Luka 18
18
Kuomba pasipo kuchoka.
1Akawaambia mfano wa kwamba: Imewapasa kuomba siku zote pasipo kuchoka,#Rom. 12:12; Kol. 4:2; 1 Tes. 5:17. 2akasema: Katika mji fulani mlikuwa na mwamuzi asiyemwogopa Mungu, wala hakumcha mtu ye yote. 3Tena mle mjini mlikuwa na mwanamke mjane aliyemwendea mara kwa mara na kusema: Niamua na mpingani wangu! 4Lakini siku nyingi hakutaka; kisha akasema moyoni mwake: Ijapo, nisimwogope Mungu, wala nisimche mtu ye yote, 5Lakini kwa sababu ananisumbua, nitamwamulia mjane huyo, mwisho asije, akanipiga machoni.#Luk. 11:7-8. 6Bwana akasema: Sikilizeni, mwamuzi mwenye upotovu anavyosema! 7Naye Mungu asiwaamulie aliowachagua, wakimlilia mchana na usiku? Au atawakawilia? 8Nawaambiani: Atawaamulia upesi. Mwasemaje? Mwana wa mtu atakapokuja ataona wanaomtegemea nchini?#Rom. 16:20.
Fariseo na mtoza kodi.
9*Kulikuwa na watu waliojiwazia wenyewe kuwa waongofu, wakawabeza wengine, akawaambia mfano huu: 10Watu wawili walipanda kwenda Patakatifu kuomba. Wa kwanza alikuwa Fariseo, wa pili mtoza kodi. 11Fariseo akasimama, akaomba na kusema hivi moyoni mwake: Mungu, nakushukuru, kwa sababu sifanani na watu wengine walio wanyang'anyi, wapotovu, wagoni, wala sifanani na huyu mtoza kodi.#Yes. 58:2-3. 12Kila juma nafunga siku mbili, tena ninatoa fungu la kumi la vyote, ninavyovipata.#Mat. 23:23. 13Lakini mtoza kodi akasimama mbali, asitake hata kuyainua macho mbinguni, ila akajipiga kifua akisema: Mungu, nionee huruma mimi niliye mkosaji!#Sh. 51:3-6; Mat. 5:6. 14Nawaambiani: Huyu alishuka kwenda nyumbani kwake mwenye wongofu kuliko yule. Kwani kila anayejikweza mwenyewe atanyenyekezwa; naye anayejinyenyekeza mwenyewe atakwezwa.*#Luk. 14:11; Sh. 51:19; Mat. 23:12.
Kuwabariki watoto.
(15-17: Mat. 19:13-15; Mar. 10:13-16.)
15Wakamletea hata vitoto, awaguse. Lakini wanafunzi walipowaona waliwatisha. 16Ndipo, Yesu alipowaita, waje kwake, akisema: Waacheni vitoto, waje kwangu, msiwazuie! Kwani walio hivyo ufalme wa Mungu ni wao. 17Kweli nawaambiani: Mtu asiyeupokea ufalme wa Mungu kama kitoto hatauingia kamwe.#Mat. 18:3.
Mwenye mali nyingi.
(18-30: Mat. 19:16-29; Mar. 10:17-30.)
18Kulikuwa na mkubwa, akamwuliza akisema: Mfunzi mwema, nifanye nini, niurithi uzima wa kale na kale? 19Yesu akamwambia: Unaniitaje mwema? Hakuna aliye mwema, asipokuwa Mungu peke yake tu. 20Maagizo unayajua, ya kwamba: Usizini! Usiue! Usiibe! Usisingizie! Mheshimu baba yako na mama yako!#2 Mose 20:12-17. 21Naye akasema: Hayo yote nimeyashika, tangu nilipokuwa kijana. 22Yesu alipoyasikia akamwambia: Umesaza kimoja bado: vyote pia, ulivyo navyo, viuze, uvigawie maskini! Hivyo utakuwa na kilimbiko mbinguni. Kisha uje, unifuate!#Mat. 6:20. 23Lakini alipoyasikia haya, akasikitika sana, kwani alikuwa mwenye mali nyingi. 24Yesu alipomwona hivyo, akasema: Vitazameni vigumu vinavyowazuia waegemeao mali kuingia katika ufalme wa Mungu! 25Masumbuko ya ngamia ya kupenya tunduni mwa sindano ni madogo kuliko yake mwenye mali ya kuuingia ufalme wa Mungu. 26Wao waliosikia wakasema: Ikiwa hivyo, yuko nani awezaye kuokoka? 27Akasema: Mambo yasiyowezekana kwa watu huwezekana kwa Mungu.
Malipo.
28Petero akasema: Tazama, sisi tumeviacha vyetu vyote, tukakufuata wewe. 29Ndipo, alipowaambia: Kweli nawaambiani: Hakuna mtu aliyeacha nyumba au mkewe au ndugu au wazazi au wana kwa ajili ya ufalme wa Mungu, 30asiporudishiwa na kuongezwa mara nyingi siku hizi za kuwapo nchini; tena siku zile zitakazokuja ataupata nao uzima wa kale na kale.#Mar. 10:30.
Mwana wa mtu atateswa.
(31-34: Mat. 20:17-19; Mar. 10:32-34.)
31*Akawatwaa wale kumi na wawili, akawaambia: Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu. Huko Mwana wa mtu aliyoandikiwa na wafumbuaji yatatimizwa yote:#Luk. 9:22,44; Yes. 53. 32atatiwa mikononi mwa wamizimu, afyozwe nao pamoja na kutukanwa na kutemewa mate. 33Tena watampiga viboko, kisha watamwua. Naye siku ya tatu atafufuka. 34Lakini hao hawakuyasikia haya hata kidogo, neno hili likawa limefichika, wasilijue maana, wasiyatambue yaliyosemwa.#Mar. 9:32.
Kipofu wa Yeriko.
(35-43: Mat. 20:29-34; Mar. 10:46-52.)
35Ikawa, alipokaribia Yeriko, palikuwa na kipofu aliyekaa njiani kando akiomba sadaka. 36Aliposikia, kundi la watu linapita, akauliza: Kuna nini? 37Wakamsimulia, ya kuwa Yesu wa Nasareti anapita. 38Ndipo, alipopaza sauti akisema: Yesu, mwana wa Dawidi, nihurumie! 39Wao waliotangulia walipomkaripia, anyamaze, yeye akakaza sana kupaza sauti: Mwana wa Dawidi, nihurumie! 40Ndipo, Yesu aliposimama, akaagiza, aletwe kwake. Alipomfikia, akamwuliza: 41Wataka, nikufanyie nini? Naye akasema: Bwana, nataka, nipate kuona. 42Yesu akamwambia: Ona! Kunitegemea kwako kumekuponya.#Luk. 17:19. 43Papo hapo akapata kuona, akamfuata akimtukuza Mungu. Nao watu wote walioviona wakamsifu Mungu.
Trenutno izabrano:
Luka 18: SRB37
Istaknuto
Podijeli
Kopiraj
Želiš li da tvoje istaknuto bude sačuvano na svim tvojim uređajima? Kreiraj nalog ili se prijavi
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.