Luka 23
23
Isa Apelekwa Kwa Pilato
(Mathayo 27:1-14; Marko 15:1-5; Yohana 18:28-38)
1 Kisha umati wote wa watu ukainuka na kumpeleka Isa kwa Pilato. 2 Nao wakaanza kumshtaki wakisema: “Tumemwona huyu mtu akipotosha taifa letu, akiwazuia watu wasilipe kodi kwa Kaisari na kujiita kuwa yeye ni Al-Masihi, mfalme.”
3 Basi Pilato akamuuliza Isa, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”
Isa akajibu, “Wewe wasema.”
4 Pilato akawaambia viongozi wa makuhani na watu wote waliokuwepo, “Sioni sababu ya kutosha kumshtaki mtu huyu!”
5 Lakini wao wakakazana kusema, “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika Uyahudi yote, tangu Galilaya alikoanzia, hadi sehemu hii!”
Isa Apelekwa Kwa Herode
6 Pilato aliposikia hayo akauliza, “Huyu mtu ni Mgalilaya?” 7 Alipofahamu kwamba Isa alikuwa chini ya mamlaka ya Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa pia Yerusalemu.
8 Herode alipomwona Isa alifurahi sana, kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amesikia mambo mengi kumhusu yeye. Pia alitarajia kumwona akifanya miujiza kadha wa kadha. 9 Herode akamuuliza maswali mengi, lakini Isa hakumjibu lolote. 10Wakati huo viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walikuwepo wakitoa mashtaka yao kwa nguvu sana. 11 Herode na askari wake wakamdhihaki Isa na kumfanyia mzaha. Wakamvika vazi zuri sana, wakamrudisha kwa Pilato. 12 Siku hiyo, Herode na Pilato wakawa marafiki; kabla ya jambo hili walikuwa na uadui kati yao.
Isa Ahukumiwa Kifo
(Mathayo 27:15-26; Marko 15:6-15; Yohana 18:39–19:16)
13 Basi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu, 14 akawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami nimeona hakuna msingi wowote wa mashtaka yenu dhidi yake. 15Wala Herode hakumwona na kosa lolote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lolote linalostahili kifo. 16 Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachia.” [ 17 Kwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu.]
18 Ndipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyo! Tufungulie Baraba!” 19(Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini, na kwa ajili ya uuaji).
20Pilato, akitaka kumwachia Isa, akasema nao tena. 21Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”
22 Kwa mara ya tatu, Pilato akawauliza, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yoyote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi, na kisha nitamwachia.”
23Lakini watu wakazidi kupiga kelele kwa nguvu zaidi, wakidai kwamba Isa asulubiwe. Hivyo, kelele zao zikashinda. 24 Kwa hiyo Pilato akatoa hukumu kwamba madai yao yatimizwe. 25Akamfungua yule mtu aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kuhusika katika uasi dhidi ya serikali na mauaji. Akamkabidhi Isa mikononi mwao, wamfanyie watakavyo.
Kusulubiwa Kwa Isa
(Mathayo 27:32-44; Marko 15:21-32; Yohana 19:17-27)
26 Walipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni mwenyeji wa Kirene, aliyekuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Isa. 27 Idadi kubwa ya watu wakamfuata Isa, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea. 28 Isa akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. 29 Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao matumbo yao hayakuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’ 30 Ndipo
“ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni!”
na vilima, “Tufunikeni!” ’
31 Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?”
32 Watu wengine wawili wahalifu, walipelekwa pamoja na Isa ili wakasulubiwe. 33Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulubisha Isa pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto. 34 Isa akasema, “Baba,#23:34 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.
35 Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Al-Masihi wa Mungu, Mteule wake.”
36 Askari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe, 37 na wakamwambia, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”
38 Kwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: huyu ndiye mfalme wa wayahudi.
Maandishi haya yalikuwa yameandikwa kwa lugha za Kiyunani, Kilatini na Kiebrania.
39 Mmoja wa wale wahalifu waliosulubiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Al-Masihi? Jiokoe mwenyewe na utuokoe na sisi.”
40Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu iyo hiyo? 41 Sisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lolote.”
42 Kisha akasema, “Isa, unikumbuke utakapokuja katika Ufalme wako.”
43 Isa akamjibu, “Amin, nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”#23:43 Paradiso maana yake bustani nzuri, hapa ina maana mahali zinapokwenda roho za wacha Mungu, yaani watakatifu.
Kifo Cha Isa
(Mathayo 27:45-56; Marko 15:33-41; Yohana 19:28-30)
44 Ilikuwa kama saa sita mchana, nalo giza likafunika nchi yote hadi saa tisa, 45 kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili. 46 Isa akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho.
47 Yule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu, akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.” 48 Watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao. 49 Lakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya.
Maziko Ya Isa
(Mathayo 27:57-61; Marko 15:42-47; Yohana 19:38-42)
50 Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki, jina lake Yusufu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wayahudi,#23:50 Baraza la Wayahudi hapa ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa ndilo baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi, lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. 51 lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa mwenyeji wa Arimathaya huko Uyahudi, naye alikuwa anaungojea Ufalme wa Mwenyezi Mungu kwa matarajio makubwa. 52Yusufu alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Isa. 53Akaushusha kutoka msalabani, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limezikiwa mtu mwingine bado. 54 Ilikuwa Siku ya Maandalizi, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza.
55 Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Isa wakimfuata kutoka Galilaya wakamfuata Yusufu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Isa ulivyolazwa. 56 Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.
Trenutno odabrano:
Luka 23: NMM
Istaknuto
Podijeli
Kopiraj
Želiš li svoje istaknute stihove spremiti na sve svoje uređaje? Prijavi se ili registriraj
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018 by Biblica, Inc.
Used with permission.
All rights reserved worldwide.