Yohana 8

8
1Usiku ule Yesu akaenda katika mlima wa Mizeituni. 2Mapema asubuhi akarudi katika eneo la Hekalu. Watu wengi wakaja kwake, naye akakaa pamoja nao na kuwafundisha.
3Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta kwake mwanamke waliyemfumania akizini. Wakamlazimisha asimame mbele ya watu. 4Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, mwanamke huyu amekamatwa akifanya zinaa. 5Sheria ya Musa inatuagiza kumponda kwa mawe mpaka afe mwanamke wa jinsi hiyo. Je! Unasema tufanye nini?”
6Watu hao waliyasema haya ili kumtega Yesu. Walitaka kumkamata akisema mambo tofauti ili wapate mashtaka ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama chini na kuanza kuandika kwenye udongo kwa kidole chake. 7Viongozi wa Kiyahudi waliendelea kumuuliza swali lao hilo. Naye akainuka na kusema, “Yeyote hapa ambaye hajawahi kutenda dhambi awe wa kwanza kumponda jiwe mwanamke huyu.” 8Kisha Yesu akainama chini tena na kuendelea kuandika katika udongo.
9Waliposikia hayo, wale watu walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine. Wanaume wazee wakitangulia kwanza, na kisha wengine wakifuata. Wakamwacha Yesu peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake. 10Kisha Yesu akainua uso wake tena na kumwambia, “Wameenda wapi hao wote? Je! hakuna aliyekuhukumu kuwa una hatia?” 11Mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja aliyenihukumu, Bwana.”#8:11 Nakala za kale na bora za Kiyunani hazina mistari 7:53–8:11. Nakala zingine zina sehemu hii katika maeneo mbalimbali kitabuni.
Kisha Yesu akasema, “Hata mimi sikuhukumu. Unaweza kwenda sasa, lakini usifanye dhambi tena.”
Yesu ni Nuru ya Ulimwengu
12Baadaye Yesu akazungumza tena na watu. Akasema, “Mimi ndiye nuru ya ulimwengu. Yeyote atakayenifuata mimi hataishi gizani kamwe. Atakuwa na nuru inayoleta uzima.”
13Lakini Mafarisayo wakamwambia Yesu, “Unapojishuhudia mwenyewe, unakuwa ni wewe peke yako unayethibitisha kuwa mambo haya ni kweli. Hivyo hatuwezi kuyaamini unayosema.”
14Yesu akajibu, “Ndiyo, nasema mambo haya juu yangu mwenyewe. Lakini watu wanaweza kuamini ninayosema, kwa sababu mimi najua nilikotoka. Pia najua ninakoenda. Lakini ninyi hamjui mimi ninakotoka wala ninakoenda. 15Mnanihukumu kama watu wanavyowahukumu wengine. Mimi simhukumu mtu yeyote. 16Lakini ikiwa ninahukumu, basi hukumu yangu ni ya kweli, kwa sababu ninapohukumu sifanyi hivyo peke yangu. Baba aliyenituma yuko pamoja nami. 17Sheria yenu inasema kwamba mashahidi wawili wakilisema jambo hilo hilo, basi mnapaswa kukubali wanayosema. 18Mimi shahidi ninayeshuhudia mambo yangu mwenyewe. Na Baba yangu aliyenituma ndiye shahidi wangu mwingine.”
19Watu wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?”
Yesu akajibu, “Hamnijui mimi wala Baba yangu hamumjui. Lakini mngenijua mimi, mngemjua Baba pia.”
20Yesu alisema maneno haya alipokuwa anafundisha katika eneo la Hekalu, karibu na chumba ambamo sadaka za Hekaluni zilitunzwa. Hata hivyo hakuna hata mmoja aliyemkamata, kwa sababu wakati sahihi wa kufanya hivyo ulikuwa bado haujafika.
Baadhi ya Wayahudi Hawamwelewi Yesu
21Kwa mara nyingine, Yesu akawaambia watu, “Mimi nitawaacha. Nanyi mtanitafuta, lakini pamoja na hayo mtakufa katika dhambi zenu. Kwani hamuwezi kuja kule niendako.”
22Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakaulizana wenyewe, “Je! atajiua mwenyewe? Je! ndiyo maana alisema, ‘Hamuwezi kuja kule niendako’?”
23Lakini Yesu akawaambia, “Ninyi watu ni wa hapa chini, lakini mimi ni wa kule juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu, lakini mimi si wa ulimwengu huu. 24Niliwaambia kwamba mnaweza kufa katika dhambi zenu. Ndiyo, kama hamtaamini kuwa MIMI NDIYE,#8:24 MIMI NDIYE Hili ni kama Jina la Mungu lililotumiwa katika Agano la Kale. Tazama Isa 41:4; 43:10; Kut 3:14. Hata hivyo, Inaweza kuwa na maana ya “Mimi Ndiye”, maana yake “Mimi Ndiye Masihi”. Pia katika mstari wa 28,58. mtakufa katika dhambi zenu.”
25Wakamwuliza, “Sasa wewe ni nani?”
Yesu akajibu, “Mimi ni yule niliyekwisha kuwaambia tangu mwanzo kuwa ni nani. 26Ninayo mengi zaidi ya kusema na ya kuwahukumu. Lakini nawaambia watu yale tu niliyosikia kutoka kwake aliyenituma, naye daima husema kweli.”
