Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Nyakati 14

14
Nyumba ya Daudi na jamaa yake
(2 Samweli 5:11-16)
1Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mwerezi, waashi na maseremala ili kumjengea jumba la kifalme. 2Naye Daudi akatambua kwamba Mwenyezi Mungu amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na kwamba ufalme wake umetukuzwa kwa ajili ya Israeli, watu wake.
3Huko Yerusalemu Daudi akaoa wake wengine zaidi na akawa baba wa wana wengi wa kiume na wa kike. 4Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Sulemani, 5Ibihari, Elishua, Elpeleti, 6Noga, Nefegi, Yafia, 7Elishama, Beeliada na Elifeleti.
Daudi awashinda Wafilisti
(2 Samweli 5:17-25)
8Wafilisti waliposikia kuwa Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli yote, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akatoka ili kwenda kukabiliana nao. 9Basi Wafilisti walikuwa wameingia na kushambulia Bonde la Warefai, 10Hivyo Daudi akamuuliza Mungu: “Je, niende kuwashambulia hao Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?”
Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nenda, nitawatia mikononi mwako.”
11Hivyo Daudi pamoja na watu wake wakakwea hadi Baal-Perasimu, akawashinda huko. Akasema, “Kama maji yanavyofurika, Mungu amewafurikia adui zangu kwa kutumia mkono wangu.” Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Baal-Perasimu. 12Wafilisti walikuwa wametupa miungu yao huko, naye Daudi akaamuru iteketezwe kwa moto.
13Kwa mara nyingine Wafilisti wakavamia lile bonde; 14hivyo Daudi akamuuliza Mungu tena, naye Mungu akamjibu, “Usiwafuate moja kwa moja, bali wazungukie na uwashambulie kutoka mbele ya hiyo miti ya miforosadi. 15Mara utakaposikia sauti ya kutembea vileleni vya miti ya miforosadi, basi utoke upigane vita, kwa sababu hiyo itaonesha kwamba Mungu amekutangulia ili kupiga jeshi la Wafilisti.” 16Kwa hiyo Daudi akafanya kama alivyoagizwa na Mungu, wakalipiga jeshi la Wafilisti kuanzia Gibeoni hadi Gezeri.
17Hivyo umaarufu wa Daudi ukaenea katika kila nchi, naye Mwenyezi Mungu akayafanya mataifa yote kumwogopa Daudi.

Iliyochaguliwa sasa

1 Nyakati 14: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia