Luka 22
22
Yuda Iskariota.
(1-2: Mat. 26:1-5; Mar. 14:1-2.)
1Ikawa karibu sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, inayoitwa Pasaka. 2Nao watambikaji wakuu na waandishi wakatafuta, ndivyo wapate kumwangamiza. Maana walikuwa wakiwaogopa watu wa kwao.#Luk. 20:19.
(3-6: Mat. 26:14-16; Mar. 14:10-11.)
3Satani akamwingia Yuda anayeitwa Iskariota, naye alikuwa mwenzao wale kumi na wawili.#Yoh. 13:2,27. 4Akaenda zake, akasemezana nao watambikaji wakuu na wakubwa wa askari, ndivyo apate kumtia mikononi mwao. 5Wakafurahi, wakapatana naye fedha za kumpa. 6Ndipo, alipowaitikia waziwazi, akatafuta njia iliyofaa ya kumtoa, watu wasijue.
Kula Pasaka.
(7-23: Mat. 26,17-29; Mar. 14,12-25.)
7Ilipofika siku ya kula mikate isiyotiwa chachu, ndiyo siku iliyopasa kuchinja kondoo ya Pasaka,#2 Mose 12:18-20. 8akamtuma Petero na Yohana akisema: Nendeni, mtuandalie kondoo ya Pasaka, tupate kuila! 9Nao wakamwambia: Unataka, tukuandalie wapi? 10Akawaambia: Tazameni, mtakapoingia mjini mtakutana na mtu anayechukua mtungi wa maji, mfuateni mpaka nyumbani, atakamoingia! 11Mwambieni mwenye nyumba: Mfunzi anakuuliza: Kiko wapi chumba cha kukaa, ndimo niile kondoo ya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu? 12Ndipo, atakapowaonyesha chumba kikubwa kilichotandikwa, humo tuandalieni! 13Nao wakaenda, wakaona, kama alivyowaambia, wakaiandaa kondoo ya Pasaka.#Luk. 19:32.
Chakula cha Bwana.
14*Saa ilipofika, akaja kukaa chakulani, nao mitume wakakaa pamoja naye. 15Akawaambia: Nimetunukia sanasana kuila Pasaka hii pamoja nanyi, nikingali sijateswa bado. 16Kwani nawaambiani: Sitaila tena, mpaka patakapotimia katika ufalme wa Mungu.#Luk. 13:29. 17Kisha akatwaa kinyweo, akashukuru akisema: Mkitwae hiki, mgawiane wenyewe! 18Kwani nawaambiani: Tangu sasa sitayanywa tena mazao ya mizabibu, mpaka ufalme wa Mungu utakapokuja. 19Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema: Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyizeni hivyo, mnikumbuke!#1 Kor. 11:23-25. 20Vivyo hivyo akakitwaa nacho kinyweo, walipokwisha kula, akisema: Kinyweo hiki ndicho Agano Jipya katika damu yangu inayomwagwa kwa ajili yenu.* 21Lakini tazameni, mkono wa mwenye kunichongea upo hapa mezani pamoja nami!#Yoh. 13:21-22. 22Mwana wa mtu anakwenda njia yake, kama alivyotakiwa; lakini yule mtu, ambaye atachongewa naye, atapatwa na mambo. 23Nao wakaanza kuulizana wao kwa wao: Kwetu sisi yuko nani atakayelifanya jambo hilo?
Nani mkubwa?
(24-26: Mat. 20:25-27; Mar. 10:42-44.)
24Kukawa mabishano kwao ya kwamba: Kati yetu ni nani aliye mkubwa?#Luk. 9:46. 25Naye akawaambia: Wafalme wa mataifa huwatawala, nao wenye nguvu kwao huitwa mabwana wakubwa, 26lakini ninyi msiwe hivyo! Ila aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo, naye mwenye kuongoza na awe kama mwenye kutumika! 27Kwani aliye mkubwa ni yupi? Anayekaa chakulani au anayetumika? Si yule anayekaa chakulani? Lakini mimi kati yenu niko kama mwenye kutumika.#Yoh. 13:4-14. 28Nanyi ndinyi mlioandamana nami katika kujaribiwa kwangu. 29Kwa hiyo mimi nawawekea ninyi ufalme, kama Baba yangu alivyoniwekea mimi, 30mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu, nanyi mtakaa katika viti vya kifalme, myahukumu hayo mashina kumi na mawili ya Isiraeli.#Mat. 19:28.
Simoni Petero.
(31-34: Mat. 26:31-35; Mar. 14:27-31; Yoh. 13:36-38.)
31Simoni, Simoni, tazama, Satani amewataka ninyi, awapepete, kama wanavyopepeta ngano!#2 Kor. 2:11. 32Lakini mimi nimekuombea, kunitegemea kwako kusikome. Nawe hapo, utakapogukia, uwatie ndugu zako nguvu!#Sh. 51:15; Yoh. 17:11,15,20. 33Naye akamwambia: Bwana, nikiwa pamoja nawe niko tayari kwenda, ijapo iwe kifungoni, hata kufani. 34Naye akasema: Nakuambia, Petero: Jogoo hatawika leo, usipokwisha kunikana mara tatu kwamba: Simjui.
Panga mbili.
35Akawauliza: Nilipowatuma pasipo mfuko na mkoba na viatu, kulikuwako kitu, mlichokikosa? Wakasema: Hakuna hata kimoja.#Luk. 9:3. 36Akawaambia: Lakini sasa mwenye mfuko na autwae, na mkoba vilevile, naye mwenye kuukosa na auze nguo yake, anunue upanga! 37Kwani nawaambiani: Lile lililoandikwa sharti litimie kwangu mimi la kwamba:
Akahesabiwa kuwa mwenzao wapotovu;
kwani naliyoandikiwa hutimia.#Yes. 53:12; Mar. 15:28. 38Nao wakasema: Bwana, tazama, hapa ziko panga mbili! Naye akawaambia: Basi.
