kinaungua Tazama Kut 3:1-12. alisema kwamba Bwana ni ‘Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo.’#Kut 3:6 38Ni Mungu wa wanaoishi tu. Hivyo watu hawa kwa hakika hawakuwa wamekufa. Ndiyo, kwa Mungu watu wote bado wako hai.”
39Baadhi ya walimu wa sheria wakasema, “Mwalimu, jibu lako ni zuri.” 40Hakuna hata mmoja aliyekuwa na ujasiri wa kumwuliza swali jingine.
Je! Masihi ni Mwana wa Daudi?
(Mt 22:41-46; Mk 12:35-37)
41Kisha Yesu akasema, “Kwa nini watu husema kwamba Masihi ni Mwana wa Daudi? 42Katika kitabu cha Zaburi, Daudi mwenyewe anasema,
‘Bwana Mungu alimwambia Bwana wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kulia,
43na nitawaweka adui zako chini ya mamlaka yako.’#20:43 chini ya mamlaka yako Kwa maana ya kawaida, “mpaka nitakapowafanya maadui zako kuwa kiti cha kuweka miguu yako”. #Zab 110:1
44Hivyo ikiwa Daudi anamwita Masihi, ‘Bwana’. Inawezekanaje Masihi awe mwana wa Daudi?”
Tahadhali Juu ya Walimu wa Sheria
(Mt 23:1-36; Mk 12:38-40; Lk 11:37-54)
45Watu wote walipokuwa wanamsikiliza Yesu, akawaambia wafuasi wake, 46“Iweni waangalifu dhidi ya walimu wa sheria. Wanapenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi yanayoonekana ya heshima. Na wanapenda pale watu wanapowasalimu kwa heshima maeneo ya masoko. Wanapenda kukaa sehemu za heshima katika masinagogi na sehemu za watu maarufu katika sherehe. 47Lakini huwalaghai wajane na kuchukua nyumba zao. Kisha kujionesha kuwa waongofu wa mioyo kuomba sala ndefu. Mungu atawaadhibu kwa hukumu kuu.”
Currently Selected:
Luka 20: TKU
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International