Λογότυπο YouVersion
Εικονίδιο αναζήτησης

Luka 4

4
Isa ajaribiwa nyikani
(Mathayo 4:1-11; Marko 1:12-13)
1Isa, akiwa amejaa Roho Mtakatifu wa Mungu, akarudi kutoka Yordani. Akaongozwa na Roho wa Mungu hadi nyikani, 2ambako alijaribiwa na ibilisi kwa siku arobaini. Kwa siku zote hizo hakula chochote, hivyo baada ya muda huo akaona njaa.
3Ibilisi akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.”
4Isa akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’#4:4 Kumbukumbu 8:3
5Ibilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonesha milki zote za dunia kwa mara moja. 6Akamwambia, “Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa yeyote ninayetaka. 7Hivyo ukinisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako.”
8Isa akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’#4:8 Kumbukumbu 6:13
9Kisha ibilisi akampeleka hadi Yerusalemu, akamweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini kutoka hapa, 10kwa maana imeandikwa:
“ ‘Atakuagizia malaika wake
ili wakulinde kwa uangalifu;
11nao watakuchukua mikononi mwao,
usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’#4:11 Zaburi 91:11, 12
12Isa akamjibu, “Imenenwa: ‘Usimjaribu Mwenyezi Mungu, Mungu wako.’#4:12 Kumbukumbu 6:16
13Ibilisi alipomaliza kila jaribu, akamwacha Isa hadi wakati mwingine ufaao.
Huduma ya Isa huko Galilaya
(Luka 4:14–9:50)
Isa aanza kuhubiri
(Mathayo 4:12-17; Marko 1:14-15)
14Kisha Isa akarudi hadi Galilaya, akiwa amejaa nguvu za Roho wa Mungu, nazo habari zake zikaenea katika sehemu zote za nchi za kandokando. 15Akaanza kufundisha kwenye masinagogi#4:15 Nyumba za ibada na mafunzo. yao, na kila mmoja akamsifu.
Isa akataliwa Nasiri
(Mathayo 13:53-58; Marko 6:1-6)
16Isa akaenda Nasiri, alipolelewa, na siku ya Sabato alienda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome, 17naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa:
18“Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi yu juu yangu,
kwa sababu amenipaka mafuta
kuwahubiria maskini Habari Njema.
Amenituma kuwatangazia wafungwa
kufunguliwa kwao,
na vipofu kupata kuona tena,
kuwaweka huru wanaoteswa,
19na kutangaza mwaka wa Mwenyezi Mungu uliokubalika.”#4:19 Isaya 61:1, 2
20Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. 21Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.”
22Watu wote walimsifu na kuyastaajabia maneno yake yaliyojaa neema, wakaulizana, “Je, huyu si mwana wa Yusufu#4:22 Yusufu hakuwa baba mzazi wa Isa, bali alikuwa baba mlezi.?”
23Isa akawaambia, “Bila shaka mtatumia mithali hii: ‘Tabibu, jiponye mwenyewe! Mambo yale tuliyosikia kwamba uliyafanya huko Kapernaumu, yafanye na hapa kwenye mji wako.’ ”
24Isa akasema, “Amin, nawaambia, hakuna nabii anayekubalika katika mji wake mwenyewe. 25Lakini ukweli ni kwamba palikuwa na wajane wengi katika Israeli wakati wa Ilya, mbingu zilipofungwa kwa miaka mitatu na miezi sita pakawa na njaa kuu katika nchi nzima. 26Hata hivyo Ilya hakutumwa hata kwa mmoja wao, bali kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. 27Pia palikuwa na wengi wenye ukoma katika Israeli katika siku za nabii Al-Yasa, lakini hakuna hata mmoja wao aliyetakaswa, isipokuwa Naamani mtu wa Shamu#4:27 yaani Siria.”
28Watu wote katika sinagogi waliposikia maneno haya, wakakasirika sana. 29Wakasimama, wakamtoa nje ya mji, wakamchukua hadi kwenye kilele cha mlima ambao mji huo ulikuwa umejengwa juu yake, ili wamtupe chini kutoka mteremko mkali. 30Lakini yeye akapita papo hapo katikati ya umati huo wa watu akaenda zake.
Isa atoa pepo mchafu
(Marko 1:21-28)
31Kisha Isa akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilaya, na katika siku ya Sabato akawa anafundisha. 32Wakashangazwa sana na mafundisho yake, maana maneno yake yalikuwa na mamlaka.
33Ndani ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu. Naye akapaza sauti kwa nguvu akisema, 34“Tuache! Tuna nini nawe, Isa Al-Nasiri? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”
35Basi Isa akamkemea yule pepo mchafu, akamwamuru, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Yule pepo mchafu akamwangusha yule mtu chini mbele yao wote, akatoka pasipo kumdhuru.
36Watu wote wakashangaa, wakaambiana, “Mafundisho haya ni ya namna gani? Anawaamuru pepo wachafu kwa mamlaka na nguvu, nao wanatoka!” 37Habari zake zikaanza kuenea kila mahali katika sehemu ile.
Isa amponya mama mkwe wa Simoni na pia watu wengi
(Mathayo 8:14-17; Marko 1:29-34)
38Isa akatoka katika sinagogi, akaenda nyumbani mwa Simoni. Basi huko alimkuta mama mkwe wa Simoni akiwa ameshikwa na homa kali, nao wakamwomba Isa amsaidie. 39Hivyo Isa akamwinamia na kukemea ile homa, nayo ikamwacha. Akaamka mara moja, naye akaanza kuwahudumia.
40Jua lilipokuwa linatua, watu wakamletea Isa watu wote waliokuwa na maradhi mbalimbali, naye akaweka mikono yake juu ya kila mgonjwa, naye akawaponya. 41Pepo wachafu pia wakawatoka watu wengi, nao walipokuwa wakitoka wakapiga kelele, wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Isa akawakemea na kuwazuia wasiseme, kwa maana walimjua kuwa yeye ndiye Al-Masihi.#4:41 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.
42Kesho yake, kulipopambazuka, Isa alienda mahali pa faragha. Watu wengi wakawa wanamtafuta kila mahali, nao walipomwona wakajaribu kumzuia asiondoke. 43Lakini yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri Habari Njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.” 44Naye aliendelea kuhubiri katika masinagogi ya Yudea.

Επιλέχθηκαν προς το παρόν:

Luka 4: NENO

Επισημάνσεις

Κοινοποίηση

Αντιγραφή

None

Θέλετε να αποθηκεύονται οι επισημάνσεις σας σε όλες τις συσκευές σας; Εγγραφείτε ή συνδεθείτε