Getisemane.
(39-46: Mat. 26:30,36-46; Mar. 14:26,32-42.)
39*Kisha akatoka, akaenda mlimani pa michekele, kama alivyozoea, nao wanafunzi wake wakamfuata.#Yoh. 18:1. 40Alipofika pale akawaambia: Mwombe, msije kuingia majaribuni! 41Akaepukana nao na kuja mbali kidogo kama hapo, mtu anapotupa jiwe, akapiga magoti, akaomba akisema: 42Baba, ukitaka kipitishe kinyweo hiki, nisikinywe! Lakini yasifanyike, niyatakayo mimi, ila yafanyike uyatakayo wewe! 43Ndipo, malaika alipomtokea toka mbinguni, akamtia nguvu.#1 Fal. 19:5. 44Kisha akawa akigombana na kifo, kwa hiyo akajihimiza kuomba, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yaliyodondoka chini. 45Alipoinuka katika kuomba, akawajia wanafunzi, akawakuta, wamelala usingizi kwa sikitiko, 46akawaambia: Mbona mmelala usingizi? Inukeni, mwombe, msije kuingia majaribuni!*
Kutolewa na Yuda.
(47-53: Mat. 26:47-56; Mar. 14:43-49; Yoh. 18:2-11.)
47Angali akisema, mara wakaja kundi la watu, mmoja wao wale kumi na wawili, jina lake Yuda, akiwatangulia, akamkaribia Yesu kumnonea. 48Yesu akamwambia: Yuda, unamchongea Mwana wa mtu kwa kumnonea? 49Nao waliokuwa pamoja naye walipoyaona yatakayokuwapo, wakasema: Bwana, tuwapige kwa upanga? 50Mwenzao mmoja akampiga mtumwa wa mtambikaji mkuu, akamkata sikio la kuume. 51Lakini Yesu akajibu akisema: Waacheni, wamalize! Akamgusa sikio, akamponya. 52Kisha Yesu akawaambia waliomjia, wale watambikaji wakuu na wakuu wa Patakatifu na wazee: Mmetoka wenye panga na rungu, kama watu wanavyomwendea mnyang'anyi. 53Kila siku nilikuwa nanyi hapo Patakatifu, lakini hamkunyosha mikono, mnikamate. Lakini hii ndiyo saa yenu, ndipo, giza linaposhikia nguvu.#Yoh. 7:30; 8:20.
Kukana kwa Petero.
(54-62: Mat. 26:57,58,69-75; Mar. 14:53,54,66-72; Yoh. 18:12-18, 25-27.)
54*Walipokwisha kumkamata, wakampeleka, wamwingize nyumbani mwa mtambikaji mkuu. Lakini Petero akafuata mbalimbali. 55Walipowasha moto katikati ya ua na kukaa pamoja, naye Petero akaja kukaa katikati yao. 56Kijakazi alipomwona, akikaa penye mwangaza wa moto, akamkazia macho, akasema: Hata huyu alikuwa pamoja naye. 57Akakana akisema: Simjui, mama. 58Punde kidogo mwingine akamwona, akasema: Wewe nawe u mwenzao. Lakini Petero akasema: Mwenzangu, siye mimi. 59Saa moja ilipopita, mwingine akakaza kusema: Kweli hata huyu alikuwa pamoja naye, kwani ni Mgalilea. 60Lakini Petero akasema: Mwenzangu, sijui, unavyosema. Angali akisema, papo hapo jogoo akawika. 61Ndipo, Bwana alipomgeukia Petero, amtazame; hapo Petero akalikumbuka lile neno la Bwana, kama alivyomwambia: Jogoo atakapokuwa hajawika leo, utakuwa umenikana mara tatu.#Luk. 22:34. 62Akatoka nje, akalia sana kwa uchungu.*
Yesu anafyozwa.
(63-65: Mat. 26:67-68; Mar. 14:65.)
63*Wale waume waliomshika Yesu wakamfyoza na kumpiga, 64wakamfunika uso, wakamwuliza wakisema: Fumbua! Ni nani aliyekupiga? 65Hata masimango mengine mengi wakasema na kumtukana.
Mwana wa Mungu
(66-71: Mat. 26:59-66; Mar. 14:55-64.)
66Kulipokucha, wakakusanyika wazee wa kwao na watambikaji wakuu na waandishi, wakampeleka barazani kwa wakuu wao wote.#Yoh. 18:24. 67Wakasema: Tuambie, kama wewe ndiwe Kristo! Akawaambia: Nikiwaambia, hamtanitegemea; 68lakini nikiwauliza, hamtanijibu, wala hamtanifungua. 69Lakini tangu sasa Mwana wa mtu atakuwa amekaa kuumeni kwa nguvu ya Mungu.#Sh. 110:1. 70Ndipo, waliposema wote: Je? Ndiwe mwana wa Mungu? Naye akawaambia: Ninyi mnasema, kwani nimi ndiye. 71Nao wakasema: Ushuhuda tunautakia nini tena? Kwani wenyewe tumevisikia, anavyosema.*
Trenutno izabrano:
Luka 22: SRB37
Istaknuto
Podijeli
Kopiraj
Želiš li da tvoje istaknuto bude sačuvano na svim tvojim uređajima? Kreiraj nalog ili se prijavi
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.