Mwanzo 13

13
Abramu na Loti wanatengana
1Abramu akarudi kutoka Misri, akaingia upande wa Negebu. Alikuwa na mkewe na mali yake yote pamoja na Loti. 2Wakati huo, Abramu alikuwa ametajirika sana. Alikuwa na mifugo, fedha na dhahabu. 3Akaendelea kusafiri toka eneo la Negebu hadi Betheli. Alifika mahali alipokuwa amepiga kambi ya hema hapo awali, kati ya Betheli na Ai, 4ambapo alikuwa amejenga madhabahu. Hapo Abramu akamwomba Mwenyezi-Mungu kwa jina lake. 5Kadhalika, Loti, ambaye alifuatana na Abramu, alikuwa na kondoo, mifugo na hema. 6Idadi ya mifugo yao ilikuwa kubwa mno hata nchi ile haikuweza kuwatosha Abramu na Loti kuishi pamoja. 7Basi, kukazuka ugomvi kati ya wachungaji wa Abramu na wachungaji wa Loti. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo.
8Basi, Abramu akamwambia Loti, “Kusiwe na mafarakano kati yetu wala kati ya wachungaji wako na wachungaji wangu, kwa sababu sisi ni jamaa moja. 9Tazama nchi hii yote mbele yako. Na tutengane. Ukienda kushoto, mimi nitakwenda kulia; ukienda kulia, mimi nitakwenda kushoto.”
10Loti akatazama, akaliona bonde la mto Yordani, akaona kuwa lina maji ya kutosha kila mahali, kama bustani ya Mwenyezi-Mungu#13:10 Bustani ya Mwenyezi-Mungu: Au: “Bustani kubwa sana”. Wazo la uzuri wa eneo hilo pia limo katika matumizi ya maneno hayo. Baadhi wanafikiri inawezekana wazo hilo limeunganishwa na maneno “bustani ya Edeni” (Mwa 2:8-14). Mji wa “Soari” ulikuwa pia katika eneo hilo. na kama nchi ya Misri upande wa Soari. (Hii ilikuwa kabla Mwenyezi-Mungu hajaiangamiza miji ya Sodoma na Gomora).#13:10 Sodoma na Gomora: Vijiji au miji ambayo labda ilikuwa kusini ya Bvahari ya Chumvi na ambayo kuteketezwa kwake kunasimuliwa katika Mwa 18-19. 11Kwa hiyo, Loti akajichagulia bonde lote la mto Yordani,#13:11 Bonde … la Mto Yordani: Hili ni bonde linaloenea pande zote mbili za Mto Yordani mpaka mto huo unapoingia Bahari ya Chumvi. akaelekea mashariki, na hivyo wakatengana. 12Abramu akabaki nchini Kanaani na Loti akakaa kati ya miji iliyokuwa bondeni, akahamishia kambi yake Sodoma. 13Watu wa Sodoma walikuwa waovu na watenda dhambi wakuu dhidi ya Mwenyezi-Mungu.
Abramu anaoneshwa nchi
14Baada ya Loti kujitenga na Abramu, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Angalia toka hapo ulipo utazame pande zote: kaskazini, kusini, mashariki na magharibi. 15Nchi hii yote unayoiona nitakupa wewe na wazawa wako iwe yenu milele. 16Wazawa wako nitawafanya wawe wengi wasiohesabika, kama vile mavumbi ya nchi yasivyoweza kuhesabika! 17Basi, inuka uitembelee nchi hii katika mapana na marefu, kwani nitakupa wewe.”#13:14-17 Rejea Mate 7:5; Gal 3:16. Hapa inarudiwa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Abrahamu. Taz Mwa 12:2 maelezo. 18Kwa hiyo, Abramu akang'oa hema, akaenda kukaa karibu na mialoni ya Mamre#13:18 Mamre: Mahali yapata kilomita 3 kaskazini ya Hebroni ambapo yamkini palikuwa mahali pa ibada. Mahali hapo panahusika sana katika habari za Abrahamu. kule Hebroni;#13:18 Hebroni: Mji ulioko katika eneo la milima ya Yudea, yapata kilomita 30 kusini mwa Yerusalemu. Huu ni mji wa zamani kuliko miji mingine katika Palestina (rejea Hes 13:22). Waarabu waliuita “El Jalil” maana yake “Rafiki” kwa heshima ya Abrahamu, rafiki wa Mungu (2Nya 20:7; Isa 41:8; Yak 2:23). huko akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu.

Одоогоор Сонгогдсон:

Mwanzo 13: BHNTLK

Тодруулга

Хуваалцах

Хувилах

None

Тодруулсан зүйлсээ бүх төхөөрөмждөө хадгалмаар байна уу? Бүртгүүлэх эсвэл нэвтэрнэ үү