1 Nyakati 12
12
Mashujaa waungana na Daudi
1Hawa ndio watu waliomjia Daudi huko Siklagi, wakati alikuwa amefukuzwa mbele ya Sauli mwana wa Kishi (walikuwa miongoni mwa mashujaa waliomsaidia Daudi vitani. 2Walikuwa na pinde na walikuwa na uwezo wa kupiga mishale au kutupa mawe kwa kombeo wakitumia mkono wa kushoto au wa kulia. Hawa walikuwa ndugu zake Sauli kutoka kabila la Benyamini):
3Mkuu wao alikuwa Ahiezeri, na wa pili Yoashi, wote wana wa Shemaa Mgibeathi;
pia Yezieli na Peleti wana wa Azmawethi;
Beraka, Yehu Mwanathothi, 4na Ishmaya Mgibeoni, shujaa miongoni mwa wale Thelathini, aliyekuwa kiongozi wa wale Thelathini;
Yeremia, Yahazieli, Yohanani, Yozabadi Mgederathi, 5Eluzai, Yerimothi, Bealia, Shemaria, Shefatia Mharufi;
6Elkana, Ishia, Azareli, Yoezeri na Yashobeamu wana wa Kora;
7Yoela na Zebadia, wana wa Yerohamu kutoka Gedori.
8Baadhi ya Wagadi wakajitenga na kujiunga na Daudi katika ngome yake huko jangwani. Walikuwa mashujaa hodari, wakiwa wamejiandaa kwa vita, na wenye uwezo wa kutumia ngao na mkuki. Nyuso zao zilikuwa nyuso za simba na walikuwa na wepesi kama paa milimani.
9Ezeri alikuwa mkuu wao,
Obadia alikuwa wa pili katika uongozi, Eliabu wa tatu,
10Mishmana wa nne, Yeremia wa tano,
11Atai wa sita, Elieli wa saba,
12Yohanani wa nane, Elzabadi wa tisa,
13Yeremia wa kumi, na Makbanai wa kumi na moja.
14Hawa Wagadi walikuwa majemadari. Aliyekuwa mdogo alikuwa kama watu mia moja, naye aliyekuwa mkuu alikuwa kama watu elfu moja. 15Hao ndio walivuka Mto Yordani katika mwezi wa kwanza ukiwa umefurika hadi kwenye kingo zake zote, wakawatorosha watu wote walioishi kwenye mabonde, kuelekea mashariki na magharibi.
16Wabenyamini wengine na baadhi ya watu kutoka Yuda pia walikuja kwa Daudi katika ngome yake. 17Daudi akatoka nje kuwalaki na akawaambia, “Kama mmekuja kwangu kwa amani, kunisaidia, mimi niko tayari kuwaruhusu ninyi kuungana nami. Lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa adui zangu wakati mikono yangu haina hatia, basi Mungu wa baba zetu aone na awahukumu.”
18Kisha Roho wa Mungu akaja juu ya Amasai, mkuu wa wale Thelathini, naye akasema:
“Sisi tu watu wako, ee Daudi!
Nasi tuko pamoja na wewe, ee mwana wa Yese!
Amani, naam, amani iwe kwako,
pia amani kwa wale walio upande wako,
kwa kuwa Mungu wako atakusaidia.”
Kwa hiyo Daudi akawapokea na kuwafanya viongozi wa vikosi vyake vya uvamizi.
19Baadhi ya watu kutoka kabila la Manase wakajiunga na Daudi alipoenda pamoja na Wafilisti kupigana na Sauli. (Daudi na watu wake hawakuwasaidia Wafilisti kwa sababu baada ya ushauri, watawala wao walimrudisha. Wakasema, “Itatugharimu vichwa vyetu kama Daudi atatuasi na kurudi kwa Sauli bwana wake.”) 20Daudi alipoenda Siklagi, hawa ndio wanaume wa kabila la Manase waliojiunga naye: Adna, Yozabadi, Yediaeli, Mikaeli, Yozabadi, Elihu na Silethai, viongozi wa vikosi vya watu elfu moja katika kabila la Manase. 21Walimsaidia Daudi dhidi ya makundi ya uvamizi, kwa kuwa wote walikuwa mashujaa hodari na walikuwa majemadari katika jeshi lake. 22Siku baada ya siku watu walikuja kumsaidia Daudi, hadi akawa na jeshi kubwa, kama jeshi la Mungu.
Wengine waungana na Daudi huko Hebroni
23Hawa ndio watu waliojiandaa kwa ajili ya vita waliokuja kwa Daudi huko Hebroni ili kumtwalia ufalme kutoka kwa Sauli, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema:
24watu wa Yuda, wanaochukua ngao na mikuki walikuwa elfu sita na mia nane wakiwa tayari kwa vita.
25Watu wa Simeoni, mashujaa waliokuwa wamejiandaa kwa vita, walikuwa elfu saba na mia moja.
26Watu wa Lawi walikuwa elfu nne na mia sita, 27pamoja na Yehoyada, kiongozi wa jamaa ya Haruni, aliyekuwa na watu elfu tatu na mia saba, 28na Sadoki, kijana shujaa hodari, aliyekuwa na maafisa ishirini na wawili kutoka jamaa yake.
29Watu wa Benyamini, ndugu zake Sauli, walikuwa elfu tatu; wengi wao walikuwa wameendelea kuwa waaminifu kwa Sauli hadi wakati huo.
30Watu wa Efraimu, mashujaa hodari elfu ishirini na mia nane, watu waliokuwa maarufu katika koo zao.
31Watu wa nusu ya kabila la Manase, waliotajwa kwa majina ili waje kumweka Daudi kuwa mfalme, watu elfu kumi na nane.
32Watu wa Isakari, waliofahamu majira na kujua kile ambacho Israeli inapasa kufanya, walikuwa viongozi mia mbili, pamoja na jamaa zao wote chini ya uongozi wao.
33Watu wa Zabuloni, wapiganaji hodari, tayari kwa vita wakiwa na silaha za kila aina, ili kumsaidia Daudi kwa uaminifu thabiti, walikuwa elfu hamsini.
34Watu wa Naftali, maafisa elfu moja, pamoja na watu elfu thelathini na saba wenye ngao na mikuki.
35Watu wa Dani, elfu ishirini na nane na mia sita waliokuwa wamejiandaa kwa vita.
36Watu wa Asheri, wapiganaji hodari elfu arobaini waliokuwa wameandaliwa kwa vita.
37Na pia watu kutoka mashariki mwa Yordani, watu wa Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase, wakiwa na kila aina ya silaha, walikuwa elfu mia moja na ishirini.
38Wote hawa walikuwa wapiganaji waliojitolea kutumika katika jeshi.
Walikuja Hebroni wakiwa wameamua kikamilifu kumfanya Daudi mfalme juu ya Israeli yote. Waisraeli wengine wote walikuwa pia na nia hiyo moja ya kumfanya Daudi kuwa mfalme. 39Watu hawa wakakaa huko na Daudi siku tatu, wakila na kunywa, kwa sababu jamaa zao zilikuwa zimewapatia mahitaji yao. 40Pia, majirani zao hata wale walio mbali hadi Isakari, Zabuloni na Naftali, walikuja wakiwaletea vyakula walivyovibeba kwa punda, ngamia, nyumbu na maksai. Kulikuwa na wingi wa unga, maandazi ya tini, maandazi ya zabibu kavu, divai, mafuta, ng’ombe na kondoo, kwa maana kulikuwa na furaha katika Israeli.
Iliyochaguliwa sasa
1 Nyakati 12: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.