1 Nyakati 11
11
Daudi atawazwa mfalme wa Israeli
(2 Samweli 5:1-10)
1Waisraeli wote walimjia Daudi kwa pamoja huko Hebroni, wakamwambia, “Sisi ni mwili wako na damu yako. 2Zamani, wakati Sauli alikuwa mfalme, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani, naye Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’ ”
3Wazee wote wa Israeli walipokuwa wamewasili kwa Mfalme Daudi huko Hebroni, alifanya mapatano nao huko Hebroni mbele za Mwenyezi Mungu, nao wakampaka Daudi mafuta awe mfalme wa Israeli, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu aliloahidi kupitia kwa Samweli.
Daudi ateka Yerusalemu
4Daudi na Waisraeli wote wakaenda Yerusalemu (ndio Yebusi). Nao Wayebusi walioishi humo 5wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu.” Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.
6Daudi alikuwa amesema, “Yeyote atakayeongoza mashambulizi dhidi ya Wayebusi atakuwa jemadari mkuu.” Yoabu mwana wa Seruya akawa wa kwanza kukwea, naye akawa mkuu.
7Daudi akafanya makao yake kwenye ngome, hivyo ukaitwa Mji wa Daudi. 8Akajenga mji pande zote, kuanzia Milo hadi kwenye ukuta kuzunguka; wakati huo huo Yoabu akajenga sehemu zingine zilizobaki za Yerusalemu. 9Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni alikuwa pamoja naye.
Mashujaa wa Daudi
(2 Samweli 23:8-39)
10Hawa walikuwa wakuu wa mashujaa wa Daudi: wao pamoja na Waisraeli wote wakauimarisha ufalme wake ili kuenea katika nchi yote, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu aliloahidi. 11Hii ndio orodha ya mashujaa wa Daudi:
Yashobeamu Mhakmoni alikuwa mkuu wa maafisa; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia tatu, aliowaua katika pambano moja.
12Aliyefuata alikuwa Eleazari, mwana wa Dodai Mwahohi, mmoja wa wale mashujaa watatu. 13Huyo alikuwa pamoja na Daudi huko Pas-Damimu, wakati Wafilisti walikusanyika huko kwa ajili ya vita. Mahali palipokuwa na shamba limejaa shayiri, vikosi vya Israeli vikawakimbia Wafilisti. 14Lakini Eleazari na Daudi wakasimama imara katikati ya lile shamba, nao wakalishindania na kuwaua Wafilisti. Naye Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa.
15Wakuu watatu miongoni mwa wale thelathini walimwendea Daudi kwenye mwamba, katika pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti walikuwa wamepiga kambi katika Bonde la Warefai. 16Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu. 17Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilichoko karibu na lango la Bethlehemu!” 18Kwa hivyo wale watatu, wakapita katikati ya safu za Wafilisti, wakachota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini yeye akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Mwenyezi Mungu. 19Akasema, “Mungu apishie mbali kwamba nifanye hivi! Je kweli, niinywe damu ya watu hawa waliohatarisha maisha yao?” Kwa sababu walihatarisha maisha yao kuyaleta yale maji, Daudi hakukubali kuyanywa.
Huo ndio uliokuwa ujasiri wa wale mashujaa watatu.
20Abishai, ndugu yake Yoabu ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia tatu, ambao aliwaua; kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu. 21Alitunukiwa heshima maradufu ya wale Watatu, akawa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao.
22Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba. 23Alimuua Mmisri aliyekuwa na urefu kama dhiraa tano#11:23 Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25.. Ingawa huyo Mmisri alikuwa na mkuki kama mti wa mfumaji mkononi, Benaya alimwendea na rungu. Akamnyang’anya Mmisri mkuki wake na kumuua nao. 24Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu. 25Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu: Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.
26Wale mashujaa walikuwa:
Asaheli nduguye Yoabu,
Elhanani mwana wa Dodo kutoka Bethlehemu,
27Shamothi Mharori,
Helesi Mpeloni,
28Ira mwana wa Ikeshi kutoka Tekoa,
Abiezeri kutoka Anathothi,
29Sibekai Mhushathi,
Ilai Mwahohi,
30Maharai Mnetofathi,
Heledi mwana wa Baana Mnetofathi,
31Itai mwana wa Ribai kutoka Gibea ya Benyamini,
Benaya Mpirathoni,
32Hurai kutoka mabonde ya Gaashi,
Abieli Mwaribathi,
33Azmawethi Mbaharumi,
Eliaba Mshaalboni,
34wana wa Hashemu Mgiloni,
Yonathani mwana wa Shagee Mharari,
35Ahiamu mwana wa Sakari Mharari,
Elifale mwana wa Uru,
36Heferi Mmekerathi,
Ahia Mpeloni,
37Hezro Mkarmeli,
Naarai mwana wa Ezbai,
38Yoeli nduguye Nathani,
Mibhari mwana wa Hagri,
39Seleki Mwamoni,
Naharai Mbeerothi, mbeba silaha wa Yoabu mwana wa Seruya,
40Ira Mwithiri,
Garebu Mwithiri,
41Uria Mhiti,
Zabadi mwana wa Alai,
42Adina mwana wa Shiza Mreubeni, aliyekuwa mkuu wa Wareubeni, akiwa pamoja na watu thelathini,
43Hanani mwana wa Maaka,
Yoshafati Mmithni,
44Uzia Mwashterathi,
Shama na Yeieli wana wa Hothamu Mwaroeri,
45Yediaeli mwana wa Shimri,
nduguye Yoha Mtizi,
46Elieli Mmahawi,
Yeribai na Yoshavia wana wa Elnaamu,
Ithma Mmoabu,
47Elieli, na Obedi na Yaasieli Mmesobai.
Iliyochaguliwa sasa
1 Nyakati 11: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.