Mathayo 27
27
Yesu Apelekwa kwa Gavana Pilato
(Mk 15:1; Lk 23:1-2; Yh 18:28-32)
1Mapema asubuhi, viongozi wote wa makuhani na viongozi wazee walikutana na kuamua kumwua Yesu. 2Wakamfunga kamba, wakamwondoa na kwenda kumkabidhi kwa Pilato, gavana wa Kirumi.
Yuda Ajiua
(Mdo 1:18-19)
3Baada ya kumkabidhi Yesu, Yuda aliona kila kitu kilichotokea na kujua kuwa wameamua kumwua Yesu. Naye alihuzunika sana kutokana na kile alichokifanya. Hivyo alirudisha vile vipande thelathini vya sarafu vya fedha kwa wakuu wa makuhani na viongozi wazee. 4Yuda aliwaambia, “Nimetenda dhambi. Nimemsaliti kwenu mtu asiye na hatia ili auawe.”
Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Hilo halituhusu. Ni tatizo lako, siyo letu sisi.”
5Hivyo Yuda akavitupa vipande thelathini vya fedha Hekaluni, kisha akatoka akaenda kujinyonga.
6Viongozi wa makuhani wakaviokota vile vipande vya fedha Hekaluni. Wakasema, “Sheria yetu haituruhusu kuweka fedha hii katika hazina ya Hekalu, kwa sababu fedha hii imelipwa kwa ajili ya kifo, ni fedha yenye damu.” 7Hivyo wakaamua kutumia fedha hiyo kwa kununulia shamba linaloitwa Shamba la Mfinyanzi kwa ajili ya kuwazikia wageni wanapokufa wakiwa ziarani katika mji wa Yerusalemu. 8Ndiyo sababu eneo hilo bado linaitwa Shamba la Damu. 9Hili lilitimiza maneno ya nabii Yeremia aliposema:
“Walichukua sarafu thelathini za fedha. Hicho ni kiasi ambacho Waisraeli waliamua kulipa kwa ajili ya uhai wake. 10Walizitumia sarafu hizo thelathini za fedha kununulia shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniamuru.”#27:9-10 Walichukua … alivyoniamuru Tazama Zek 11:12-13; Yer 32:6-9.
Gavana Pilato Amhoji Yesu
(Mk 15:2-5; Lk 23:3-5; Yh 18:33-38)
11Yesu alisimama mbele ya Gavana, Pilato, ambaye alimwuliza Yesu, “Wewe ni mfalme wa Wayahudi?”
Yesu akajibu, “Waweza kusema hivyo.”
12Lakini viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi walipomshutumu, hakusema kitu.
13Hivyo Pilato akamwambia, “Husikii mashtaka haya yote wanayokushtaki wewe? Kwa nini hujibu?”
14Lakini Yesu hakujibu kitu, gavana alishangaa sana.
Pilato Ajaribu Kumwachia Huru Yesu
(Mk 15:6-15; Lk 23:13-25; Yh 18:39–19:16)
15Kila mwaka wakati wa Pasaka, gavana angemwachia huru mfungwa mmoja yeyote ambaye watu wangetaka aachiwe huru. 16Wakati huo alikuwepo mtu gerezani aliyejulikana kuwa ni mtu mbaya. Mtu huyu aliitwa Baraba.
17Kundi la watu lilipokusanyika, Pilato aliwaambia, “Nitamwacha huru mtu mmoja. Mnataka nani nimwache huru: Baraba au Yesu aitwaye Masihi?” 18Pilato alijua kuwa viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu walikuwa wanamwonea wivu.
19Pilato alipokuwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akamtumia ujumbe uliosema, “Usifanye jambo lolote juu ya huyo mtu. Hana hatia. Nimeota ndoto juu yake usiku, na ndoto hiyo imenihangaisha sana.”
20Lakini viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi waliwaambia watu waombe Baraba aachiwe huru na Yesu auawe.
21Pilato akasema, “Nina Baraba na Yesu. Je! mnataka nimwache huru yupi?”
Watu wakajibu, “Baraba!”
22Pilato akauliza, “Sasa nimfanye nini Yesu, aitwaye Masihi?”
Watu wote wakasema, “Mwue msalabani!”
23Pilato akauliza, “Kwa nini mnataka nimwue Yesu? Amefanya kosa gani?”
