Logótipo YouVersion
Ícone de pesquisa

Mwanzo 11

11
Mnara wa Babeli
1Wakati huo dunia yote ilikuwa na lugha moja na msemo mmoja. 2Watu walipoelekea upande wa mashariki, wakafika kwenye tambarare katika nchi ya Shinari#11:2 yaani Babeli, nao wakaishi huko.
3Wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tufyatue matofali na tuyachome vizuri kwa moto.” Walitumia matofali badala ya mawe, na lami kuunganisha hayo matofali. 4Ndipo wakasema, “Njooni, tujijengee mji wenye mnara ambao utafika hadi mbinguni, ili tujipatie jina, tusije tukatawanyika duniani kote.”
5Lakini Mwenyezi Mungu akashuka ili auone mji na mnara ambao wanadamu walikuwa wanaujenga. 6Mwenyezi Mungu akasema, “Ikiwa kama taifa moja wanaozungumza lugha moja wameanza kufanya hili, basi hakuna lolote watakalopanga kufanya ambalo halitawezekana kwao. 7Njooni, tushuke tuvuruge lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.”
8Hivyo Mwenyezi Mungu akawatawanya kutoka mahali pale waende duniani kote; nao wakaacha kuujenga huo mji. 9Ndiyo maana pakaitwa Babeli, kwa sababu hapo ndipo Mwenyezi Mungu alipoivuruga lugha ya dunia nzima. Kutoka hapo Mwenyezi Mungu akawatawanya duniani kote.
Vizazi vya Shemu hadi Abramu
(1 Nyakati 1:24-27)
10Hivi ndivyo vizazi vya Shemu.
Miaka miwili baada ya gharika, Shemu alipokuwa na umri wa miaka mia moja, akamzaa Arfaksadi. 11Baada ya kumzaa Arfaksadi, Shemu aliishi miaka mia tano, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
12Arfaksadi alipokuwa ameishi miaka thelathini na tano, akamzaa Shela. 13Baada ya kumzaa Shela, Arfaksadi aliishi miaka mia nne na tatu (403), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
14Shela alipokuwa ameishi miaka thelathini, akamzaa Eberi. 15Baada ya kumzaa Eberi, Shela aliishi miaka mia nne na tatu (403), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
16Eberi alipokuwa ameishi miaka thelathini na nne, akamzaa Pelegi. 17Baada ya kumzaa Pelegi, Eberi aliishi miaka mia nne na thelathini (430), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
18Pelegi alipokuwa ameishi miaka thelathini, akamzaa Reu. 19Baada ya kumzaa Reu, Pelegi aliishi miaka mia mbili na tisa (209), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
20Reu alipokuwa ameishi miaka thelathini na mbili, akamzaa Serugi. 21Baada ya kumzaa Serugi, Reu aliishi miaka mia mbili na saba (207), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
22Serugi alipokuwa ameishi miaka thelathini, akamzaa Nahori. 23Baada ya kumzaa Nahori, Serugi aliishi miaka mia mbili, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
24Nahori alipokuwa ameishi miaka ishirini na tisa, akamzaa Tera. 25Baada ya kumzaa Tera, Nahori aliishi miaka mia moja na kumi na tisa (119), akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
26Tera alipokuwa ameishi miaka sabini, akamzaa Abramu, na baadaye akawazaa Nahori na Harani.
Wazao wa Tera
27Hivi ndivyo vizazi vya Tera.
Tera aliwazaa Abramu, Nahori na Harani. Harani akamzaa Lutu. 28Tera alipokuwa bado hai, Harani akafa katika Uru ya Wakaldayo, nchi aliyozaliwa. 29Abramu na Nahori walioa. Mke wa Abramu aliitwa Sarai, naye mke wa Nahori aliitwa Milka; Milka na Iska walikuwa watoto wa Harani. 30Sarai alikuwa tasa, hakuwa na watoto.
31Tera akawachukua Abramu mwanawe, mjukuu wake Lutu mwana wa Harani, na Sarai mkwewe, mke wa Abramu mwanawe, wakatoka Uru ya Wakaldayo pamoja, wakaenda nchi ya Kanaani. Lakini walipofika Harani, wakaishi huko.
32Tera aliishi miaka mia mbili na mitano (205), akafa huko Harani.

Atualmente selecionado:

Mwanzo 11: NENO

Destaque

Partilhar

Copiar

None

Quer salvar os seus destaques em todos os seus dispositivos? Faça o seu registo ou inicie sessão