27Wale watu hawakuelewa alikuwa anazungumza habari za nani. Kwani Yeye alikuwa anawaambia habari za Baba. 28Naye akawaambia, “Mtamwinua juu#8:28 Mtamwinua juu Ina maana kugongomelewa msalabani na “kuinuliwa juu yake ili kufa”. Inaweza kuwa pia kuwa na maana ya pili: “Kuinuliwa juu”. Mwana wa Adamu. Ndipo mtakapojua kuwa MIMI NDIYE. Mtajua kuwa lo lote nilifanyalo silifanyi kwa mamlaka yangu. Mtajua kuwa nayasema tu yale Baba yangu aliyonifundisha. 29Yeye aliyenituma yuko pamoja nami. Siku zote nafanya yale yanayompendeza. Naye hajawahi kuniacha peke yangu.” 30Yesu alipokuwa akisema mambo haya, watu wengi wakamwamini.
Yesu Azungumzia Uhuru kutokana na Dhambi
31Hivyo Yesu akawaambia Wayahudi waliomwamini, “Kama mtaendelea kuyakubali na kuyatii mafundisho yangu, mtakuwa wafuasi wangu wa kweli. 32Mtaijua kweli, na kweli hiyo itawafanya muwe huru.”
33Wakamjibu, “Sisi ni wazaliwa wa Abrahamu. Na hatujawahi kamwe kuwa watumwa. Sasa kwa nini unasema kuwa tutapata uhuru?”
34Yesu akasema, “Ukweli ni huu, kila anayefanya dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35Mtumwa hakai na jamaa yake siku zote. Lakini mwana hukaa na jamaa yake siku zote. 36Hivyo kama Mwana atawapa uhuru, mtakuwa mmepata uhuru wa kweli. 37Najua kuwa ninyi ni wazaliwa wa Abrahamu. Lakini mmekusudia kuniua, kwa sababu hamtaki kuyakubali mafundisho yangu. 38Nawaambia yale ambayo Baba yangu amenionyesha. Lakini ninyi mnayafanya yale mliyoambiwa na baba yenu.”
39Wakasema, “Baba yetu ni Abrahamu.”
Yesu akasema, “Kama mngekuwa wazaliwa wa Abrahamu kweli, mngefanya yale aliyofanya Abrahamu. 40Mimi ni mtu niliyewaambia ukweli niliousikia kutoka kwa Mungu. Lakini Abrahamu hakufanya kama hayo mnayotaka kufanya. 41Mnafanya yale aliyofanya baba yenu.”
Lakini wakasema, “Sisi sio kama watoto ambao hawajawahi kumjua baba yao ni nani. Mungu ni Baba yetu. Ni baba pekee tuliye naye.”
42Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu kweli, mngenipenda. Nilitoka kwa Mungu, na sasa niko hapa. Sikujileta kwa mamlaka yangu mwenyewe. Mungu alinituma. 43Hamuyaelewi mambo ninayosema, kwa sababu hamuwezi kuyakubali mafundisho yangu. 44Baba yenu ni ibilisi. Ninyi ni wa kwake. Nanyi mnataka kufanya anayotaka. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo. Siku zote alikuwa kinyume na ukweli. Hakuna ukweli ndani yake. Yuko kama uongo anaousema. Ndiyo, ibilisi ni mwongo. Na ni baba wa uongo.
45Nawaambieni ukweli, na ndiyo maana hamniamini. 46Kuna mtu miongoni mwenu anayeweza kunishuhudia kuwa mimi nina hatia ya dhambi? Kama nawaeleza ukweli, kwa nini hamniamini? 47Yeyote aliye wa Mungu huyapokea anayosema. Lakini ninyi hamuyapokei anayosema Mungu, kwa sababu ninyi si wa Mungu.”
Yesu Azungumza Juu yake na Abrahamu
48Wayahudi wakajibu, “Sisi tunasema kuwa wewe ni Msamaria na pepo anakufanya uwe mwendawazimu! Je! hatuko sahihi kusema hivyo?”
49Yesu akajibu, “Sina pepo ndani yangu. Nampa heshima Baba yangu, lakini ninyi hamnipi heshima. 50Sijaribu kujitukuza mimi mwenyewe. Yupo mmoja anayetaka kunitukuza. Ndiye hakimu. 51Nawaahidi, yeyote anayeendelea kutii mafundisho yangu, hatakufa milele.”
52Wayahudi wakamwambia Yesu, “Sasa tunatambua kuwa una pepo ndani yako! Hata Abrahamu na manabii walikufa. Lakini unasema, ‘Yeyote anayetii mafundisho yangu, hatakufa kamwe.’ 53Wewe si mkuu zaidi ya baba yetu Abrahamu! Yeye alikufa na manabii nao walikufa. Unadhani wewe ni nani?”
54Yesu akajibu, “Kama ningejipa heshima mwenyewe, heshima hiyo isingelifaa kwa namna yoyote ile. Yule anayenipa mimi heshima ni Baba yangu. Ninyi mnasema kuwa ndiye Mungu wenu. 55Lakini kwa hakika hamumjui yeye. Mimi namjua. Kama ningesema simjui, basi ningekuwa mwongo kama ninyi. Lakini namjua, na kuyatii anayosema. 56Baba yenu Abrahamu alifurahi sana kwamba angeiona siku nilipokuja duniani. Hakika aliiona na akafurahi sana.”
57Wayahudi wakamwambia Yesu, “Ati nini? Wawezaje kusema ulimwona Abrahamu? Wewe bado hujafikisha hata umri wa miaka hamsini!”
58Yesu akajibu, “Ukweli ni kwamba, kabla Abrahamu hajazaliwa MIMI NIPO.” 59Aliposema haya, wakachukua mawe ili wamponde. Lakini Yesu akajificha, na kisha akaondoka katika eneo la Hekalu.

S'ha seleccionat:

Yohana 8: TKU

Subratllat

Comparteix

Copia

None

Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió