Yohana 9
9
Yesu Amponya Aliyezaliwa Pasipo Kuwa na Uwezo wa Kuona
1Yesu alipokuwa anatembea, alimwona mtu asiyeona tangu alipozaliwa. 2Wafuasi wake wakamwuliza, “Mwalimu, kwa nini mtu huyu alizaliwa asiyeona? Dhambi ya nani ilifanya hili litokee? Ilikuwa ni dhambi yake mwenyewe au ya wazazi wake?” 3Yesu akajibu, “Si dhambi yoyote ya huyo mtu wala ya wazazi wake iliyosababisha awe asiyeona. Alizaliwa asiyeona ili aweze kutumiwa kuonesha mambo makuu ambayo Mungu anaweza kufanya. 4Kukiwa bado ni mchana, tunapaswa kuendelea kuzifanya kazi zake Yeye aliyenituma. Usiku unakuja, na hakuna mtu atakayeweza kufanya kazi wakati wa usiku. 5Nikiwa bado nipo ulimwenguni, mimi ndiye nuru ya ulimwengu.”
6Yesu aliposema haya, akatema mate chini kwenye udongo, akatengeneza tope na kumpaka yule asiyeona katika macho yake. 7Yesu akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu” (Siloamu maana yake ni “Aliyetumwa”.) Hivyo mtu yule akaenda katika bwawa lile, akanawa na kurudi akiwa mwenye kuona.
8Majirani zake na wengine waliomwona akiomba omba wakasema, “Angalieni! Hivi huyu ndiye mtu yule aliyekaa siku zote na kuomba omba?”
9Wengine wakasema, “Ndiyo! Yeye ndiye.” Lakini wengine wakasema, “Hapana, hawezi kuwa yeye. Huyo anafanana naye tu.”
Kisha yule mtu akasema, “Mimi ndiye mtu huyo.”
10Wakamwuliza, “Kulitokea nini? Uliwezaje kupata kuona?”
11Akawajibu, “Mtu yule wanayemwita Yesu alitengeneza tope akayapaka macho yangu. Kisha akaniambia ‘Nenda kanawe kwenye bwawa la Siloamu.’ Hivyo nikaenda kule na kunawa, na ndipo nikaweza kuona.”
12Wakamwuliza, “Yuko wapi mtu huyo?”
Akajibu, “Mimi sijui aliko.”
Baadhi ya Mafarisayo Wana Maswali
13Kisha watu wakampeleka huyo mtu kwa Mafarisayo. 14Siku Yesu alipotengeneza yale matope na kuyaponya macho ya mtu huyo ilikuwa ni Sabato. 15Hivyo Mafarisayo wakamwuliza huyo mtu, “Uliwezaje kuona?”
Akawajibu, “Alipaka matope katika macho yangu. Nikaenda kunawa, na sasa naweza kuona.”
16Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyo mtu hatii sheria inayohusu siku ya Sabato. Kwa hiyo hatoki kwa Mungu.”
Wengine wakasema, “Lakini mtu aliye mtenda dhambi hawezi kufanya ishara kama hizi?” Hivyo hawakuelewana wao kwa wao. 17Wakamuuliza tena huyo mtu, “Kwa vile aliponya macho yako, unasemaje juu ya mtu huyo?”
Akajibu, “Yeye ni nabii.” 18Viongozi wa Kiyahudi walikuwa bado hawaamini kwamba haya yalimtokea mtu huyo; kwamba alikuwa haoni na sasa ameponywa. Lakini baadaye wakawaita wazazi wake. 19Wakawauliza, “Je! huyu ni mwana wenu? Mnasema alizaliwa akiwa haoni. Sasa amewezaje kuona?”
20Wazazi wake wakajibu, “Tunafahamu kwamba mtu huyu ni mwana wetu. Na tunajua kuwa alizaliwa akiwa asiyeona. 21Lakini hatujui kwa nini sasa anaweza kuona. Hatumjui aliyeyaponya macho yake. Muulizeni mwenyewe. Yeye ni mtu mzima anaweza kujibu mwenyewe.” 22Walisema hivi kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Kiyahudi. Viongozi walikwisha azimia kwamba, wangemwadhibu mtu yeyote ambaye angesema Yesu alikuwa Masihi. Wangewazuia hao wasije tena kwenye sinagogi. 23Ndiyo maana wazazi wake walisema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni yeye!”
24Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakamwita yule aliyekuwa haoni. Wakamwambia aingie ndani tena. Wakasema, “Unapaswa kumheshimu Mungu na kutuambia ukweli. Tunamjua mtu huyu kuwa ni mtenda dhambi.”
25Yule mtu akajibu, “Mimi sielewi kama yeye ni mtenda dhambi. Lakini nafahamu hili: Nilikuwa sioni, na sasa naweza kuona!”
26Wakawuuliza, “Alikufanyia nini? Aliyaponyaje macho yako?”
27Akajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia hayo. Lakini hamkutaka kunisikiliza. Kwa nini mnataka kusikia tena? Mnataka kuwa wafuasi wake pia?”
28Kwa hili wakampigia makelele na kumtukana wakisema, “Wewe ni mfuasi wake, siyo sisi! Sisi ni wafuasi wa Musa. 29Tunafahamu kwamba Mungu alisema na Musa. Lakini wala hatujui huyu mtu anatoka wapi!”
30Yule mtu akajibu, “Hili linashangaza kweli! Hamjui anakotoka, lakini aliyaponya macho yangu. 31Wote tunajua kuwa Mungu hawasikilizi watenda dhambi, bali atamsikiliza yeyote anayemwabudu na kumtii. 32Hii ni mara ya kwanza kuwahi kusikia kwamba mtu ameponya macho ya mtu aliyezaliwa asiyeona. 33Hivyo lazima anatoka kwa Mungu. Kama asingetoka kwa Mungu, asingefanya jambo lolote kama hili.”
34Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ulizaliwa ukiwa umejaa dhambi. Unataka kutufundisha sisi?” Kisha wakamwambia atoke ndani ya sinagogi na kukaa nje.
Kutoona Kiroho
35Yesu aliposikia kuwa walimlazimisha huyo mtu kuondoka, alikutana naye na kumuuliza, “Je! unamwamini Mwana wa Adamu?”
36Yule mtu akajibu, “Niambie ni nani huyo, bwana, ili nimwamini.” 37Yesu akamwambia, “Umekwisha kumwona tayari. Mwana wa Adamu ndiye anayesema nawe sasa.”
38Yule mtu akajibu, “Ndiyo, ninaamini, Bwana!” Kisha akainama na kumwabudu Yesu.
39Yesu akasema, “Nilikuja ulimwenguni ili ulimwengu uweze kuhukumiwa. Nilikuja ili wale wasiyeona waweze kuona. Kisha nilikuja ili wale wanaofikiri wanaona waweze kuwa wasiyeona.”
40Baadhi ya Mafarisayo walikuwa karibu na Yesu. Wakamsikia akisema haya. Wakamwuliza, “Nini? Unasema sisi pia ni wale wasiyeona?”
41Yesu akasema, “Kama mngekuwa wasiyeona hakika, msingekuwa na hatia ya dhambi. Lakini kwa kuwa mnasema mnaona, basi bado mngali na hatia.”
S'ha seleccionat:
Yohana 9: TKU
Subratllat
Comparteix
Copia
Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International