YouVersion Logo
Search Icon

Yeremia 10

10
Ibada za sanamu na ibada za kweli
1Sikilizeni neno analowaambieni Mwenyezi-Mungu,
enyi Waisraeli!
2Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Msijifunze mienendo ya mataifa mengine,
wala msishangazwe na ishara za mbinguni;
yaacheni mataifa mengine yashangazwe nazo.
3Maana, mila za dini za watu hawa ni za uongo.
Mtu hukata mti msituni
fundi akachonga kinyago cha mungu kwa shoka.
4Kisha watu hukipamba kwa fedha na dhahabu
wakakipigilia misumari kwa nyundo
ili kisije kikaanguka.
5Vinyago vyao ni kama vinyago vya kutishia ndege
katika shamba la matango,
havina uwezo wa kuongea;
ni lazima vibebwe
maana haviwezi kutembea.
Msiviogope vinyago hivyo,
maana haviwezi kudhuru,
wala haviwezi kutenda lolote jema.”
6Ee Mwenyezi-Mungu, hakuna aliye kama wewe;
wewe ni mkuu na nguvu yako yajulikana.
7Nani asiyekuogopa wewe, ee mfalme wa mataifa?
Wewe wastahili kuheshimiwa.
Miongoni mwa wenye hekima wote wa mataifa,
na katika falme zao zote,
hakuna hata mmoja aliye kama wewe.
8Wote ni wajinga na wapumbavu
mafunzo ya vinyago ni upuuzi mtupu!
9Vinyago hivyo hupambwa kwa fedha kutoka Tarshishi,
na dhahabu kutoka Ofiri;
kazi ya mafundi stadi na wafua dhahabu.
Zimevishwa nguo za samawati na zambarau,
zilizofumwa na wafumaji stadi.
10Lakini Mwenyezi-Mungu ni Mungu wa kweli;
Mungu aliye hai, mfalme wa milele.
Akikasirika, dunia hutetemeka,
mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.
11Basi, utawaambia hivi: “Miungu ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia. Itatoweka kabisa duniani na chini ya mbingu.”
Wimbo wa kumsifu Mungu
12Mwenyezi-Mungu aliiumba dunia kwa nguvu zake;
kwa hekima yake aliuimarisha ulimwengu,
kwa akili yake alizitandaza mbingu.
13Anapotoa sauti yake, maji hunguruma mbinguni,
huzusha ukungu kutoka mipaka ya dunia.
Huufanya umeme umulike wakati wa mvua,
na kuutoa upepo katika ghala zake.
14Binadamu ni mjinga na mpumbavu;
kila mfua dhahabu huaibishwa na vinyago vyake;
maana, vinyago hivyo ni uongo mtupu.
Havina uhai wowote ndani yao.
15Havina thamani, ni udanganyifu mtupu;
wakati vitakapoadhibiwa vyote vitaangamia.
16Lakini Mungu wa Yakobo si kama vinyago hivyo,
maana, yeye ndiye aliyeumba vitu vyote,
na Israeli ni taifa lililo mali yake;
Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndilo jina lake.
Uhamisho unakaribia
17Kusanyeni vitu vyenu enyi watu mliozingirwa.
18Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Wakati huo nitawatupa nje ya nchi hii,
nitawataabisha asibaki mtu yeyote.”
19Ole wangu mimi Yerusalemu maana nimejeruhiwa!
Jeraha langu ni baya sana!
Lakini nilisema: “Hakika haya ni mateso,
na sina budi kuyavumilia.”
20Lakini hema langu limebomolewa,
kamba zake zote zimekatika;
watoto wangu wameniacha, na kwenda zao,
wala hawapo tena;
hakuna wa kunisimikia tena hema langu,
wala wa kunitundikia mapazia yangu.
21Nami Yeremia nikasema:
Wachungaji wamekuwa wajinga,
hawakuomba shauri kwa Mwenyezi-Mungu;
kwa sababu hiyo, hawakufanikiwa,
na kondoo wao wote wametawanyika.
22Sikilizeni sauti! Habari zinatufikia.
Kuna kishindo kutoka kaskazini.
Taifa kutoka kaskazini linakuja,
kuifanya miji ya Yuda kuwa jangwa
ambamo kutakuwa na mapango ya mbweha!
23Najua, ee Mwenyezi-Mungu,
binadamu hana uwezo na maisha yake;
hakuna mtu awezaye kuyaongoza maisha yake.
24Utukosoe, ee Mwenyezi-Mungu, lakini si kwa ghadhabu,
wala kwa hasira yako, tusije tukaangamia.
25Imwage hasira yako juu ya mataifa yasiyokuabudu,
na juu ya watu ambao hawakutambui.
Maana, wamewaua wazawa wa Yakobo;
wamewaua na kuwaangamiza kabisa,
na nchi yao wameiacha magofu.

Currently Selected:

Yeremia 10: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in