Yohana 6

6
Isa Alisha Wanaume 5,000
(Mathayo 14:13-21; Marko 6:30-44; Luka 9:10-17)
1 Baada ya haya, Isa alikwenda ng’ambo ya Bahari ya Galilaya, ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia. 2 Umati mkubwa wa watu uliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa. 3 Kisha Isa akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. 4 Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
5 Isa alipotazama na kuuona ule umati mkubwa wa watu ukimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” 6Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya.
7 Filipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili,#6:7 Dinari 200 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 200; mshahara wa kibarua ulikuwa dinari moja kwa siku. hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa ili kila mtu apate kidogo.”
8 Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia, 9 “Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa umati huu wote?”
10Isa akasema, “Waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi. Palikuwa na wanaume wapatao 5,000. 11 Ndipo Isa akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wameketi. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka.
12Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee chochote.” 13Hivyo wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vya ile mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili wadogo vilivyobakishwa na waliokula.
14 Baada ya watu kuona muujiza ule Isa aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!” 15 Isa akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake.
Isa Atembea Juu Ya Maji
(Mathayo 14:22-33; Marko 6:45-52)
16 Ilipofika jioni, wanafunzi wake waliteremka kwenda baharini. 17Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Isa alikuwa hajajumuika nao. 18Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. 19 Wanafunzi walipokuwa wamekwenda mwendo wa karibu maili tatu au nne,#6:19 Maili tatu au nne ni kama kilomita 5 au 6. walimwona Isa akitembea juu ya maji akikaribia mashua, nao wakaogopa sana. 20 Lakini Isa akawaambia, “Ni mimi. Msiogope.” 21Ndipo wakamkaribisha kwa furaha ndani ya mashua, na mara wakafika ufuoni walikokuwa wakienda.
Watu Wanamtafuta Isa
22 Siku iliyofuata, wale watu waliokuwa wamebaki ng’ambo waliona kwamba palikuwepo na mashua moja tu na kwamba Isa hakuwa ameondoka pamoja na wanafunzi wake, ila walikuwa wameondoka peke yao. 23 Lakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia zikafika karibu na mahali pale walipokula mikate baada ya Bwana Isa kumshukuru Mwenyezi Mungu. 24Mara wale watu wakatambua kwamba Isa hakuwepo hapo, wala wanafunzi wake. Wakaingia kwenye mashua hizo, wakaenda Kapernaumu ili kumtafuta Isa.
Isa Ni Mkate Wa Uzima
25 Walipomkuta Isa ng’ambo ya bahari wakamuuliza, “Mwalimu, umefika lini huku?”
26 Isa akawajibu, “Amin, amin nawaambia, ninyi hamnitafuti kwa kuwa mliona ishara na miujiza, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27 Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba#6:27 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi amemtia muhuri.”
28Ndipo wakamuuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?”
29 Isa akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.”
30 Hivyo wakamuuliza, “Utafanya ishara gani ya muujiza, ili tuione tukuamini? Utafanya jambo gani? 31 Baba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa, ‘Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.’ ”
32 Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Musa aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33 Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
34 Wakamwambia, “Bwana Isa, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.”
35 Isa akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe. 36 Lakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini. 37 Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na yeyote ajaye kwangu, sitamfukuzia nje kamwe. 38 Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. 39 Haya ndiyo mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho. 40 Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.”
41Wayahudi wakaanza kunung’unika kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” 42 Wakasema, “Huyu si Isa, mwana wa Yusufu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?”
43Hivyo Isa akawaambia, “Acheni kunung’unikiana ninyi kwa ninyi. 44Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho. 45 Imeandikwa katika Manabii, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Yeyote amsikilizaye Baba na kujifunza kutoka kwake, huyo huja kwangu. 46 Hakuna mtu yeyote aliyemwona Baba isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu, yeye ndiye peke yake aliyemwona Baba. 47 Amin, amin nawaambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele. 48 Mimi ni mkate wa uzima. 49 Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa. 50 Lakini hapa kuna mkate utokao mbinguni, ambao mtu yeyote akiula, hatakufa. 51 Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”
52 Ndipo Wayahudi wakaanza kuhojiana vikali wao kwa wao wakisema, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?”
53 Hivyo Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. 54 Mtu yeyote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho. 55Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56 Yeyote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake. 57 Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu. 58 Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.” 59Isa alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi#6:59 Nyumba ya ibada na mafunzo. huko Kapernaumu.
Wafuasi Wengi Wamwacha Isa
60 Wengi wa wafuasi wake waliposikia jambo hili wakasema, “Mafundisho haya ni magumu. Ni nani awezaye kuyapokea?”
61 Isa alipojua kwamba wafuasi wake wananung’unika kuhusu mafundisho yake, akawaambia, “Je, jambo hili limewaudhi? 62 Ingekuwaje basi kama mngemwona Mwana wa Adamu akipaa kwenda zake huko alipokuwa kwanza? 63 Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima. 64 Lakini baadhi yenu hamwamini.” Kwa maana Isa alifahamu tangu mwanzo wale ambao hawangemwamini miongoni mwao na yule ambaye angemsaliti. 65 Akaendelea kusema, “Hii ndiyo sababu niliwaambia kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.”
66 Tangu wakati huo wafuasi wake wengi wakarejea nyuma wakaacha kumfuata.
67 Hivyo Isa akawauliza wale wanafunzi wake kumi na wawili, “Je, ninyi pia mnataka kuondoka?”
68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana Isa, tuondoke twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. 69 Tunaamini na kujua kuwa wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu.”
70 Ndipo Isa akajibu, “Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Lakini mmoja wenu ni ibilisi.” 71 (Hapa alikuwa anasema juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili, ndiye ambaye baadaye angemsaliti Isa.)

Terpilih Sekarang Ini:

Yohana 6: NMM

Highlight

Kongsi

Salin

None

Ingin menyimpan sorotan merentas semua peranti anda? Mendaftar atau log masuk