Lakini walipaza sauti wakisema, “Mwue msalabani!”
24Pilato akaona hakuna jambo ambalo angefanya ili kubadili nia yao. Kiukweli ilionekana wazi kuwa kungetokea fujo. Hivyo alichukua maji na kunawa mikono yake#27:24 kunawa mikono yake Pilato alifanya hivi kama ishara kuwa hakuwa amekubaliana na hakushiriki jambo ambalo watu waliamua kufanya. mbele yao wote. Akasema, “Sina hatia na kifo cha mtu huyu. Ninyi ndio mnaofanya hili!”
25Watu wakajibu, “Tutawajibika kwa kifo chake sisi wenyewe na hata watoto wetu!”
26Kisha Pilato akamwachia huru Baraba. Na akawaambia baadhi ya askari wamchape Yesu viboko. Kisha akamkabidhi Yesu kwa askari ili akauawe msalabani.
Askari wa Pilato Wamdhihaki Yesu
(Mk 15:16-20; Yh 19:2-3)
27Kisha askari wa Pilato wakamchukua Yesu mpaka kwenye nyumba ya gavana, kikosi kizima cha wale askari kikakusanyika pamoja kumzunguka Yesu. 28Wakamvua nguo zake na kumvalisha kivazi chekundu.#27:28 kivazi chekundu Pengine kilikuwa kivazi cha askari kilichoonekana kama mavazi ya zambarau yanayovaliwa na wafalme. Walimvalisha Yesu hiki kumdhihaki kwa kudai kuwa yeye ni mfalme. 29Kisha wakatengeneza taji kutokana na matawi ya miiba na kuiweka kwenye kichwa chake na wakaweka fimbo kwenye mkono wake wa kulia. Kisha kwa kumdhihaki, wakainama mbele zake. Wakasema, “Tunakusalimu, mfalme wa Wayahudi!” 30Walimtemea mate. Kisha wakachukua fimbo yake na kuanza kumpiga nayo kichwani. 31Baada ya kumaliza kumdhihaki, askari walimvua kivazi chekundu na kumvalisha nguo zake. Kisha wakamwongoza kwenda kuuawa msalabani.
Yesu Awambwa Msalabani
(Mk 15:21-32; Lk 23:26-43; Yh 19:17-19)
32Askari walipokuwa wanatoka mjini wakiwa na Yesu, walimwona mtu mmoja kutoka Kirene aliyeitwa Simoni, na wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. 33Walifika mahali palipoitwa Golgotha. (Yaani “Eneo la Fuvu la Kichwa”.) 34Askari walimpa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo.#27:34 nyongo Pengine ilitumika kama dawa ya kupunguza maumivu. Lakini alipoionja, alikataa kuinywa.
35Askari walimgongomea Yesu msalabani, kisha wakacheza kamari ili wagawane nguo za Yesu. 36Askari walikaa pale ili kumlinda. 37Wakaweka alama juu ya kichwa chake kuonesha mashtaka dhidi yake yaliyosema: Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.
38Wahalifu wawili waligongomewa kwenye misalaba pamoja na Yesu, mmoja aliwekwa upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto wa Yesu. 39Watu waliokuwa wakipita pale walitikisa vichwa vyao na kumtukana Yesu matusi 40kwa kusema, “Ulisema ungeweza kubomoa Hekalu na kulijenga tena katika siku tatu. Jiokoe mwenyewe! Teremka chini kutoka kwenye huo msalaba ikiwa kweli wewe ni Mwana wa Mungu!”
41Viongozi wa Makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikuwepo pale pia. Nao pia walimdhihaki Yesu kama watu wengine walivyofanya. 42Walisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa yeye mwenyewe! Watu husema kuwa yeye ni mfalme wa Israeli. Ikiwa yeye ni mfalme, ashuke kutoka msalabani. Ndipo tutamwamini. 43Alimtumaini Mungu. Hivyo Mungu amwokoe sasa, ikiwa hakika Mungu anamtaka. Yeye mwenyewe alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’” 44Hata wale wahalifu wawili waliokuwa misalabani upande wa kulia na wa kushoto wa Yesu walimtukana.
