Yeremia 9
9
1Laiti kichwa changu kingekuwa kisima cha maji,
na macho yangekuwa chemchemi ya machozi
ili nipate kulia mchana na usiku,
kwa ajili ya watu wangu waliouawa!
2Laiti ningekuwa na mahali pa kukaa jangwani,
ambamo ningewaacha watu wangu na kwenda zangu.”
Mwenyezi-Mungu asema:
“Wote ni watu wazinzi,
ni genge la watu wahaini.
3Hupinda maneno yao kama pinde;
wameimarika kwa uongo na si kwa haki.
Huendelea kutoka uovu hata uovu,
wala hawanitambui mimi.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
4Kila mmoja ajihadhari na jirani yake!
Hata ndugu yeyote haaminiki,
kila ndugu ni mdanganyifu,
na kila jirani ni msengenyaji.
5Kila mmoja humdanganya jirani yake,
hakuna hata mmoja asemaye ukweli.
Wamezifundisha ndimi zao kusema uongo;
hutenda uovu kiasi cha kushindwa kabisa kutubu.
6Wanarundika dhuluma juu ya dhuluma,
na udanganyifu juu ya udanganyifu.
Wanakataa kunitambua mimi.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
7Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema:
Tazama, nitawayeyusha na kuwajaribu!
Au, nifanye nini zaidi na watu wangu waovu?
8Ndimi zao ni kama mishale yenye sumu,
daima haziishi kudanganya;
kila mmoja huongea vema na jirani yake,
lakini moyoni mwake hupanga kumshambulia.
9Je, nisiwaadhibu kwa sababu ya mambo haya?
Je, nisilipe kisasi kwa taifa kama hili?
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Nyakati za kulia na kuomboleza
10Nitaililia na kuiomboleza milima;
nitayaombolezea malisho nyikani,
kwa sababu yamekauka kabisa,
hakuna mtu apitaye mahali hapo.
Hakusikiki tena sauti za ng'ombe;
ndege na wanyama wamekimbia na kutoweka.
11Mwenyezi-Mungu asema:
“Nitaifanya Yerusalemu magofu matupu,
naam, nitaifanya kuwa pango la mbweha;
na miji ya Yuda nitaifanya kuwa jangwa,
mahali pasipokaliwa na mtu yeyote.”
12Nami nikauliza, “Je kuna mtu mwenye hekima kiasi cha kuweza kueleza mambo haya? Mwenyezi-Mungu aliongea na nani hata huyo aweze kutangaza kitu hicho? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa tupu kama jangwa hata hakuna mtu apitaye humo?”
13Mwenyezi-Mungu akajibu: “Kwa kuwa wamekataa kushika sheria yangu niliyowapa, wamekataa kutii sauti yangu na kufuata matakwa yake. 14Badala yake wamefuata kwa ukaidi fikira za mioyo yao, wakaenda kuyaabudu Mabaali kama walivyofundishwa na wazee wao. 15Basi, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Tazama nitawalisha watu hawa uchungu na kuwapa maji yenye sumu wanywe. 16Nitawatawanya kati ya mataifa ambayo wao wenyewe wala wazee wao hawakupata kuyajua; nitawafanya waandamwe na vita mpaka hapo nitakapowaangamiza wote.”
Watu wa Yerusalemu walilia msaada
17Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:
“Fikirini na kuwaita wanawake waomboleze;
naam, waiteni wanawake hodari wa kuomboleza.
18Waambieni: ‘Njoni hima mkaomboleze juu yetu,
macho yetu yapate kuchuruzika machozi,
na kope zetu zibubujike machozi kama maji.’”
(Yeremia)
19Kilio kinasikika Siyoni:
“Tumeangamia kabisa!
Tumeaibishwa kabisa!
Lazima tuiache nchi yetu,
maana nyumba zetu zimebomolewa!
20Enyi wanawake, sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu!
Tegeni masikio msikie jambo analosema.
Wafundisheni binti zenu kuomboleza,
na jirani zenu wimbo wa maziko:
21‘Kifo kimepenya madirisha yetu,
kimeingia ndani ya majumba yetu;
kimewakatilia mbali watoto wetu barabarani,
vijana wetu katika viwanja vya mji.
22Maiti za watu zimetapakaa kila mahali
kama marundo ya mavi mashambani,
kama masuke yaliyoachwa na mvunaji,
wala hakuna atakayeyakusanya.’
Ndivyo alivyoniambia Mwenyezi-Mungu niseme.”
23Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Mwenye hekima asijivunie nguvu zake,
wala tajiri asijivunie utajiri wake.
24Anayetaka kujivuna na ajivunie jambo hili:
Kwamba ananifahamu
kwamba anajua Mwenyezi-Mungu hutenda mema,
hufanya mambo ya haki na uadilifu duniani.
Watu wa namna hiyo ndio wanipendezao.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
25Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo nitawaadhibu wote waliotahiriwa mwilini tu: 26Wamisri, Wayuda, Waedomu, Waamoni, Wamoabu na wakazi wote wa jangwani wanaonyoa denge.#9:26 wanaonyoa denge: Watu hao walinyoa denge kwa heshima ya mungu wao, desturi ambayo Waisraeli walikatazwa (taz Lawi 19:27). Maana watu hawa wote na Waisraeli wote hawakutahiriwa moyoni.”
Currently Selected:
Yeremia 9: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.