YouVersion logo
Ikona pretraživanja

Luka 7

7
Yesu Amponya Mtumishi wa Afisa wa Jeshi
(Mt 8:5-13; Yh 4:43-54)
1Yesu alipomaliza kuwaambia watu mambo yote aliyotaka kuwaambia, alikwenda mjini Kapernaumu. 2Afisa wa jeshi katika mji wa Kapernaumu alikuwa na mtumishi aliyekuwa wa muhimu sana kwake. Mtumishi huyu alikuwa mgonjwa sana karibu ya kufa. 3Afisa huyu aliposikia kuhusu Yesu, aliwatuma baadhi ya viongozi wa wazee wa Kiyahudi kwa Yesu. Aliwataka wamwombe Yesu aende kumponya mtumishi wake. 4Wazee walikwenda kwa Yesu, wakamsihi amsaidie afisa. Walisema, “Mtu huyu anastahili msaada wako, 5Kwa sababu anawapenda watu wetu na ametujengea sinagogi.”
6Hivyo Yesu alikwenda nao. Alipoikaribia nyumba ya yule afisa, afisa aliwatuma rafiki zake kumwambia Yesu, “Bwana, huhitaji kufanya kitu chochote maalumu kwa ajili yangu. Sistahili wewe uingie nyumbani mwangu. 7Ndiyo maana sikuja mimi mwenyewe kwako. Unahitaji kutoa amri tu na mtumishi wangu atapona. 8Ninajua hii, kwa kuwa ninaelewa mamlaka. Kuna watu wenye mamlaka juu yangu, na nina askari walio chini ya mamlaka yangu. Nikimwambia askari mmoja ‘nenda’, huenda. Na nikimwambia mwingine ‘njoo’, huja. Pia nikimwambia mtumwa wangu ‘fanya hiki’, hunitii.”
9Yesu aliposikia hayo alishangaa, akawageukia watu waliokuwa wanamfuata, akawaambia, “Ninawaambia, Sijawahi kuona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.”
10Kundi lililotumwa kwa Yesu waliporudi nyumbani, walimkuta yule mtumishi amepona.
Yesu Amfufua Kijana wa Mama Mjane
11Siku iliyofuata Yesu na wafuasi wake walikwenda katika mji wa Naini. Kundi kubwa la watu walisafiri pamoja nao. 12Yesu alipolikaribia lango la mji, aliona watu wamebeba maiti. Alikuwa ni mwana pekee wa mama mjane. Watu wengi kutoka mjini walifuatana na yule mama mjane. 13Bwana alipomwona yule mama, alimwonea huruma na kumwambia, “Usilie.” 14Akakaribia, akaligusa jeneza. Wanaume waliokuwa wamebeba jeneza wakasimama. Ndipo Yesu akamwambia kijana aliyekufa, “Kijana, nakuambia, inuka!” 15Yule kijana, akaketi, akaanza kuongea. Yesu akamrudisha kwa mama yake.
16Kila mtu aliingiwa hofu. Wakaanza kumsifu Mungu na kusema, “Nabii mkuu yuko hapa pamoja nasi!” na “Mungu amekuja kuwasaidia watu wake!”
17Habari hii kuhusu Yesu ikaenea katika Uyahudi yote, na kila sehemu kuzunguka pale.
Yohana Atuma Watu Kumwuliza Yesu Swali
(Mt 11:2-19)
18Wafuasi wa Yohana Mbatizaji walimweleza Yohana Mbatizaji kuhusu mambo haya yote. Naye aliwaita wanafunzi wake wawili. 19Akawatuma waende na kumwuliza Yesu, “Wewe ndiye tuliyesikia anakuja, au tumsubiri mwingine?”
20Wafuasi wa Yohana walipofika kwa Yesu, wakasema, “Yohana Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: ‘Wewe ndiye yule anayekuja, au tumsubiri mwingine?’”
21Wakati ule ule Yesu alikuwa amewaponya watu wengi madhaifu na magonjwa yao. Aliwaponya waliokuwa na pepo wabaya na kuwafanya wasiyeona wengi kuona. 22Kisha aliwaambia wanafunzi wa Yohana, “Nendeni mkamweleze Yohana yale mliyoyaona na kuyasikia: wasiyeona wanaona, walemavu wa miguu wanatembea, wenye magonjwa mabaya ya ngozi wanatakasika, wasiyesikia wanasikia. Waliokufa wanafufuliwa na Habari Njema inahubiriwa kwa maskini. 23Heri wale wasio na mashaka kunikubali mimi.”#7:23 Heri … kunikubali mimi Au “Baraka kuu ni kwa wale wasio na mashaka kunikubali.”
24Baada ya wanafunzi wa Yohana kuondoka, Yesu akaanza kuwaambia watu kuhusu Yohana, “Mlitoka kwenda jangwani kuona nini? Mtu aliyekuwa dhaifu, kama unyasi unaotikiswa na upepo? 25Mlitegemea kuona nini? Mtu aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hilo. Watu wanaovaa mavazi mazuri na kuishi kwa anasa wako katika majumba ya wafalme. 26Sasa, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yohana ni zaidi ya nabii. 27Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana:
‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’#Mal 3:1
28Ninawaambia, hakuna aliyewahi kuzaliwa aliye mkuu kuliko Yohana. Lakini mwenye umuhimu mdogo, katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana.”
29(Watu waliposikia hili, wote walikubali kuwa mafundisho ya Mungu yalikuwa mazuri. Hata watoza ushuru waliobatizwa na Yohana walikiri. 30Lakini Mafarisayo na wanasheria walikataa kuukubali mpango wa Mungu kwa ajili yao; hawakumruhusu Yohana awabatize.)
31“Niseme nini kuhusu watu wa wakati huu? Niwafananishe na nini? Wanafanana na nini? 32Ni kama watoto waliokaa sokoni. Kundi moja la watoto likawaita watoto wengine na kusema,
‘Tuliwapigia filimbi
lakini hamkucheza.
Tuliwaimba wimbo wa huzuni,
lakini hamkulia.’
33Yohana Mbatizaji alikuja na hakula chakula cha kawaida au kunywa divai. Nanyi mkasema, ‘Ana pepo ndani yake.’ 34Mwana wa Adamu amekuja anakula na kunywa. Mnasema, ‘Mwangalieni anakula sana na kunywa sana divai. Ni rafiki wa watoza ushuru na watenda dhambi wengine.’ 35Lakini hekima huoneshwa kuwa sahihi kwa wale wanaoikubali.”
Yesu na Mwanamke Mwenye Dhambi
36Mmoja wa Mafarisayo alimwalika Yesu kula chakula nyumbani mwake. Yesu akaenda nyumbani kwa yule Farisayo, akaketi#7:36 akaketi Waliketi kwa kujilaza kidogo kuelekea katika meza ya chakula katika mzunguko, miguu yao ikiwa imenyooka kwa nyuma. katika nafasi yake sehemu ya kulia chakula.
37Alikuwepo mwanamke mmoja katika mjini ule aliyekuwa na dhambi nyingi. Alipojua kuwa Yesu alikuwa anakula chakula nyumbani kwa Farisayo, alichukua chupa kubwa yenye manukato ya thamani sana. 38Alisimama karibu na miguu ya Yesu akilia. Kisha alianza kuisafisha miguu ya Yesu kwa machozi yake na akaifuta kwa nywele zake, akaibusu mara nyingi na kuipaka manukato.
39Farisayo aliyemwalika Yesu alipoona hili, alijisemea moyoni mwake, “Mtu huyu angekuwa nabii, angetambua kuwa mwanamke huyu anayemgusa ni mwenye dhambi.”
40Katika kujibu kile Farisayo alichokuwa akifikiri, Yesu akasema, “Simoni nina kitu cha kukwambia.”
Simoni akajibu, “Nieleze, Mwalimu.”
41Yesu akasema, “Kulikuwa watu wawili. Wote wawili walikuwa wanadaiwa na mkopeshaji mmoja. Mmoja alidaiwa sarafu mia tano za fedha, na wa pili sarafu hamsini za fedha. 42Watu wale hawakuwa na fedha, hivyo hawakuweza kulipa madeni yao. Lakini mkopeshaji aliwasamehe wote wawili. Kati ya wote wawili ni yupi atakayempenda mkopeshaji zaidi?”
43Simoni akajibu, “Nafikiri ni yule aliyekuwa anadaiwa fedha nyingi.”
Yesu akamwambia, “Umejibu sawa.” 44Kisha akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, “Unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako hukunipa maji ili ninawe miguu yangu. Lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kuikausha kwa nywele zake. 45Wewe hukunisalimu kwa busu, lakini amekuwa akinibusu miguu yangu tangu nilipoingia. 46Hukuniheshimu kwa mafuta kwa ajili ya kichwa changu, lakini yeye amenipaka miguu yangu manukato yanayonukia vizuri. 47Ninakwambia kuwa dhambi zake zilizo nyingi zimesamehewa. Hii ni wazi, kwa sababu ameonesha upendo mkubwa. Watu wanaosamehewa kidogo hupenda kidogo.”
48Kisha akamwambia mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.”
49Watu waliokaa naye sehemu ya chakula wakaanza kusema mioyoni mwao, “Mtu huyu anadhani yeye ni nani? Anawezaje kusamehe dhambi?”
50Yesu akamwambia mwanamke, “Kwa sababu uliamini, umeokolewa kutoka katika dhambi zako. Nenda kwa amani.”

Trenutno odabrano:

Luka 7: TKU

Istaknuto

Podijeli

Kopiraj

None

Želiš li svoje istaknute stihove spremiti na sve svoje uređaje? Prijavi se ili registriraj