Yesu Afariki
(Mk 15:33-41; Lk 23:44-49; Yh 19:28-30)
45Ilipofika adhuhuri, giza liliifunika Israeli yote kwa muda wa masaa matatu. 46Yapata saa tisa alasiri Yesu alilia kwa sauti kuu akisema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” yaani “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha peke yangu?”#Zab 22:1
47Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hili wakasema, “Anamwita Eliya.”#27:47 Anamwita Eliya Neno hili “Mungu wangu” (ni Eli kwa Kiebrania ama Eloi kwa Kiaramu) ilisikika kwa watu kama jina la Eliya. Nabii maarufu aliyeishi mikaka kama 850 KK.
48Mtu mmoja alikimbia haraka akaenda kuchukua sponji, akaijaza siki, akaifunga kwenye fimbo na akanyoosha fimbo ili kumpa Yesu sponji ili anywe siki. 49Lakini wengine walisema, “Usimjali. Tunataka tuone ikiwa Eliya atakuja kumsaidia.”
50Yesu akalia kwa sauti kuu tena, kisha akafa.#27:50 akafa Kwa maana ya kawaida, “roho yake ikamwacha”.
51Yesu alipokufa, pazia la Hekalu lilipasuka vipande viwili. Mpasuko wake ulianzia juu mpaka chini. Kulitokea pia tetemeko la ardhi na miamba ilipasuka. 52Makaburi yalifunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa walifufuka kutoka kwa wafu. 53Walitoka makaburini. Na baada ya Yesu kufufuliwa kutoka kwa wafu, walikwenda kwenye mji mtakatifu wa Yerusalemu, na watu wengi waliwaona.
54Afisa wa jeshi na askari waliokuwa wanamlinda Yesu walitetemeka sana kwa kuogopa tetemeko la ardhi na kila walichokiona kikitokea. Wakasema, “Hakika alikuwa Mwana wa Mungu!”
55Wanawake wengi waliomfuata Yesu kutoka Galilaya kumhudumia walikuwepo pale wakiangalia wakiwa wamesimama mbali na msalaba. 56Miongoni mwao alikuwepo Mariamu Magdalena, Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu na pia mama yao Yakobo na Yohana#27:56 Yakobo na Yohana Kwa maana ya kawaida, “wana wa Zebedayo”. alikuwepo pale.
Yesu Azikwa
(Mk 15:42-47; Lk 23:50-56; Yh 19:38-42)
57Jioni ile, mtu mmoja tajiri aliyeitwa Yusufu alikuja Yerusalemu. Alikuwa mfuasi wa Yesu kutoka katika mji wa Arimathaya. 58Alikwenda kwa Pilato na akamwomba mwili wa Yesu. Pilato akawaamuru askari wampe Yusufu wa Arimathaya mwili wa Yesu. 59Aliuchukua mwili na kuuvingirisha katika kitambaa mororo cha kitani safi. 60Yusufu akauzika mwili wa Yesu katika kaburi mpya alilokuwa amelichonga kwenye mwamba mlimani. Kisha akalifunga kaburi kwa kuvingirisha jiwe kubwa kuziba mlango wa kaburi. Baada ya kufanya hivi, akaondoka. 61Mariamu Magdalena na mwanamke mwingine aliyeitwa Mariamu walikuwa wamekaa karibu na kaburi.
Kaburi la Yesu Lalindwa
62Siku ile ilikuwa Siku ya Maandalizi. Siku iliyofuata, viongozi wa makuhani na Mafarisayo walimwendea Pilato. 63Wakamwambia, “Mkuu, tunakumbuka kuwa yule mwongo alipokuwa hai alisema, ‘Nitafufuka kutoka kwa watu katika siku tatu.’ 64Hivyo amuru ili kaburi lilindwe kwa siku tatu. Wafuasi wake wanaweza kuja na kujaribu kuiba mwili. Kisha wataweza kumwambia kila mtu kuwa alifufuka kutoka kwa wafu. Uongo huo utakuwa hatari zaidi ya hata waliyosema juu yake alipokuwa hai.”
65Pilato akasema, “Chukueni baadhi ya askari, na mwende mkalinde kaburi kwa namna mnavyojua.” 66Kisha walikwenda kaburini na kuliweka salama dhidi ya wezi. Walifanya hivi kwa kuliziba kwa jiwe langoni na kuwaweka askari wa kulinda kaburi.
S'ha seleccionat:
Mathayo 27: TKU
Subratllat
Comparteix
Copia
Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International