Luka 21
21
Mjane Aonesha Jinsi Ulivyo Utoaji wa Kweli
(Mk 12:41-44)
1Yesu alitazama na kuwaona matajiri wakimtolea Mungu sadaka zao katika sanduku la sadaka ndani ya Hekalu. 2Kisha akamwona mjane maskini akiweka sarafu mbili za shaba kwenye sanduku. 3Akasema, “Mjane huyu maskini ametoa sarafu mbili tu. Lakini ukweli ni kuwa, ametoa zaidi ya hao matajiri wote. 4Wale wanavyo vingi, na wametoa vile ambavyo hawavihitaji. Lakini mwanamke huyu ni maskini sana, lakini ametoa vyote alivyokuwa akitegemea ili aishi.”
Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao
(Mt 24:1-14; Mk 13:1-13)
5Baadhi ya watu walikuwa wanazungumza kuhusu uzuri wa Hekalu lililojengwa kwa mawe safi na kupambwa kutokana na matoleo mbalimbali ambayo watu humtolea Mungu ili kutimiza nadhili zao.
6Lakini Yesu akasema, “Wakati utafika ambao yote mnayoyaona hapa yatateketezwa. Kila jiwe katika majengo haya litatupwa chini. Hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jingine.”
7Baadhi ya watu wakamwuliza Yesu, “Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Dalili ipi itatuonyesha kwamba ni wakati wa mambo haya kutokea?”
8Yesu akasema, “Iweni waangalifu, msije mkarubuniwa. Watu wengi watakuja wakitumia jina langu, watasema, ‘Mimi ndiye Masihi,’#21:8 Masihi Kwa maana ya kawaida, “Yule ambaye”, kwa maana ya Mfalme Mteule wa Mungu aliyetumwa na Mungu. Tazama Mt 24:5 na Masihi katika Orodha ya Maneno. na ‘Wakati sahihi umefika!’ Lakini msiwafuate. 9Mtakaposikia kuhusu vita na machafuko, msiogope. Mambo haya lazima yatokee kwanza. Lakini mwisho hautakuja haraka.”
10Kisha Yesu akawaambia, “Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. 11Kutakuwa matetemeko makubwa, kutakuwa njaa na magonjwa ya kutisha sehemu nyingi. Mambo ya kutisha yatatokea, na mambo ya kushangaza yatatokea kutoka mbinguni ili kuwaonya watu.
12Lakini kabla ya mambo haya yote kutokea, watu watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawahukumu katika masinagogi yao na kuwafunga gerezani. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na magavana. Watawatendea mambo haya yote kwa sababu ninyi ni wafuasi wangu. 13Lakini hili litawapa ninyi fursa ya kuhubiri juu yangu. 14Msihofu namna mtakavyojitetea, 15Nitawapa hekima kusema mambo ambayo adui zenu watashindwa kuyajibu. 16Hata wazazi wenu, ndugu zenu, jamaa, na rafiki watawageuka. Watawaua baadhi yenu. 17Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. 18Lakini hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyenu utakaopotea. 19Mtayaokoa maisha yenu ikiwa mtaendelea kuwa imara katika imani mnapopita katika mambo haya yote.
Kuharibiwa Kwa Mji wa Yerusalemu
(Mt 24:15-21; Mk 13:14-19)
20Mtakapoona majeshi yameuzunguka mji wa Yerusalemu, ndipo mtajua kuwa wakati wa kuharibiwa kwake umefika. 21Watu walioko katika Uyahudi wakati huo wakimbilie milimani. Mtu yeyote atakaye kuwa Yerusalemu wakati huo aondoke haraka. Ikiwa utakuwa karibu na mji, usiingie mjini! 22Manabii waliandika mambo mengi kuhusu wakati ambao Mungu atawaadhibu watu wake. Wakati ninaouzungumzia ni wakati ambao mambo haya yote lazima yatokee. 23Wakati huu utakuwa mgumu kwa wanawake wenye mimba au wanaonyonyesha watoto wadogo, kwa sababu mambo mabaya yatakuja katika nchi hii. Mungu atawaadhibu watu wake kwa sababu wamemkasirisha. 24Baadhi ya watu watauawa, wengine watafanywa watumwa na kuchukuliwa katika nchi mbalimbali. Mji mtakatifu wa Yerusalemu utatekwa na kuwekwa chini ya utawala wa wageni mpaka wakati ulioruhusiwa wao kufanya hivi utakapokwisha.
Yesu Atakaporudi Tena
(Mt 24:29-31; Mk 13:24-27)
25Mambo ya kushangaza yatatokea kwenye jua, mwezi na nyota na watu katika dunia yote wataogopa na kuchanganyikiwa kutokana na kelele za bahari na mawimbi yake. 26Watazimia kwa hofu na kuogopa watakapoona mambo yanayoupata ulimwengu. Kila kitu katika anga kitabadilishwa. 27Kisha watu watamwona Mwana wa Adamu akija katika wingu mwenye nguvu na utukufu mwingi. 28Mambo haya yakianza kutokea, simameni imara na msiogope. Jueni kuwa wakati wa Mungu kuwaweka huru umekaribia!”
Maneno Yangu Yataishi Milele
(Mt 24:32-35; Mk 13:28-31)
29Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Tazameni miti yote. Mtini ni mfano mzuri. 30Unapochipua majani mnatambua kwamba majira ya joto yamekaribia. 31Kwa namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yanatokea, mtajua kwamba ufalme wa Mungu umekaribia kuja.
32Ninawahakikishia kwamba, wakati mambo haya yote yatakapotokea, baadhi ya watu wanaoishi sasa watakuwa hai bado. 33Ulimwengu wote, dunia yote na anga vitapita, lakini maneno yangu yataishi milele.
Kuweni Tayari Wakati Wote
34Iweni waangalifu, msiutumie muda wenu katika sherehe za ulevi na kuhangaikia maisha haya. Mkifanya hivyo, hamtaweza kufikiri vyema na mwisho unaweza kuja mkiwa hamjajiandaa. 35Mwisho utakuja kwa kushitukiza kwa kila mtu duniani. 36Hivyo, iweni tayari kila wakati. Ombeni ili muepuke mambo haya yote yatakayotokea na mweze kusimama kwa ujasiri mbele za Mwana wa Adamu.”
37Wakati wa mchana Yesu aliwafundisha watu katika eneo la Hekalu. Usiku alitoka nje ya mji na kukaa usiku kucha kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. 38Kila asubuhi watu wote waliamka mapema kwenda kumsikiliza Yesu katika Hekalu.
Currently Selected:
Luka 21: TKU
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International